Header Ads

WABUNGE TUMIENI VIZURI KINGA YENU

Na Happiness Katabazi
IBARA ya 100(1)ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inasema hivi “ Kutakuwa na uhuru wa mawazo,majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano,au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.
Ibara 100(2) inasema “ Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika. Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta Bungeni kwa njia ya maombi,muswada,hoja au vinginevyo”. Leo nimelazimika kuanza makala hii kwa kutumia nukuu hiyo ya Ibara ya Katiba ya nchi, kwani kadri siku zinavyo zidi kwenda baadhi ya wabunge wetu wakiitumia kinga hiyo vibaya kinyume na makusudio ya ibara hiyo. Kwani hivi sasa tunaona baadhi ya wabunge wetu wawapo bungeni wanakwepa kabisa kuzungumzia kero za majimbo yao walizotumwa na wapiga kura wao badala yake wameamua kujikita zaidi kwa kuwakile wanachokiita kuwalipua wenzao kuwa ambao wengine hata sio wabunge tena kwa kuwataja majina na nyadhifa zao wakiwahusisha na makosa mbalimbali na kuitimisha kwa kusema wanao ushahidi wa tuhuma hizo. Sitaki kuwataja kwa majina wabunge ambao majimbo yao yanakero lukuki lakini wawapo bungeni hawazizungumzii kero hizo kabisa kutwa utawasikia ,wanaomba mwongozo wa Spika,utaratibu, mwekezaji,au afisa fulani wa serikali ni fisadi,tunaomba bunge lituruhusu tujadili ajali ya meli iliyotokea wiki iliyopita wakati wataalamu walitueleza bado wanaendelea na uchunguzi wa chanzo cha Boti iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kuzama. Kwa kweli uwa nasikia hasira na kichefuchefu pindi nisikiapo wabunge wa aina hiyo wanaongea maneno hayo bungeni.Hivi unajadili ajali ya boti ambayo hata chanzo chake bado kilikuwa hakijulikani ,hukuwepo eneo la tukio, unajadili nini kama sio uwendawazimu na matumizi mabaya ya muda wa bunge ambalo linaendeshwa kwa kodi za wananchi? Hivi hiyo ajali hiyo ya boti imewauma sana hadi mnataka muijadili kuliko shida za wapiga kura wenu ambao wanakabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama,uhaba wa vyumba vya kujifungulia wajawazito? Hivi wapiga kura wenu mlikaa nao saa ngapi na wapi wakawatuma muende kujadili ajali hiyo ya meli iliyotokea wiki iliyopita?Mambo mnayotumwa tena kwa maandishi mkawaseme bungeni wala hatusikii mkishupaza shingo,mkitishia kususia vikao vya bunge kama kero za majimbo yenu hazitajadiliwa na bunge hilo. Nyie baadhi ya wabunge mnaowatuhumu wabunge wenzenu na wananchi wengine ambao si wabunge kuwa ni mafisadi, hivi nyie mnausafi gani maana nanyie vile vile mkae mkijua mmejificha kwenye mawingu ,mnaonekana na watu wanaowaona na nyie wanawashuhudia kuwa siyo wasafi hata kidogo ,ni wachafu na wengi mnadaiwa mlitumia hila,husuda katika kushinda ubunge. Imeanza kuwa mila na desturi sasa mbunge ambaye ni mtunga sheria anapata taarifa za uhalifu kabla vikao vya bunge havijaanza ,hizo taarifa anazikalia anasuburi kipindi cha bunge la bajeti kikifika akipata fursa ya kuchangia bajeti ya wizara fulani, ndiyo utamsikia mbunge huyo eti akijinasibu anazo taarifa za kutendeka kwa uhalifu na ofisa fulani. Uwa nasikitika sana ninapomwona mbunge anazungumza tuhuma hizo ndani ya bungeni, kwasababu kifungu cha nane cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, inasema kutokufahamu sheria siyo kinga ya kutokuadhibiwa na Kifungu cha saba cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, kinasema kila mtu ambaye ana taarifa za kutaka au kutendeka kwa kosa ,mtu huyo anapaswa atoe taarifa katika mamlaka husika. Sasa na shangazwa na wabunge hao ambao ndiyo watunga sheria wetu wanashindwa kutimiza kwa vitendo matakwa ya vifungu hivyo vya sheria. Hivi bunge siku hizi ndiyo limegeuka kuwa kituo cha polisi au mahakama?Maana polisi ndiyo inapokea taarifa na kuzichunguza na kukamata na mahakama nayo ndiyo inasikiliza mashitaka na kutolea maamuzi sasa tuwaulize nyie wabunge waropokaji , mnavyokalia hizo taarifa za ubadhirifu bila kuzipeleka TAKUKURU,Polisi,Uhamiaji mnazipelekea bungeni mnaajenda gani? Maana taifa hili hivi sasa limekuwa na aina ya wanasiasa wengi uchwara ,wasiyotaka kukaa chini na changanua mambo kwa mapana yake na kuyafanyiakazi matokeo yake wanaibua hoja zisizoendelevu ambazo hazitufundishi chochote sisi wananchi zaidi ya hoja hizo zimekuwa na malengo ya kulipizana visazi na kuumizana kisiasa na kujitafutia uaamuru wa chee wa kisiasa.Ni upuuzi. Na matokeo ya kuwa na aina hii ya wanasiasa ambao jukumu la kufikiri sawa sawa ni jinsi gani wataweza kuliletea taifa letu maendeleo makubwa ,ndiyo maana tunashuhudia hivi sasa aina hii ya wanasiasa uchwara wa hapa nchini anakaa katika madaraka ya kibunge au uwaziri kwa kipindi kifupi sana ukilinganisha na awamu za serikali zilizopita. Kutwa baadhi ya wabunge wetu wawapo bungeni wamegeuka kuwa kama waimbaji wa miziki ya Mipasho ,mbunge huyu kamtuhumu mbunge wa chama kile ,mbunge huyu kakituhumu mbunge Yule.Yaani tafrani. Hivi hiyo mipasho na vijembe vyenu mnavyorushiana na kususia vikao vya bunge kwasababu ajenda zenu hazijakubaliwa na spika zinatusaidia nini sisi wapiga wenu?Jibu ni jepesi havitusaidii chochote.Ningewaona wamaana mnaposusia kikao cha bunge ,msuse na kupokea posho,sio mnasusia kikao cha bunge halafu posho mnapokea. Umefika wakati sasa kwa Watanzania wote tunaofikiri sawa sawa na kuitakia mema taifa letu kujitokeza kwa wingi kwenda kutoa maoni yenu kwenye Tume ya Kukusanya maoni ya marekebisho ya Katiba na kutoa maoni yetu,ikiwemo kutoa maoni ya kuwa hiyo ibara ya 100(1,2),ifanyiwe marekebisho kidogo na badala yake kiongezwe kipengele cha kukataza wabunge wasijadili tuhuma za mtu fulani ambazo hawana ushahidi nazo na endapo mbunge atajadili tuhuma hasizo na ushahidi nazo Yule aliyetuhumiwa awe na mamlaka ya kumshitaki mbunge huyo,naamini tabia ya wabunge kudhulia wenzao uongo ndani ya bunge itakoma. Na sisi watanzania wengi tulivyo tunakasumba moja mbaya sana tuhuma dhidi ya mtu fulani zinapotolewa leo hata kama hazina uthibitisho basi hizo taarifa ndiyo nzinaaminiwa na wananchi wengi hata ikija kutokea mbele ya safari tuhuma hizo siyo za kweli tayari mtu huyo jina lake limekuwa limeshachafuka na jamii itamchukulia kuwa mtu huyo ni mchafu. Kinga hiyo ya wabunge wawapo bungeni hawawezi kushitakiwa tunaona inaanza kutumika ndivyo sivyo, hivyo ni vyema basi ibara hiyo inayowapatia kinga hiyo ikabadilishwa na kuongezwa makali licha uhuru wao wa kujadili ndani ya bunge uwepo ila uwe na mipaka. Uhuru usitukime vibaya kwaajili ya kupakana matope,kushushia heshima na kujitafutia umaarufu chetu na wanasiasa wetu. Kumbukeni Bunge ni mhimili wenye heshima yake lakini kadri siku zinavyokwenda, tunashuhudia matamshi, matendo,hoja zinalishushia heshima bunge letu taratibu. Kumbukeni wabunge, spika mmekabidhiwa bunge hilo kuliongoza,bunge likiwa ni bunge lenye heshima na taadhima lakini hali ilivyo hivi sasa kwa wakati fulani haipendezi. Wakati bado mnao jisahiisheni ,jitambueni nyie ni watu wazima mmepewa dhamana na wananchi kuwawakilisha katika bunge sasa mnapofanya mambo yasiyonajita kwa taifa na wananchi wa ujumla,mkae mkijua mnajishushia heshima na bunge letu litadharauliwa na hata nyingine. Mungu ibariki Tanzania,mungu ibariki Afrika 0716 774494 www.katabazihappy.blogspot.com Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 24 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.