Header Ads

SHAHIDI ADAI PONDA ALIAMASISHA WAISLAMU WAFANYE UVAMIZI




Na Happiness Katabazi


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu  Dar es Salaam imeelezwa kuwa Katibu  wa Jumuiya na Taasisi za kiislamu Shekhe Ponda Issa Ponda  ndiye aliwapatia taarifa masheikh  wa misikiti  pamoja na kuwaamasisha  waumini wa dini ya kiislamu waende wakaiokombee mali ya waislamu ambacho ni kiwanja Chan’ombe Markas ambacho walidai kimeporwa wakati kiwanja hicho si mali ya waislamu ni mali ya kampuni ya Agritanza Ltd.

Madai hayo yaliyolewa jana na shahidi wa 14 wa upande wa Jamhuri D/C Koplo Zakayo  katika kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.milioni 59 inayomkabili Ponda na wenzake 48  wakati akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa ambapo alidai kuwa  alidai kuwa mshitakiwa Ayubu Juma alimueleza hayo wakati akimuhoji katika kituo cha polisi Kijitonyama.

Koplo Zakayo alidai, Juma alimueleza kuwa Oktoba 12 mwaka jana ,saa mbili usiku  baada ya swala ya Insha kumalizika  katika msikiti Mwanamtoti, Shekhe Amri  Said ambaye ni kiongozi wa msikiti huo, aliwatangazia waumini waliokuwa wameudhulia ibada hiyo  kuwa amepata taarifa kutoka kwa  mshitakiwa wa kwanza  Ponda kuwa eneo la Markas ambao wao walidai ni mali ya waislamu wakati Bakatwa inadai eneo hilo si mali ya waislamu kuwa limevamiwa.

Zakayo alidai kuwa Juma alimweleza kuwa Sheikh Said akaendelea kuwatangazia kuwa Ponda amewataka  waislamu waungane kwenda kulikomboa eneo hilo  lakini yeye alishindwa kwenda hadi usiku wa Oktoba 16 mwaka jana  alipowasisitizia, wakaenda watu 14 walipofika katika eneo la Chang’ombe   wakaambiwa wajenge msikiti wa muda.

Aliendelea kueleza kuwa , Juma katika maelezo yake alimueleza kuwa Baraza la Waislamu (BAKWATA) waliuza eneo hilo kwa manufaa yao binafsi  na pia hawakuwa wamefuata taratibu  za kisheria kwasababu  kiwanja kile ni mali ya waislamu.
Kwa upande wake shahidi wa 13, Koplo Masiku ambaye ni ASkari kituo cha polisi Chang’ombe alidai kuwa, wakati akimuhoji mshitakiwa Khalid Issa alimueleza kuwa, walikwenda katika eneo la Chang’ombe Markazi kwaajili yakufanya harambee ya kujenga msikiti.

Koplo Masiku alidai kuwa wakati akimhoji mshitakiwa Abdalah Senza , mshitakiwa huyo alimweleza  kuwa aliteuliwa na viongozi wa msikiti wa Vingunguti kwa ajili ya kwenda kulinda eneo hilo linalomilikiwa na waislamu ili lisiuzwe.

Katika maelezo yake alidai, eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na Wamisri na walijenga shule ili waislamu wasome bure pamoja na hospitali ambayo bado haijaanza kutoa huduma. Aidha mashahidi hao wawili walitoa maelezo waliyokuwa wamewachukua washitakiwa hao wakati wakiwahoji  na waliomba mahakama ipokee kama vielelezo na mawakili wa upande wa utetezi hawakupinga .

Hakimu  Nongwa alipokea nakala ya maelezo hayo kama vielelezo na kisha akaiarisha kesi hiyo hadi Jumatatu ijayo ambayo shahidi wa 15 ataanza kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo ambayo ambayo imeanza kusikilizwa mfululizo tangu Jumatatu wiki hii chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama na akaamuru Ponda na mshitakiwa wa tano Mkadamu Abdallah warudishwe rumande kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka,Dk.Eliezer Feleshi bado hajaondoa hati yake iliyowangia dhamana na akaamuru washitakiwa dhamana zao zinaendelea.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Februali 23 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.