HATIMA YA PONDA MACHI 4
Na Happiness
Katabazi
UPANDE wa
Jamhuri katika kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi ya Sh.milioni 59
inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda na
wenzake 49 wameiomba Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone Ponda na wenzake wanakesi ya kujibu
kwasababu umeweza kujenga kesi yao.
Kesi hiyo
ambayo jana ilikuja kwaajili ya upande wa jamhuri unaowakilishwa na wakili
Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka na Inspekta wa Polisi, Hamisi Said na upande wa utetezi
unaowakilishwa na Juma Nassor na Njama kuwasilisha majumuisho yao kwa njia yam
domo ya kuomba mahakama iwaone washitakiwa wanakesi ya kujibu au la.
Kwa upande wake wakili Kweka aliikumbusha
mahakama kuwa washitakiwa wanakabiliwa na makosa matano ambayo ni kula njama
kutenda kosa, kuingia kwa nguvu kwenye kiwanja cha Chang’ombe Markas ambacho ni
mali ya Kampuni ya Agritanza Ltd, kujimilikisha kiwanja hicho, wizi na
uchochezi.
Wakili Kweka
alidai kuwa washitakiwa wote ni kweli walitenda makosa hayo na ndiyo maana
walikuingia kwa jinai tangu Oktoba 12 hadi walipokuja kukamatwa usiku wa
kuamkia katikaOktoba 17 mwaka jana katika kiwanja hicho na uwepo wao katika
kiwanja hicho katika siku hizo zote ni ndiyo walitenda kosa la kujimilikisha
kiwanja hicho isivyo halali.
Akilichambua
kosa la wizi alidai kuwa wakati washitakiwa wameingia kwa jinai katika kiwanja
hicho walikuta kokoto, mchanga mali ya Agritanza na kwa makusudi wakaamua
kutumia malighafi hizo kwaajili ya kujenga msikiti mdomo ndani ya kiwanja hicho
bila idhini ya mmiliki wa kiwanja hicho ambacho ni kampuni hiyo.
Kuhusu kosa
la uchochezi wakili Kweka alidai kielelezo cha 13 kilichotolewa na Shahidi 17 ,F
8586/DC Ismail ambaye alimhoji mshitakiwa aitwaye Fiswaali ambaye ni mkazi wa
Mlandizi ambaye katika maelezo yake ambayo yalipokelewa na mahakama kama
kielelezo cha 13, alimweleza shahidi huyo kuwa yeye alisikia wito toka Redio
Iman ambayo ilikuwa ikiwataka waislamu wote waende wakaongeze nguvu ya kujenga
msikiti katika kiwanja cha Chang’ombe
Markas kwasababu kiwanja hicho mali ya waisilamu na kilikuwa kimeibwa.
“Kwa maelezo
hayo ya mshitakiwa Fiswaali ambayo maelezo hayo yalipokelewa na mahakama kama
ushahidi tosha kwa mshitakiwa wa kwanza(Ponda) na mshitakiwa wa tano (Mkadamu)
walitenda kosa hilo la kuchochea washitakiwa waende kutenda makosa yanayowakabili
katika kiwanja hicho.
Aidha Kweka
ambaye alitumia dakika kumi tu kuwasilisha majumuisho alidai upande wa jamhuri
umeweza kujenga kesi yake kupitia mashahidi wake 16 na vielelezo 13
walivyovileta mahakamani ambapo waamini kisheria vitawafanya washitakiwa
wapande kizimbani kujitetea.
Kwa upande
wake wakili wa utetezi Nassor Juma akiwasilisha majumuisho yake, aliomba
mahakama iwaone washitakiwa hawa kesi ya kujibu na waachiliwe huru kwasababu
kesi hiyo imefunguliwa na polisi kwa jazba na upande wa jamhuri umeshindwa
kujenga kesi yao na kwamba mahakama kuwaambia washitakiwa wanakesi ya kujibu ni
kuwasumbua bure washitakiwa.
Wakili
Nassor alidai wanachokiona katika kesi hiyo ni kuwa kuna mgogoro wa ardhi ambao
ulitakiwa ukatatuliwa kwanza na Mahakama ya Ardhi kwa mujibu wa kifungu cha 167
cha Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999.
Nassor
alidai kuwa katika hati ya mashitaka ,kosa la kwanza ni la kula njama kutenda
kosa na kwamba jamhuri imeshindwa kuanisha ni kosa gani hilo la jinai au madai
lililotendwa na washitakiwa na kwamba hata hilo kosa la tano la kushawishi au
uchochezi upande wa jamhuri umeshindwa kuanisha wazi washitakiwa walishawishiwa
kutenda kosa lipi ambalo limesababishwa kufunjwa kwa sheria.
Akichambua
kosa kosa la pili, tatu na nne la
kuingia kwa jinai, kujimilikisha kiwanja hicho isivyo halali na wizi, wakili
huyo alidai washitakiwa hawakuingia kwa jinai kwani hata shahidi wa jamhuri ambaye
ni mlinzi alieleza kuwa Ponda alifika
katika eneo hilo akawasalimia
Asalamaleku na Asalamaleku manaake amani
iwe na kisha mlinzi huyo akampatia simu
Ponda akaongea na shahidi wa tatu ambaye ni mmiliki wa kiwanja hicho Sulemain
Hilary na kuhoji kuwa kama Ponda aliwasalimia vizuri , je huko ndiko kuingia
kwa jinai?
Kuhusu kosa
la wizi alidai washitakiwa hao hawajatenda kosa na upande wa jamhuri umeshindwa
kulithibitisha kwani Hilal alitoa ushahidi unaosema ndani ya kiwanja chake
kulikuwa na kokoto, mchanga ambazo hata hazijaletwa kama kielelezo na kwamba
washitakiwa walichokifanya ni kutumia malighafi hizo kujengea msikiti mdomo na
kwamba huo sio wizi.
“Sisi upande
wa utetezi tunaiomba mahakama hii iwaachirie huru washitakiwa wote na iwaone
hawana kesi ya kujibu kwasababu kesi hii imefunguliwa kwa jazba na polisi na
upande wa jamhuri umehindwa kuleta ushahidi ambao utaweza kuishawishi mahakama
iwaone washitakiwa wote wana kesi ya kujibu”alidai wakili Nassor.
Kwa upande
wake Hakimu Nongwa aliarisha kesi hiyo hadi Machi 4 mwaka huu, ambapo atakuja
kutoa uamuzi wa ama kuwaona washitakiwa wana kesi ya kujibu au la na kuamuru
Ponda na Mkadamu warudishwe rumande kwasababu bado Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP), Dk.Eliezer Feleshi hajaondoa hati yake ya kuwafungia dhamana.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi Mosi mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment