Header Ads

FAHAMU FAIDA,CHANGAMOTO ZINAZOKABILI BALOZI ZETU UGENINI

Na Happiness Katabazi,aliyekuwa Brazil UBALOZI wa uwakilishi wa Umoja wa Mataifa New York, Marekani; Tanzania ni miongoni mwa ofisi za balozi kongwe za Afrika na imeweza kuiletea sifa na mafanikio makubwa nchi yetu ikiwemo kuitangaza Tanzania katika jumuiya ya kimataifa. Mwandishi wa makala hii ambaye alikuwa nchini Brazil kuhudhuria mkutano wa Rio+20 uliofanyika Juni 20-22 mwaka huu katika Jiji la Rio de Janeiro ambao zaidi ya wakuu wa nchi 140 wameudhuria mkutano ambao ulifunguliwa na Rais wa Brazil, Dilima Roussef na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na kwa upande wa Tanzania iliwakilishwa na Makamu wa Rais Dk. Mohamed Garib Bilal. Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya mazingira, Dk. Tereza Huvisa, aliye ongozana na Mshauri Mwandamizi wa Rais Jakaya Kikwete wa masuala ya diplomasia, Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais anayeshughulikia Mazingira Serikali ya Mapinduzi Zanzibar , Fatma Abdulhabib Fereji na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mahadhi Juma Maalim na maofisa wengine waandamizi wa serikali. Aliweza kufanya mahojiano ya ana kwa ana yaliyofanyika katika ofisi za Kituo cha Rio(Rio Centro) ambapo Tanzania ina ofisi zake hapo na Kaimu Balozi wa Uwakilishi wa Tanzania umoja wa Mataifa, New York, Dk. Justin Seruhere na Ofisa wa Mambo ya Nje, Mkuu wa ubalozi huo, Modesti Mero ambapo kwa upande wa Dk. Seruhere amelezea changamoto mbalimbali zinazoikabili ofisi hiyo ya ubalozi na faida ambayo nchi inapata kutokana na Tanzania kuwa na ofisi za ubalozi mjini Newyork na kuelezea muundo wa utendaji kazi wa ofisi hiyo. Kwa upande wa Mero yeye ameelezea jinsi ofisi ya Ubalozi wa Uwakilishi wa Umoja wa Mataifa New York, ilivyoshikiri kikamilifu na Ofisi ya Makamu wa Rais kuandaa ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa Rio +20. Yafuatayo ni mahojiano baina ya mwandishi wa makala hii na Kaimu Balozi Dk. Seruhere ambaye pia ni Mwanadiplomasia Mkuu. Swali:Tueleze shughuli zinazofanywa na ofisi ya Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, Marekani? Jibu: Ofisi hiyo inafanya shughuli za kuiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Mataifa. Uwakilishi huu tunaufanya kwa kutangaza jina la Tanzania katika UN. Shughuli zote zinapofanyika Tanzania na taasisi zake na sekta binafsi kwa Umoja wa Mataifa na kwa taasisi na makampuni ya kigeni yanayokuja kuwekeza nchini kwetu. Napenda ieleweke wazi kuwa shughuli za Umoja wa Mataifa zinafanyika katika kamati sita. Kamati ya kwanza inashugulikia na masuala ya upokonyaji wa silaha ili kusaidia Umoja wa Mataifa kusimamia amani , usalama duniani. Kamati ya pili ni ile inayoshughulikia masuala ya ushirikiano wa kimataifa na fedha na uchumi. Kamati ya tatu inashughulika na haki za binadamu na masuala mtambuka. Kamati ya nne ni kamati inayokomesha ukoloni duniani. Kwa hivi sasa tuna nchi 16 hazijajitawala na nchi moja wapo ambayo haijajitawala barani Afrika ni Sahara Magharibi. Kamati ya tano ni utawala na bajeti na kamati ya sita ni ile inayoshughulika na masuala ya sheria na mipaka ya bahari. Katika katika kila kamati hizo ina afisa anayeshughulikia kamati yake kila siku. Swali: Ofisi yenu ya ubalozi New York inakabiliwa na changamoto zipi? Jibu: Ofisi inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa rasilimali watu na ufinyu wa bajeti wa kuendeshea shughuli za ofisi hiyo. Ila tunachukua hatua za kukabiliana na changamoto hizo mbili kwa kununua jengo la ubalozi wetu New york kwani Oktoba mwaka jana serikali ilinunua jengo la ubalozi kwa thamani ya dola za Marekani milioni 24.5 lenye urefu wa ghorofa sita ambalo lipo Mtaa wa 53 Na. 307E, ambalo ghorofa mbili zitatumika kama ofisi za ubalozi huo na ghorofa zitakazokuwa zimesalia zitatumika kama kitega uchumi kwa ajili ya kupangisha wapangaji. Hata hivyo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa chini ya Waziri Bernard Membe inachukua hatua ya kukarabati hizo ghorofa mbili, ili ofisi za ubalozi wetu ziweze kuhamia katika ghorofa hizo mbili na ukarabati wa ghorofa hizo unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja baada ya mkandarasi kupewa kazi. Swali: Ni msaada gani ubalozi unaiomba Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa uwasaidie? Jibu: Ofisi yetu inaiomba wizara hiyo ituongezee rasilimali watu, ili waweze kuja kutuongezea nguvu katika kazi mbalimbali kwa sababu uwakilishi wa Tanzania unaushawishi mkubwa UN kuliko baadhi ya nchi nyingi na mashirika ya UN yanapenda kushirikisha ya Tanzania katika kupata maoni na miongozo kuhusu masuala mbalimbali ya kimataifa katika nyanja ya siasa, uchumi, amani na usalama. Swali: Tanzania inafaidika vipi kwa kuwa na ofisi ya Ubalozi wa Ushiriki pale New York? Jibu: Faida ya kwanza ni kuisaidia UN kutekeleza majukumu yake likiwemo jukumu la kusaidia Umoja wa Mataifa kutekeleza jukumu lake na kuwasimamia amani,usalama na maendeleo duniani kwa mujibu wa Katiba ya UN ya mwaka 1945. Faida ya pili ni kutoa ushawishi kwa nchi zilizoendelea na nchi za Kiafrika. Faida ya tatu, ni kuendeleza diplomasia ya kiuchumi kwa kushawishi wawekezaji na watalii kuja Tanzania kuwekeza na watalii wa nje kuja ndani kuleta mapato. Faida ya nne ni kusimamia uendelezaji wa sera ya Tanzania ya uhusiano wa kimataifa. Swali: Unauzungumziaje mchango wa ubalozi wetu mjini New York kimataifa? Jibu: Ubalozi wa New York umeweka ushawishi mkubwa duniani toka tumepata uhuru . Kwa hiyo kila ofisa wetu anayekuja kufanyakazi hapa anatakiwa adumishe heshima hiyo. Kwa sababu Tanzania imeongoza kushawishi jumuiya za kimataifa katika masuala ya maendeleo na masuala ya amani duniani na pia imeshiriki kikamilifu kuziletea uhuru baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Msumbiji, Zimbambwe na nyingine nyingi. Serikali inaendelea kuhakikisha kituo cha New York kinadumisha heshima hiyo. Kwa upande wake Ofisa Mambo ya Nje Mkuu Ubalozi Uwakilishi New York Tanzania, Modest Mero, ambaye anazungumzia kuhusu ni jinsi gani ofisi ya ubalozi ilivyoshirikiana kwa ukaribu na Ofisi ya Makamu wa Rais, katika ushiriki wa nchi katika mkutano wa Rio+20 uliomalizika Ijumaa iliyopita nchini Brazil. Mero ambaye pia ni mshiriki katika mkutano wa Rio +20 kwa upande wa Tanzania anaizungumzia Ajenda ya 21 iliyoazimiwa na mkutano wa kwanza wa Rio uliofanyika mwaka 1992 ambapo ilimalizika kwa kutoa maazimio kadhaa likiwamo azimio la ajenda ya 21. Ajenda ya 21 ni mpango wa utekelezaji wa mpango wa mataifa kuhusu utekelezaji wa UN wa maendeleo endelevu na ulikuwa ni matokeo ya mkutano wa kwanza wa kimataifa kuhusu Mazingira na Maendeleo uliofanyika Rio de Janeiro mwaka 1992. Katika mkutano huu nchi 178 ziliafiki na kuamua kwamba yatokanayo ndiyo yalikuwa dira katika shughuli za mazingira na maendeleo. Baadaye, Mkutano wa Maendeleo Endelevu (World Summit of Sustainable Development). Mkutano huo ulifanyika kwa mara ya pili mwaka 2002 jijini Johannesburg mwaka 2002. Mkutano huo wa Johannesburg uliitishwa kujadili maendeleo endelevu baada ya mkutano wa kwanza wa Rio uliofanyika 1992. Matokeo ya mkutano wa Johannesburg ni kuanzisha mpango wa utekelezaji wa maamuzi ya mkutano wa Rio ujulikanao kama (Johannesburg Plan of Implementation). Lakini mwaka 2010, Umoja wa Mataifa uliamua kuitisha mkutano mwingine wa Rio kuhusu maendeleo endelevu ili kutathmini hatima ya dunia kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kijamii na mazingira, ili kuweza kuweka mpango wa muda mrefu wa maendeleo endelevu. Nchi ya Brazil ndiyo ikaiomba jumuiya ya UN mkutano wa Rio+20 ufanyike nchini kwakwe katika jiji la Rio de Janeiro na uitwe Rio+20, ambapo tafsiri yake ni mkutano uliofanyika baada ya mkutano wa kwanza kufanyika mwaka 1992. Kwa hiyo mkutano wa Rio+20 uliomalizika Juni 22 mwaka huu ni jina lililotokana na mkutano wa kwanza wa Rio. Swali: Maandalizi ya mkutano wa Rio+20 yalianza lini na malengo ya mkutano huo ni nini? Jibu: Maandalizi yalianza tangu mwaka 2010 na yakakamilika Juni 16 mwaka huu. Maandalizi hayo kwa ujumla wa nchi zote yalishirikisha nchi wanachama wa UN, NGO’S, wafanyabiashara, serikali za mitaa. Lengo zima ni kuzungumzia maendeleo endelevu yanayozingatia uondoshwaji wa umaskini na utunzaji wa mazingira. Tanzania katika mkutano huu ikiwakilishwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Matokeo ya mkutano wa Rio+20 yamekuwa ni makubaliano ya mataifa ya kuona nama bora ya kutunza mazingira, uchumi na jamii kwa kuzingatia uondoshaji wa umaskini. Kumekuwa na majadiliano ya masuala mbalimbali yakiwemo malengo ya ukamilishaji wa malengo ya Milenia, kilimo, makazi, mazingira, uchimbaji wa madini unaozingatia mazingira,uchumi ili kuhakikisha dunia isipoteze rasilimali za kimazingira zisiharibiwe.. Nchi zinazoendelea zimejikita zaidi katika kuongelea nishati, vyakula ,utalii, usafirishaji, makazi, afya endelevu na ukuaji wa jamii na masuala ya jamii na masuala ya bahari na uchumi wa kibluu ambao unazingatia namna bora ya matumizi sahihi ya uvunaji wa rasilimali sahihi na endelevu baharini. Swali: Matokeo ya mkutano wa Rio +20 nini ? Jibu: Ni muendelezo wa makubaliano ya mkutano wa kwanza wa Rio ili kuzingatia mazingira ya sasa ya kiuchumi, mazingira na kijamii kama ilivyokubalika katika ajenda Na. 21 ya mkutano wa kwanza wa Rio uliofanyika mwaka 1992. Matokeo haya ya Rio +20 yataisaidia serikali ya Tanzania kuongeza nguvu ya utekelezaji katika taasisi zake na vyombo vyake. Vile vile matokeo ya mkutano huo wa kihistoria ambao ulihudhuliwa na wakuu wa nchi zaidi 135 yatasaidia wafanyabiashara kutumia mbinu bora ya uzalishaji wa bidhaa, kilimo, madini na shughuli zote za kibiashara kwa kuzungatia utunzaji wa mazingira. 0716 774494 www.katabazihappy.blogspot.com Chanzo:Gazeti la Tanzaia Daima la Alhamisi, Julai 5 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.