KESI YA SHEIKH PONDA ULINZI BALAA
Na Happiness Katabazi
ULINZI unaowekwa wakati wa kesi ya inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu,Sheikh Ponda Issa Ponda, na wenzake 49,umevunja rekodi.
Mwandishi wa
habari hizi ambaye alifika saa moja asubuhi katika eneo hilo la mahakama
alishuhudia askari wa kikosi cha kutuliza ghasia,na wanausalama wengine wakiwa
wamevalia nguo za kiraia wakiwa wamebeba silaha nzito yakiwemo mabomu viunoni,
na mbwa wa 12 wa jeshi la polisi wakiwa
wamezingira ndani ya nje ya mahakama
hiyo kwaajili ya kuimarisha ulinzi kwasababu walikuwa wamepata taarifa kuwa
kuna baadhi ya wafuasi wa Ponda walikuwa wamepanga kuja kufanya vurugu
mahakamani hapo.
Ponda ambaye
aliingia katika eneo hilo akitokea gereza la Segerea huku akiwa amesindikizwa
na msafara wa magari ya maji ya kuwasha’ kikojozi’, na magari ya magereza,
aliingizwa moja kwa moja hadi mabusu ya mahakama hiyo huku wanausalama
waliokuwa wamesimama getini waliweka utaratibu wa kuwazuia wadhamini, ndugu na
jamaa wa washtakiwa katika kesi hiyo kuingia ndani ya viwanja vya mahakama
hiyo hali iliyosababisha ndugu na jamaa
hao kukaa nje ya jengo la Sophia House, tofauti na hapo awali ambapo
wanausalama walilikuwa wakiwaruhusu mamia hayo ya wafuasi wake kuingia ndani
mahakama hiyo hali iliyokuwa ikisababisha msongamano mkubwa na karaha katika
chumba cha uendesheaji kesi hiyo.
Hata hivyo
baadhi ya maofisa usalama waliliambia gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa
majina yao gazetini kuwa utaratibu huo waliouanzisha jana wa kuimarisha ulinzi na kuzuia wafuasi wa
Ponda na watu wengine ambao hawana shughuli yoyote wanaokuja kuifanya
mahakamani hapo wakati kesi hiyo ikiwa inasikilizwa wala kulikaribia jengo la mahakama hiyo ya
Kisutu utakuwa ni endelevu na hawatasita kumchukulia hatua mtu yoyote
atakayekaidi amri hiyo na kuongeza kuwa hadi jana polisi iliwakamata watu
watatu ambao walikuwa wakilamizisha kuingia ndani ya eneo hilo la mahakama bila
ya sababu inayompelekea huko.
Hata hivyo
jana ndani ya ukumbi namba moja wa mahakama hiyo ambapo kesi hiyo ya Ponda uwa
inasikilizwa hapo, ilikuwa ni tofauti kwani kulikuwa na washtakiwa,
wanausalama, waandishi wa habari,mawakili na hakimu tu , hali iliyosababisha
makundi hayo kufanya kazi yao kwa nafasi na hewa kupatikana na wananchi
mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari walivipongeza vyombo vya dola kwa utaratibu huo mpya kwani wingi wa watu
uliokuwa ukifurika wakati wa kesi hiyo pia ulikuwa ukiatarisha usalama na
kusisitiza kuwa utaratibu huo uwe endelevu.
Wakili
Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka akiomuongoza shahidi wake wa nane,
D/c-Sajenti Mkombozi Mhando mbele ya
Hakimu Mkazi Victoria Nongwa alidai kuwa Novemba 11 mwaka jana, alikuwa Kituo Kikuu cha
Polisi Kati akiwa na timu ya wapelelezi wenzake toka Temeke yeye alipewa jukumu
la kumhoji mshitakiwa wa tano, Mukadam abdallah Swaleh ambapo alimpa haki zake
zote.
Sajenti
Mhando alidai katika ungamo aliloungama mshtakiwa huyo Mukadamu, mshtakiwa huyo
alikiri kushiriki kikamilifu yeye na wenzake kuingia kwa jinai kwenye kiwanja
cha Chang’ombe Markas ambacho kiwanja hicho kilikuwa mali ya Bakwata na
kilishauzwa na kwamba alishiri kujenga msikiti wa muda katika eneo hilo na
walikuwa wakisali katika eneo hilo kuanzia Oktoba 12 -17 mwaka jana, siku
wenzake waliokuwa wakilala hapo kwa kipindi chote hicho kukamatwa na jeshi la
polisi.
Sajenti
Mhando alidai kuwa Mkadamu alimweleza kuwa yeye ni mjumbe wa Taasisi ilikuwa
ikiongozwa na Ponda na kwamba Aprili mwaka jana, walipata taarifa toka kwa
mwanafunzi wa kiislamu kuwa kiwanja hicho kimeuzwa na kwamba wao kama jumuiya
waliamua kwenda kuona na Mufti Mkuu wa Tanzania,Sheikh Shaban Bin Simba kumuuliza kuhusu hilo na Simba aliwajibu kuwa
ni kweli Bakwata imeishakiuza kiwanja hicho kwa njia halali kwa kampuni ya
Agritanza Ltd.
“Mkadamu
katika ungamo lake alieleza kuwa baada ya Mufti kuwaeleza hayo wao kama jumuiya
ya kiislamu waliamua kwenda kwa aliyenunua na kumwambia asiendelee na ujenzi wa
kiwanja hicho kwani kiwanja hicho ni mali ya waislamu siyo na ilipofika Oktoba
12 mwaka jana,baada ya Swala ya Ijumaa,ndiyo Mkadamu na wenzie walivamia eneo
hilo kwa lengo la kulitwaa eneo lao
ambapo waliweka kambi hapo hadi Februli 17 mwaka jana ambapo walijenga
na msikiti wa muda na wafuasi wengine walikuwa wakilala katika eneo hilo, ila
yeye Mkadamu hakuwa akilala hapo”alidai Mhando na kuomba maelezo hayo ya ungamo
liloungamwa na mshitakiwa huyo anaomba yapokelewe kama kielelezo.
Hata hivyo
wakili wa washtakiwa Mansoor Nassor alipinga maelezo hayo yasipokelewe
kwasababu kifungu cha 50(1)(a) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 ,
yataka mtuhumiwa achukuliwe maelezo ndani ya
saa nne tangu alipokamatwa na
hapa maelezo ya onyo ya Mkadamu yanonyesha Mhando alimchukua Novemba Mosi mwaka
jana wakati tayari mshtakiwa huyo
alishakuwa amekamatwa siku tano nyuma akiwa mahabusu na kwamba kifungu cha 50((1)b cha sheria hiyo
ya makosa ya Jinai kina mpa haki ofisa wa polisi kuongeza masaa ya
kumchukua maelezo mshtakiwa na kwamba shahidi aliyepo mahakamani (Mhando)hakuna
sehemu yoyote inaonyesha aliongeza muda wa kumchukua maelezo na kwamba kifungu
cha 51(a) cha sheria hiyo pia ina mpa
mamlaka ofisa wa polisi kwenda mahakamani kuomba mahahakama imuongezee muda wa
kumhoji mshtakiwa huyo lakini kwa makusudi shahidi huyo alishindwa kufanya
hilo.
“Mheshimiwa
hakimu pia kwa makusudi shahidi huyu amekiuka matakwa ya kifungu cha 57(2) (a)
cha Sheria hiyo ambacho kina mtaka ofisa
wa polisi kuandika maelezo ya mshitakiwa kwa mtindo wa swali na jibu lakini
maelezo ya Mkadamu yameandikwa kwa mtindo wa stori tu na siyo kwa mtindo wa
swali na jibu…na kwasababu hiyo sisi upande wa utetezi tunapinga maelezo haya
yasipokelewe kwasabababu yamekiuka
matakwa ya vifungu hivyo vya sheria”alidai wakili Mansoor.
Kwa upande
wake wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka, alidai kuwa kutokana na hali
hiyo,sheria ipo wazi na inataka mahakama iendeshe uchunguzi na upande wa
jamhuri upo tayari kuleta mashahidi wa tatu kuja kuthibitisha kuwa maelezo ya
onyo ya Mkadamu yalichukuliwa kwa kufuata taratibu zote za kisheria.Hata hivyo
wakili Mansoor alidai hakuna haja ya mahakama kufanya uchunguzi kwani udhahifu
wa maelezo hayo uliofanywa na shahidi huo wakati akimchukua maelezo upo wazi
hali iliyosababisha hakimu Nongwa kusema anakubaliana na ombi la wakili wa
jamhuri lilotaka ufanyike uchunguzi wa tuhuma hizo na kwamba anaiarisha kesi
hiyo hadi leo ambapo upande wa jamhuri utaleta jumla ya mashahidi watatu kuja
kudhibitisha kuwa kuwa maelezo ya mshtakiwa hayo yalikidhi matakwa ya kisheria
na kisha atatolea uamuzi ama yapokelewe
au yasipokelewe.
Baada ya
kesi hiyo kuairisha Ponda wakati akitoka ndani ya viwanja vya mahakama hiyo,
wafuasi wake wachache ukilinganisha na siku za nyuma walikuwa wamekaa na
wengine kusimama katika jengo la Sophia House walimpungia mkono na kusema
Takbiri Takbir. Na Ponda aliondoshwa katika viwanja hivyo na kupelekwa gereza
la Segerea saa 5:21 asubuhi.
Wakati huo huo; ilipofika saa 6:40 mchana ,jumla
ya washtakiwa 54 walioandamana
isivyohalali Ijumaa iliyopita Ilala
jijini Dar es Salaam,walifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Sundi
Fimbo wakikabiliwa na makosa ya manne.
Jopo la
mawakili waandamizi wa serikali linaloongozwa na Bernad Kongora, Peter Njiku,
Nassor Katuga, Zuberi Mkakatu na Joseph
Mahugo walidai mbele ya Hakimu Fimbo kuwa washtakiwa hao ni Salum Bakari Makame, Said
Idd Ally na wenzao 51 ambapo makosa ya
kula njama kutenda kosa,kufanya
mkusanyiko haramu,kufanya maandamano ambayo yalikatazwa na jeshi la polisi na
kosa nne ambalo linamkabili mshitakiwa wa kwanza,pili na watatu ni la kushawishi wananchi kutenda mnakosa
hayo Februali 15 mwaka huu, huko wilaya ya Ilala Dar es Salaam,na washitakiwa
walikana mashitaka yote na wakili Kongora akadai upelelezi wa kesi umekamilika
na wanaomba mahakama iwapatie tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Aidha wakili
Kongora alidai hata hivyo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ametoa kibali chake
cha kuzuia dhamana kwa mshtakiwa wa kwanza, pili na watatu chini ya kifungu cha
148(4) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, na kwamba kwakuwa
washitakiwa wanakabiliwa na makosa ya kuvuruga amani ,upande wa jamhuri
unaoiomba mahakama ifunge dhamana za washtakiwa wengine 51 wa kesi hiyo hadi
hali ya usalama itakapotengamaa. Hakimu Fimbo alisema inapowasilisha hati ya DPP
ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa mahakama yake inakuwa imefungwa mkono na hivyo
haiwezi kuipinga hati hiyo ya DPP na kwamba pia mahakama yake imekubali ombi la
wakili wa jamhuri ya kuwafunguia dhamana washtakiwa hao 51 licha mashitaka
yanayowakabili yanadhamana kwa mujibu wa
sheria hadi pale hali ya usalama itakapotengamaa na akaiarisha kesi hiyo hadi
leo itakapokuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuwasomea maelezo ya awali
washitakiwa hao na kuamuru washitakiwa waende gerezani.
Chanzo:Gazeti la
Tanzania Daima la Jumanne, Februali 19 mwaka 2013
No comments:
Post a Comment