Header Ads

WANAOTUMIA LUNINGA MUDA MREFU HUPOTEZA NGUVU ZA KIUME

Na Mwandishi Wetu

WANAUME wanaotumia muda wa saa tatu na zaidi kwa siku kutazama runinga wanapoteza nguvu za kiume ukilinganisha na wale wanaotazama runinga mara chache.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya ya Umma cha Havard (HSPH) kilichopo Boston nchini Marekani, umebaini kuwa kuporomoka kwa kiwango cha mbegu za kiume kunahusiana moja kwa moja na kutofanya mazoezi na kutazama runinga kwa muda mrefu.

Imeelezwa kuwa wanaume wanaotazama runinga kwa zaidi ya saa 20 kila wiki wanapoteza asilimia 44 ya mbegu za kiume ukilinganisha na wale wasiotumia muda mrefu katika runinga.

Vilevile, wanaume wanaofanya mazoezi kwa zaidi ya saa 15 kwa wiki, wana uwezo wa kuongeza asilimia 73 ya mbegu zao ukilinganisha na wale wasiofanya mazoezi au wanaofanya mazoezi chini ya saa tano kwa wiki.

Kiongozi wa utafiti huo, Dk Audrey Gaskin alisema mtindo wa maisha unachochea zaidi upungufu wa mbegu za kiume na uzalishwaji wa mbegu za kiume.

Mtafiti huyo alifanya uchunguzi wa viwango vya mbegu za kiume za wanaume 189 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 22 kuanzia mwaka 2009 hadi 2010.

Wanaume hao walihojiwa kuhusu kiwango cha ufanyaji wao wa mazoezi, muda wanaotumia katika kutazama runinga au filamu katika kipindi cha miezi mitatu.

“Baada ya utafiti huo, nusu ya wanaume wasiofanya mazoezi na waliotumia muda mrefu katika runinga walikuwa na kiwango hafifu cha uzalishaji wa mbegu,” alisema Dk Gaskin.
Dk Gaskin alisema: “Masuala mengine ya kiafya yanayoweza kuathiri kiwango cha mbegu za kiume ni chakula, msongo wa mawazo na uvutaji wa sigara,” alisema.

Daktari huyo alisema mwanamume anapokaa kwa muda mrefu katika sofa mbegu za kiume zinapata kiwango kikubwa cha joto ambalo huathiri uzalishwaji wa mbegu.
Alisema wanaume wanaohitaji watoto wanatakiwa kuacha kuvaa nguo za ndani zinazobana ili kuimarisha kiwango cha mbegu za kiume huku madereva na waendesha baiskeli wakionywa kuwa katika hatari ya kupungukiwa kutoa mbegu nyingi.

Mhadhiri Mkuu katika Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza, Dk Allan Pacey anasema matokeo ya utafiti wake yatasaidia kuelimisha umma.

Hata hivyo, Daktari bingwa wa Uchunguzi wa Magonjwa kwenye Kitengo cha Patholojia katika Hospitali ya Muhimbili, Henry Mwakyoma aliyewahi kufanya utafiti kuhusu ugumba kwa wanaume, alisema bado utafiti wa Dk Gaskin una maswali mengi.

“Siwezi kuukubali au kuukataa utafiti wake, inawezekana ni mionzi au joto ndilo linalosababisha udhaifu wa mbegu hizo, lakini bado utafiti wake una maswali mengi,” alisema Dk Mwakyoma.
 
Chanzo:Gazeti la Mwananchi, Ijumaa, Februali 8 mwaka 2013
No comments:

Powered by Blogger.