ALIYEMJERUHI DK.ULIMBOKA KORTINI
Na Happiness Katabazi
MTU mmoja ambaye ni raia wa Kenya,Joshua Mulundi(21) jana alasiri alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkaiz Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na makosa ya kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk.Steven Ulimboka.
Wakili wa serikali Ladslaus Komanya mbele ya Hakimu Agnes Mchome, alidai kuwa Mulundi ambaye makazi yake Murang'a nchini Kenya anadaiwa kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa eneo la Leaders Club alimteka Dk. Ulimboka.
Komanya alidai shitaka la pili ni kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa katika eneo la Msitu wa Mwabepande Tegeta, Dar es Salaam kinyume na sheria mshitakiwa huyo alijaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka.
Hakimu Mchome alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kwani Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo Mulundi alidai kuwa kosa aliloshtakiwa nayo siyo sahihi.
Hata hivyo Hakimu Mchome alimwambia kuwa shauri hilo linasikilizwa Mahakama Kuu na siyo mahakamani hapo. Kesi imehairishwa hadi Agosti 5 mwaka huu itakapokuja kwaajili ya kutajwa na mshitakiwa amerejeshwa rumande.
Juni 27 mwaka huu, Dk.Ulimboka alionkitwa na msamalia mwema akiwa mtu katika msitu huo wa Mwabepande akiwa amejeruhiwa vibaya na kisha akafikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa na maumivu makali na kuanza kutibiwa lakini hata hivyo siku chache baadaye madaktari waliokuwa wakimtibu walisema wameshindwa kumtibia katika hospitali hiyo kwa sababu hakuna vifaa, hivyo wakamsafirisha kwenye nchini afrika Kusini ambako hadi sasa anaendelea na matibabu.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Julai 14 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment