Header Ads

RAIS WA MADAKTARI AFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi RAIS wa Chama cha Madaktari nchini(MALT), Dk.Namala Mkopi jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,chini ya ulinzi mkali wa polisi akikabiliwa na makosa mawili likiwemo kosa la kudharau amri halali ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi. Wakili wa serikali Tumaini Kweka na Lasdiraus Komanya mbele ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba alidai kuwa mshitakiwa ambaye ni Daktari wa Hospitali ya Kijitonyama alidai anakabiliwa na makosa mawili. Wakili Kweka alidai kuwa shitaka la kwanza ni la kudharau amri ya mahakama kinyume na kifungu cha 124 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002. Alidai kuwa kati ya Juni 26 na 28 mwaka huu,Dk.Mkopi akiwa ni Rais wa chama cha Madaktari alidharau amri halali ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ya Juni 26 mwaka huu, ambayo ilimtaka mshitakiwa huyo kwenda kwenye vyombo vya habari kuwatangazia wanachama wa chama hicho wasitishe mgomo kwani mgomo ule waliokuwa wakitaka kuufanya ni batili kama ambayo mahakama hiyo ya Divisheni ya Kazi Juni 22 mwaka huu, ilitoa amri kama hiyo ya kuubatilisha mgomo huo, lakini mshitakiwa huyo hakufanya hivyo. Wakili Kweka alilitaja kosa la pili kuwa ni kuwashawishi madaktari wagome kinyume na kifungu 390 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kuwa Juni 27 mwaka huu, mshitakiwa huyo akiwa rais wa chama hicho aliwashawishi madaktari wasitekeleze amri hiyo ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ya Juni 22 mwaka huu,na matokeo yake madaktari hao wakagoma. Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na Hakimu Kahamba alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wanaotambulika na serikali ambao watasaini bondi ya Shilingi laki tano kila mmoja. Hata hivyo Wakili wa serikali Kweka aliomba mahakama impatie dhamana mshitakiwa chini ya kifungu cha 148 (c)(6) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambacho kinamtaka mshitakiwa ili apate dhamana ni lazima asalimishe hati ya kusafiria mahakama, asitoke nje ya mkoa bila ruhusa ya mahakama. Lakini Hakimu Kahamba alisema hicho kifungu hicho kilishabatilishwa na Mahakama Kuu na kwamba yeye atatoa masharti ya dhamana kwa kutumia kifungu cha 148(c) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai , kwani kifungu hicho kinaipa mamlaka ya kutoa masharti ya dhamana kwa mshitakiwa kadri inavyoona inafaa na baada ya kusema hayo aliarisha kesi hiyo kwa dakika kumi na mshitakiwa huyo akapelekwa kuifadhiwa katika mahabusu ya mahakamani hapo. Ilipofika saa 6:50 mchana mshitakiwa huyo aliletwa ndani ya chumba cha mahakama na hakimu Kahamba akasema maneno yafuatayo; “ Hatuko hapa kwaajili ya kukomoana,tupo hapa kwaajili ya kutenda haki hivyo nampatia mshitakiwa dhamana kwa kutumia kifungu cha 148(c) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, na ambaye anaona hajalidhika na uamuzi wake aende mahakama ya juu akakate rufaa”alisema Hakimu Kahamba. Mshitakiwa huyo alitimiza masharti hayo ya dhamana na Hakimu huyo aliairisha kesi hiyo Agosti 6 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa. Jana eneo la mahakama hiyo lilikuwa limefurika madaktari wenzake na ndugu na jamaa wa Dk.Mkopi waliofikisha kumwona mshitakiwa huyo ambaye aliletewa na askari polisi chini ya ulinzi mkali. Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita baadhi ya madaktari waligoma kufanyakazi kwa madai ya kuwa wanafanyakazi katika mazingira magumu na kwamba wanaomba masulufi yao yaongezwe. Wakati huo huo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa taarifa kwa madaktari walio kwenye mafunzo kwa vitendo(Interns) imesema imepokea malalamiko kuwa kati ya tarehe 23 juni, 2012 hadi tarehe 29 juni, 2012, Madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo 372 kati ya 763 katika hospitali mbalimbali nchini, waligoma kutoa huduma kwa wagonjwa ikiwa ni wajibu wao kama madaktari. Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo kwa vyombo vya habari ambayo imesainiwana Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Regina Kikuli Kitendo hicho sio tu kilihatarisha usalama wa wagonjwa waliohitaji huduma za matibabu katika hospitali hizo, bali kilikuwa ni ukiukwaji wa maadili ya taaluma. Kikuli alisema madaktari hao waliogoma walirejeshwa Wizarani kwa barua kutoka kwenye mamlaka za hospitali walikokuwa wakifanyia mafunzo kwa vitendo. Alisema kwa kuwa Wizara ndio yenye dhamana ya usimamizi wa huduma za afya nchini, na kwa kuwa madaktari hao wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika, hivyo Wizara imewasilisha malalamiko haya huko ili Baraza liwachunguze na kuamua hatma yao kitaaluma. “Hivi sasa madaktari hao hawako maeneo yao ya kazi, na suala hili limepelekwa Baraza la Madaktari kwa uchunguzi kuhusu kitendo walichokifanya, hivyo Wizara inasitisha posho zao kuanzia Tarehe 1 Julai, 2012 hadi hapo itakapopata taarifa ya uchunguzi wa Baraza la Madaktari…madaktari wengine waliogoma, taratibu za kiutumishi zitachukuliwa na mamlaka ya ajira zao kwa mujibu wa sheria na taratibu husika”alisema Kikuli. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 11 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.