Header Ads

JAMHURI YAFUNGA USHAHIDI KESI YA MAANDAMANO HARAMU


Na Happiness Katabazi

HATIMAYE upande wa Jamhuri katika kesi ya kula njama na kufanya maandamano haramu inayomkabili Salum Bakari Makame na wenzake 52  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana ulitangaza kufunga ushahidi wake katika kesi hiyo.

Hayo yalisemwa jana na Wakili Mwandamizi wa Serikali Bernad Kongora,Peter Ndjike,Nassor Katuga,Zuberi na Josephe Mahugo mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo ambapo alidai kuwa wamefikia uamzui huo baada ya kulizika mashahidi wote waliowaletea wanaweza kuijenga kesi yao.

“Jumla ya mashahidi 10 na vielelezo 12 tulivyovileta hapa mahakamani na vikapokelewa tunaona vinatosha kabisa upande wa jamhuri ufikie maamuzi ya kufunga  ushahidi wetu leo na tunaichia mahakama ifanye utaratibu mwingine wa kisheria’alidai Wakili Kongora.

Kwa upande wake Hakimu Fimbo alisema kuwa anaiarisha kesi hiyo hadi leo ambapo itakuja kwaajili ya upande wa jamhuri na utetezi unaowakilishwa na wakili wa kujitegemea Ibrahim Tibanyendera uje kuwasilisha kwa njia ya mdomo maombi yao ya kuwaona washitakiwa wana kesi ya kujibu au la.

Awali kabla ya Hakimu Fimbo kuanza kusikiliza kesi hiyo alianza kwa kumuachilia huru mshitakiwa wa 21 baada ya wakili wa serikali Kongora kuwasilisha hati iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi chini ya kifungu cha 91(1) ya Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 ,ambapo DPP ameona hataki kuendelea kumshitaki mshitakiwa huyo ambaye wakili Tibanyendera alieleza kuwa mtu huyo ana maradhi ya akili na Mkazi wa Mkuranga na siku hiyo ya maandamano Februali 15 mwaka huu, alikamatwa wakati akiwa na mjomba wake ambaye ni mshitakiwa wa 16 wakati wakitokea katika Hospitali ya Taifa ya Mhimbili kuchukua dawa za  mshitakiwa huyo aliyeachiliwa huru jana.

Aidha jana  Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam(ZDCO), Hemed Msangi ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo aliitwa tena kwa ajili ya kuhojiwa na wakili wa utetezi ambapo alieleza  kuwa kati ya Februali 11-17 mwaka huu, yeye alikuwa ndiye Kamanda wa Polisi Kanda Maalum  ya Dar es Salaam, na kwamba  Februali 11 alipokea barua toka Shura ya Maimamu iliyokuwa imesainiwa na  Sheikh Juma Idd  ikimuomba kibari cha kufanya maandamano ya kwenda ofisi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kumhoji ni kwanini hampatii dhamana  Ponda na kwamba maandamano hayo walikuwa wakitaka yafanyike Februali 15 baada ya swala ya Ijumaa na wandamanaji watakuwa wakitokea misikiti mbalimbali.

ACP- Msangi alidai  yeye na maofisa wenzake walitafakari hiyo barua  ambayo ilikuwa na saini ya Sheikh  Juma  Idd ambaye ni Amir wa Shura ya Maimamu  Temeke na walijiuliza uzito wa maandamano hayo na kwamba jeshi hilo walibaini kuwa hawakuwa na askari wa kutosha wakuwapeleka kila msikiti kwaajili ya kuyalinda waandamanaji hao na hivyo uhaba huo wa askari ungeweza kuleta usalama mdomo na pia walifikia uamuzi wa kuyakaza maandamano yake kwasababu waliona ofisi ya DPP ipo katikati ya jiji na ina sehemu finyu hivyo maandamano hayo yangeruhusiwa yangweza kuathiri haki za watu wengine wanaotumia jengo hilo la ofisi ya DPP ambalo linatumiwa na maofisi mengi na watembea kwa mguu.

“Pia jeshi la polisi lilitazama kuwa kesi ya Ponda ipo mahakamani hivyo ingewaruhusu waandamanaji hao kwenda mahakamani ni kama kuingia huru wa mahakama  na kwamba jeshi lilipata taarifa toka kwa DPP kuwa DDP alikuwa amepokea barua toka kwa Baraza la Wanazuoni iliyokuwa ikimuomba wakazungumze naye na kwamba tayari DPP alishalikubalia baraza hilo kuwa angekutana nao Februali 28 mwaka huu, ....kwasababu hiyo mimi niliwandikia barua ya kuzuia kufanyika kwa maandamano kwa sababu hizo zilizozitaja hapo juu kwani pia jeshi lilikuwa limepata taarifa za watu walikuwa wamepanga kufanya vurugu katika maandamano hayo”alidai ZDCO-Msangi.

Aliendelea kueleza kuwa licha ya kuwapelekea zuio hilo la maandamano kwa maandishi waombaji hao wa maandamano, pia yeye aliutangazia umma kupitia vyombo vya habari kuwa jeshi la polisi limezuia maandamano hayo lakini ilipofika Februali 15 washitakiwa hao walikaidi amri hiyo ya jeshi polisi waliandamana wakiwa na mabango, mawe,na silaha za jadi na yeye alitoa amri kwa askari wake wawatawanye na kuwakamata  na kuwafikisha polisi na kisha wafiksihwe mahakamani.

Itakumbukwa kuwa kesi hii ilifunguliwa rasmi Februali 18, na Februali 19 mwaka huu itakaanza kusikilizwa mfululizo hadi jana upande wa jamhuru ilipofunga ushahidi wao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Februali 27 mwaka 2013.




  



No comments:

Powered by Blogger.