Header Ads

PONDA NA WENZAKE WAZIDI KUBANWA


Na Happiness Katabazi

MKUU wa upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Kipolisi Temeke(RCO), Ame Anange Anoqie jana ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,amesisitiza kuwa  Sheikh Issa Ponda na wenzake 49 siyo wamiliki halali wa kiwanja cha Chang’mbe Markas na kwamba waliingia kwa jinai katika kiwanja hicho.

Sambamba na hilo mamia ya watu waliokuwa wafuasi wa Ponda waliokuwa wakifika mahakamani kufuatilia kesi hiyo kuanzia Jumatatu hadi jana hawafiki ndani wala kulikaribia jengo la mahakama hiyo kwa kile kilichotaka na ulinzi mkali wa wanausalama mahakamani hapo ambapo wameweka utaratibu wa kutoruhusu mtu yoyote asiyehusika na jambo lolote mahakamani hapo kutoruhusiwa kurikaribia wala kuingia ndani ya jengo la mahakama utaratibu ambao umepongezwa .

Anoqie ambaye ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi(SSP) , na ni shahidi wa 12 wa upande wa jamhuri alitoea maelezo hayo wakati akiongozwa na wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka kutoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa alidai kuwa  Oktoba 12 mwaja alipokea taarifa toka kwa Kaimu Mpelelezi wa Wilaya ya Kipolisi Chang’ombe Inspekta Thobias Walelo ambaye alimwarifu kuwa kuna mwananchi amefika ofisi kwake Chang’ombe na kulalamika kuna kundi la watu wamevamia katika kiwanja chake cha Chang’ombe Markas.

SSP-Anoqie akaeleza kuwa baada ya Inspekta Walelo kumpatia taarifa hizo, amtaka Walelo aende kwenye eneo la tukio na azungumze na uongozi wa umati huo ambao umwenyeshe nyaraka zinazothibitisha kwamba wao ni wamiliki halali na pia akamwagiza huyo msaidi wake aende kufanya uchunguzi katika ofisi ya Ardhi katika Manispaa ya Temeke ili kubaini nani ni mmiliki halali.

“Ilipofika Oktoba 15 mwaka jana , Inspekta Walelo aliniletea taarifa ofisi ya Ardhi Temeke imempatia uthibitisho kuwa mmiliki wa kiwanja kile ni kampuni ya Agritanza na kwamba ule uongozi wa ule umati ambao ulitakiwa umletee vielelezo vya kuthibitisha kile kiwanja ni chao ulishindwa kufanya hivyo na mimi usiku wa kuamkia Oktoba 17 niagiza kikosi kazi cha askari polisi 50 kwenda kwenye kiwanja kile na kuwakamata washitakiwa ambao wapo mahakamani katika kesi hii”alidai SSP-Anoqie.

Akijibu maswali aliyokuwa akiulizwa na mawakili wa utetezi wanaongozwa na Nassor Juma na Njama kuwa ni kwanini amekurupuka kupeleleza na kuifungua kesi hiyo na kuifanya ni ya jinai badala madau, shahidi huyo alidai hajakurupuka kufungua kesi hiyo kwani yeye ni askari mpelelezi ambaye anafahamu vyema majukumu ya kazi yake na kwamba kosa la kuingia kwa jinai kwenye kiwanja cha mtu ambacho si mali yako, uchochezi, wizi wa malighafi  ni makosa yanayoangukia kwenye makosa ya jinai na siyo madai.

“Na hata kama ingekuwa ni kweli washitakiwa hawa kiwanja kile kweli kingekuwa ni chao yaani mali ya waislamu , hawakuruhusiwa kutumia njia zile za uvamizi kudai haki yao ya kukipata kile kiwanja kwani sheria za nchi zipo wazi na zinatutaka tuzifuate ,kama waliona Agritazana kawapora kiwanja chao wangeenda kutoa taarifa katika vyombo vya dola, sasa wao hilo walishindwa kulifanya matokeo yake wakaenda kuingia kwa jinai katika kiwanja hicho kwa lengo la kukitwa kinyume na sheria”alidai  Anoqie.

Aidha hakimu Nongwa aliarisha kesi hii ambayo imeanza kusikilizwa mfululizo tangu Jumatatu wiki hii hadi leo saa mbili asubuhi kwaajili ya shahidi wa 13 kuanza kutoa ushahidi wake na akaamuru Ponda na mshitakiwa wa tano, Mkadamu Abdallah kurejeshwa rumande kwasababu bado Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Dk.Eliezer Feleshi bado ajaondoa hati ya kuzuia dhamana zao kwamba   washitakiwa wengine wataendelea kuwa nje kwa dhamana.
Hali ya ulinzi na usalama wa kiwango cha juu umeendelea kuimarishwa ndani na nje ya mahakama hiyo na wanausalama waliovalia sare na wale ambao wamevalia kiraia huku askari wa kikosi cha Mbwa wakiwa nao wanalinda eneo hilo kwa kutumia mbwa hao, na vifaa maalum vya kuwapekua wananchi wanaoingia ndani ya eneo hilo na ndani ya kuendeshea kesi hiyo wanaingia wanahabari ,wanausalama, hakimu, mawakili tofauti na awali ambapo wafuasi wa Ponda walikuwa wakiruhusiwa kuingia. 

Chanzo:Gazeti  la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 22 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.