Header Ads

UNFPA YAWAFUNDA WANAHABARI

Na Happiness Katabazi SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), limewaasa waandishi wa habari nchini kuandika na kuchapisha kwa wingi habari zinazohusu afya ya uzazi wa mpango na idadi ya watu ili kujenga jamii iliyo na elimu ya afya ya uzazi wa mpango. Hayo yalisemwa jana na mwakilishi msaidizi wa UNFPA-Tanzania, Dk. Rutasha Dadi wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari ya afya ya uzazi wa mpango na siku ya idadi ya watu duniani ambayo hufanyika Julai 11 kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu kitaifa itaadhimishwa mkoani Morogoro. Dk. Dadi alisema faida ya taifa kuwa na watu wanaopanga uzazi ni kubwa kwani endapo watakuwa wanapanga itawaepusha kupata mimba zisizotarajiwa na maradhi ya kuambukiza, ikiwamo ukimwi, vifo vya mama wajawazito na watoto. “Mwisho wa siku taifa na dunia kwa ujumla litajikuta likipoteza nguvu kazi yake kwa kukosa elimu na huduma ya afya ya uzazi wa mpango,” alisema Dk. Dadi. Aliongeza kuwa Tanzania ni nchi ambayo imeridhia watu wake watumie huduma za mpango, kwa kiasi kikubwa watu hao wamekuwa wakitumia huduma hiyo licha ya kwamba bado kuna changamoto katika eneo hilo na kuongeza kuwa vyombo vya habari vinatakiwa vishiriki kikamilifu kuuelimisha umma kuhusu umuhimu wa afya ya uzazi wa mpango. Alizitaja changamoto hizo kuwa ni imani za kidini, uelewa finyu wa baadhi ya wananchi kuhusu elimu hiyo, hali inayosababisha baadhi ya watu kupoteza maisha. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne Julai 5 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.