Header Ads

AZIRAI KIZIMBANI BAADA DPP KUMFUNGIA DHAMANA







Mahakama ya Hakimu Mkazi KisutuMFANYABIASHARA Hussein Amin Suleiman (39), mwenye asili ya Kiasia, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na makosa mawili ya kudharau amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi.
Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, mshtakiwa huyo alianguka na kupoteza fahamu kizimbani baada ya kumsikia Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, akiieleza mahakama hiyo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, amewasilisha hati ya kufunga dhamana kwa mshtakiwa.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Issaya Arufani, wakili Kweka alidai kuwa kesi hiyo ni mpya na kwamba mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili.
Wakili Kweka alidai kuwa kosa la kwanza linahusu kudharau amri ya mahakama kinyume na kifungu cha 124 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 kuwa Novemba 18 mwaka 2013 huko eneo la Sea View Upanga, Dar es Salaam,  alifanya marekebisho katika kiwanja  Kitalu Na. 1032 /60 LO No. 51464 huko eneo la Ocean Road  na akafanya marekebisho kitendo ambacho ni kinyume na amri iliyotolewa na Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi  katika kesi Na. 41 ya mwaka 2012 ya Novemba 18, 2013.
Amri hiyo ilikuwa  ikiikataza Kampuni ya Twiga  Paper  Production  Limited  au wakala wake kuvunja au kufanya mabadiliko yoyote  katika nyumba iliyopo kitalu Na. 1032/60LO No. 51464 Ocean Road.
Wakili Kweka alilitaja kosa la pili kuwa ni la kudharau pia amri ya mahakama hiyo  kuwa Novemba 18 mwaka 2013 huko eneo la See view Upanga   alivunja  nyumba aliyokuwa akiishi ofisa mwenye cheo cha juu wa serikali mwenye cheo cha  Kamishna wa Fursa Sawa ya Kibiashara na nyumba hiyo ni mali ya serikali ilioyopo kwenye kitalu Na. 1032/60LO.No.51464 iliyopo eneo la Ocean Road  kinyume na amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi katika kesi  namba 240 ya mwaka 2004 iliyotolewa mwaka 2007  kwa Kampuni ya Twiga  Paper Products  Limited  au wakala wa kampuni hiyo  ambapo mahakama hiyo ilitoa amri ya kuzitaka pande zote katika kesi hiyo kuacha nyumba hiyo Na. 3 iliyopo kitalu Na. 1032/60  ibaki kama ilivyo hadi pale kesi ya msingi itakapomalizika, lakini mshtakiwa huyo alikaidi amri hiyo ya mahakama na kuivunja.
Kweka alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na wanaomba tarehe ya kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa na kwamba licha kesi inayomkabili mshtakiwa huyo ina dhamana, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka, Dk. Feleshi amewasilisha hati ya kumfungia dhamana mshtakiwa huyo chini ya kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.
Kwa upande wake wakili wa mshtakiwa, Pascal Kamala, aliipinga hati hiyo ya DPP kwa sababu inakwenda kinyume na Ibara ya 13(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inasema kila mtu ana haki ya kupata dhamana.
Hata hivyo, mwandishi wa habari hizi alikuwa akimtazama mshtakiwa aliyekuwa amesimama wakati akisomewa mashtaka yake na ilipofika wakili Kweka kuieleza mahakama kuwa DPP amefunga dhamana, mshtakiwa huyo aliyekuwa amesimama alikuwa akianza kufumba macho na kuhema kwa taabu na baada ya muda kidogo mshitakiwa huyo alianguka chini na kuanza kupepewa na ndugu zake.
Hali iliyosababisha hakimu atoke kwenye kiti chake cha enzi na kwenda kumshuhudia mshtakiwa alivyoanguka kizimbani huku mahakama yote ikibaki na taaruki.
Kuona hivyo hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 28 mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kuamuru mshitakiwa apelekwe hospitali.
Hata hivyo, ndugu mmoja wa mshtakiwa huyo ambaye jina lake halikuweza kufahamika alikuwa akimzonga mwandishi wa habari hizi asimpige picha mshtakiwa na kumtaka asiandike habari hiyoiShare

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Januari 25 Mwaka 2014


No comments:

Powered by Blogger.