Header Ads

MARANDA,FARIJALA WAFUNGWA JELA TENA

Na Happiness Katabazi MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwa mara ya pili tena imemuhukumu Kada wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Rajabu Maranda na mpwa wake Farijala Hussein imewahukumu kwenda jela miaka mitatu kila mmoja kwasababu imewakuta na hatia ya makosa sita likiwemo kosa la kujipatia Shilingi bilioni mbili kwa njia ya udanganyifu toka katika Akaunti ya Madeni ya Nje(EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania kwa njia ya udanganyifu. Sambamba na kutiwa hatiani na mahakama hiyo pia Mwenyekiti wa jopo la Mahakimu Wakazi waliokuwa wakisikiliza kesi Jaji Fatma Masengi alitoa hukumu yake peke yake inayotofautiana na wanajopo wenzie ambao ni Hakimu Mkazi Projest Kayohza na Catherine Revocate ambayo iliwaachiria huru washitakiwa na ambapo hukumu ya Jaji Masengi imebaki kuwa katika kumbukumbu za mahakama na hukumu ya mahakama ni ile iliyotolewa na mahakimu hao wawili kwasababu sheria inasema wengi wape. Hakimu Kahyoza akisoma hukumu hiyo ya mahakama alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo waliyokuwa wakiitolea hukumu ni kesi ya jinai Na.1163/2008 ambao washitakiwa hao waliokuwa wakitetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu na upande wa Jamhuri uliokuwa ukiwakilishwa na mawakili waandamizi wa serikali Arafa Msafiri na Vitalis Timoth walikuwa wakikabiliwa na jumla ya makosa saba. Aliyataja makosa hayo kuwa ni kula njama kuidanganya BoT kinyume na kifungu cha 306 ambalo wanadaiwa kulitenda Machi 22 mwaka 2005 na 2006, Kugushi hati ya jina la usajili wa jina la Biashara la Money Planner Consultant na kuonyesha hati hiyo imetolewa na BRELA huku akijua sikweli kinyume na kifungu cha 333,335(c,d(i),337, kosa la tatu hadi la tano ni la kuwasilisha nyaraka zilizogushiwa kinyume na kifungu 342, wizi wa shilingi milioni 660 kinyume na kifungu cha 258 na 265 na kosa la saba ni la kujipatia Shilingi bilioni mbili toka BoT kwa njia ya udanganyifu,vifungu vyote hivyo ni vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002. Alisema katika kuthibitisha kesi hiyo upande wa jamhuri ulileta mashahidi saba ambao Ofisa Mwandamizi toka ofisi (BRELA), Noel Shani, Saul Kisai , Mrakibu Mwandamizi wa Polisi(SSP), Safael Nkonyi ,ofisa mwandamizi toka Benki ya Taifa ya Biashara, Laison Mwakapenda,Johanes Kagendi ambaye ndiyo aliyekuwa mtaalamu wa maandishi toka jeshi la Polisi ambaye ndiye aligundua hati hizo zilikuwa zimegushiwa na washitakiwa, Sijo Frenanends toka iliyokuwa Benki ya Biashara Afrika na Johanes Boaz toka BoT ambaye katika ushahidi wake alieleza kuwa washitakiwa hao waliwasilisha maombi yao ya kutaka walipwe kiasi hicho cha fedha na BoT ambapo waliwasilisha hati hiyo ya jina la usajili na hati ya kuamisha deni inayoonyesha kampuni ya B.Grancel ya Ujerumani imeipatia idhini kampuni ya washitakiwa ya Money Planner Consultance ya Tanzania idhini ya kudai deni lake la shilingi bilioni mbili BoT na kwamba maombi hayo yalifuata taratibu zote na BoT iliwalipa kiasi hicho cha fedha washitakiwa hao. Na kwa upande wa washitakiwa hawakuleta shahidi mashahidi walikuwa ni wao wawili tu. “Baada ya kupitia hayo yote hapo juu tunafikiri hoja za kutolea uamuzi ni saba ambayo nitazitaja kama ifuatavyo: Kama washitakiwa walikula njama kuibia BoT?, kama walighushi hati ya usajili wa jina la biashara Na.150731 kwa jina la Money Planners &Consaltance? , kama walighushi hati ya kuamisha deni (deed of assignment kati ya kampuni ya B.Grancel ya Ujerumani na Money Planners&Consultance ya Tanzania?, kama waliwasilisha nyaraka hizo zilizoghushiwa Benki ya Biashara ya Afrika na BoT? na kama walijipatia shilingi biloni 1.6 toka Benki Kuu?”alisema Hakimu Kahyoza. Akianza kuichambua kuzichambua hoja hizo huku akionyesha umakini wa hali ya juu alisema anaanza kuichambua hoja ya pili ambayo ni kama washitakiwa walitenda kosa la kughushi,alisema upande wa jamhuri ulileta vielelezo kuonyesha washitakiwa walipata jina la usajili la Money Planer s&Consultance Machi 22 mwaka 2005 toka BRELA ambayo inaonyesha pia ilikuwa ikimilikiwa na Paul Nyengo na Fundi Ashei na nyaraka zote zinaonyesha ofisi ya jina hilo la kampuni iliyokuwa na Paul na Fundi katika ofisi zake zilizopo Magomeni Mapipa mtaa wa Iramba nyumba Na.7,wakati washitakiwa na watu hao wawili ni watu tofauti na mahakama imeona hiyo siyo hali ya kawaida na watu wawili tofauti kuwa na kampuni yenye jina linalofanana na ofisi za kampuni hiyo kuwa katika mtaa na namba ya nyumba zinazofanana na jina hilo linaonyesha limetolewa na BRELA kwa watu hao wawili tofauti. “Mshitakiwa wa kwanza Farijala katika utetezi wake alidai ni yeye ndiye aliyepelea BRELA ombi la mabadiliko ya jina la biashara …kwa kujichanganya changa huko mahakama hii inakubaliana na mtaalamu wa maandishi Kagendi saini zilizokuwa katika hati ya usajili wa jina la biashara ziligushiwa na Maranda katika utetezi wake alidai ni Fundi ndiye aliyepeleka maombi ya mabadiliko ya jina BRELA hazikusainiwa na shahidi wa kwanza Noel Shani ambaye ni Afisa wa BRELA, na kwamba zilisainiwa bila ridhaa yake ni wazi nyaraka hizo zimegushiwa na zimekutwa mikoni mwa washitakiwa hivyo mahakama hii imewakutana na hatia katika kosa la kughushi”alisema Hakimu Kahyoza. Akilichambua hoja ya tatu, alisema hiyo hati ya kuamisha deni inayoonyesha imetoka kampuni ya B.Grancey ya Ujerumani na Money planners&Consultance inaonyesha imesainiwa na mwakili wa kampuni hiyo ya Ujerumani na kwa upande wa Tanzania hakuisaini na hata hivyo aliyepaswa aisaini ni Paul Nyengo au Fundi Ayeshi ambayo hata hivyo ni majina ya kufikirika na hata hivyo kisheria hiyo hati ya kuamishia deni ni batili na haikupaswa kukubaliwa na benki kuu kwani ilisaniwa na upande mmoja badala ya kusainiwa na pande mbili za kampuni hiyo, hivyo mahakama hii kwa kauli moja imefikia uamuzi wa kuona hati hiyo ilighushiwa na washitakiwa kwani ilikutwa mikononi mwao na ni washitakiwa ndiyo waliitumia hati hiyo ya kuamishia deni kuipeleka BoT na kuifungulia akanti katika Benki ya Biashara ya Afrika. Hakimu Kahyoza akiijadili hoja nne ambayo ni kama washitakiwa waliwasilisha hati hizo katika Benki ya Biashara ya Afrika, alisema ukitazama ushahidi ulitolewa washitakiwa kwa nia mbaya waliwasilisha hati hizo Benki ya Biashara ya Afrika huku wakijua hati hizo zimeghushiwa na mtumishi yoyote atakayezifanyiakazi nyaraka hizo awe ni mhanga wa nyaraka hizo na kumaliza kwa kuwaona washitakiwa ndiyo waliowasilisha nyaraka hizo katika ofisi hizo na wakajipatia fedha. “Kuhusu hoja ya tano kama nyaraka hizo feki ziliwasilishwa BoT na washitakiwa hao …majibu ya hoja hiyo siyo magumu kwani shahidi wa saba alisema ni washitakiwa ndiyo walipeleka nyaraka hizo BoT wakiomba walipwe fedha Septemba 8 mwaka 2005..na tayari mahakama hii imeishathibitisha kuwa washitakiwa hao ndiyo waliogushi nyaraka hizo kwa hiyo mahakama hii katika hoja hii inauhakika kuwa ni washitakiwa ndiyo waliwasilisha nyaraka hizo zilizoghushiwa benki kuu”alisema Hakimu Kahyoza. Kuhusu hoja ya sita kama washitakiwa hao waliiba shilingi milioni 660, hakimu Kahyoza alisema katika shitaka hilo mahakama inapenda kuwa mkweli kwani upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kosa la wizi kwani ulishindwa kuleta hata shahidi wa kuja kuthibitisha kosa hilo na hivyo inawaachilia huru washitakiwa hao katika kosa hilo la wizi kwani imeshindwa kuwatia hatiani. Hakimu Kahyoza akiichambua hoja ya saba ambayo ni kama washitakiwa walijipatia ingizo la shilingi bilioni mbili toka BoT, alisema hakuna ubishi kwamba BoT iliweka kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti ya washitakiwa baada ya washitakiwa hao kuwasilisha nyaraka za zilizoghushiwa BoT na kuomba walipwe na walilipwa na kuongeza kuwa amewatia hatiani katika kosa hilo. Akiitimisha hoja ya kwanza ya kama washitakiwa walikula njama, alisema upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kosa hilo kwani katika hata katika maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa pili Maranda, alikiri kuwa hapo awali alikuwa akikutana na Farijala na kujadili ni wapi ofisi ya kampuni yao iwepo na kwamba kwa maelezo hayo mahakama hiyo imelidhika washitakiwa walitenda kosa hilo la kula njama. Kwa upande wake Jaji Masengi akisoma hukumu yake iliyotofautiana na wana jopo wenzie, alisema yeye ameamua kutoa hukumu inayotofautiana na wenzie licha hukumu ya wenzie ndiyo itabaki kuwa hukumu ya mahakama alisema amepitia ushahidi wa mashahidi wa jamhuri ameona upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yao. Jaji Masengi alisema upande wa jamhuri ambao ndiyo uliodai hati ya kuamishia deni ya baina ya kampuni hizo zimegushiwa ,ulipaswa kuleta ushahidi kuthibitisha hilo pia ulipaswa kuleta ushahidi kuonyesha hiyo kampuni ya B.Grancey ilikuwa haijaipa mamlaka kampuni ya washitakiwa kudai deni lao hapa nchini na pia ulipaswa kuleta ushahidi kama fedha hizo zilizolipwa na BoT kwa kampuni ya washitakiwa hazikuifikia kampuni hiyo ya Ujerumani. “Kwa kushindwa huko kwa upande wa jamhuri kuleta ushahidi thabiti,hukumu yangu hii inawaachiria huru washitakiwa wote”alisema Jaji Fatma Masengi. Kwa upande wake wakili Mwandamizi wa Serikali Arafa Msafiri aliomba mahakama itakapotoa adhabu yake izingatia matakwa ya kifungu cha 348 na 359 cha Sheria ya Mwenendo wa Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 na itoe amri ya kuwataka washitakiwa warudishe kiasi cha fedha wanachotuhumiwa nacho na walipe fidia kwasababu hiyo siyo mara ya kwanza washitakiwa kutiwa hatiani kwa makosa kama hayo kwani washitakiwa hao Mei mwaka jana walihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kujiapatia ingizo la shilingi bilioni 1.8 za EPA katika kesi ya jinai Na.1161/2008. Kwa upande wake wakili wa washitakiwa Majura Magafu aliomba mahakama hiyo isitoe adhabu kali kwa washitakiwa kwani hadi sasa wapo gerezani wanatumikia kifungo cha miaka mitano jela na mazingira ya makosa ni kama waliyotiwa nayo hatiani jana na pia Farijala ni mgonjwa wa Figo na Maranda ana presha ya macho. Magafu akaiomba mahakama hiyo wakati ikitoa adhabu izingatie matakwa ya kifungu 38 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ambacho kinaipa mamlaka mahakama hata katika kesi kubwa au ndogo hali za watumiwa. Akitoa adhabu kwa washitakiwa hao Hakimu Mkazi Catherine Revocate alisema jopo hilo limejadiliana na kutazama mazingira ya kesi hiyo imefikia uamuzi wa kuwatia hatiani washitakiwa katika kosa 1,2,3,4,5 na 7 na kwamba kosa la sita ambalo ni la wizi wameachiria huru na kuongeza kuwa katika makosa hayo waliyowakuta na hatia kila kosa moja ni miaka mitatu na kwamba washitakiwa hao wataanza kutumia adhabu hiyo ya miaka mitatu jela kuanzia jana. Kutiwa hatiani katika kesi hiyo jana, Maranda sasa atabakiwa akikabiliwa na kesi nyingine tatu za EPA ambazo bado azijatolewa hukumu na mahakama hiyo wakati Farijala anabakiwa akikabiliwa na kesi mbili. Mei 23 mwaka jana mahakama hiyo iliwatia hatiani washitakiwa kwa makosa ya kujipatia shilinigi bilioni 1.8 kwa njia ya udanganyifu toka katika akaunti ya EPA. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 25 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.