Header Ads

LIYUMBA AIBWAGA SERIKALI KORTINI





Na Happiness Katabazi 

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba.

Liyumba alikuwa akikabiliwa na kesi ya kukutwa na simu ya mkononi wakati akiwa gerezani, akitumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukutwa na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya fedha za umma katika ujenzi wa maghorofa mawili ya jengo la BoT.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Augusta Mbando, baada ya kuridhika na upande wa utetezi.

Hakimu huyo alisema baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na utetezi, ameridhika kuwa Liyumba hana hatia, hivyo anamwachia huru.

Hakimu huyo alisema amebaini kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Serikali ni dhahifu, hivyo umeshindwa kuishawishi mahakama yake imuone mshitakiwa ana hatia.

Hakimu Mbando akichambua ushahidi uliotolewa na upande wa Serikali, alisema ni dhahifu kwani unaonyesha Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda, alileta simu yenye namba 0653004662 ambayo walidai alikamatwa nayo mshitakiwa gerezani Januari 27 mwaka 2011 wakati akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela.

Alisisitiza kuwa ushahidi wa Serikali ni dhahifu kwa sababu umeshindwa kuionyesha mahakama simu  anayodaiwa kukutwa nayo Liyumba gerezani, namba zake zilisajiliwa na kumilikiwa na Liyumba.

“Mahakama hii inalazimika kumuona Wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda, kuwa ni mzembe  kwa sababu alikuwa na kila sababu ya kuiomba mahakama ipokee simu ile aina ya Nokia kama kielelezo na si kuiomba mahakama ipokee kama utambulisho, kwa sababu shahidi wa upande wa Serikali, Patrick, alifika mahakamani kutoa ushahidi na Wakili Kaganda alipaswa kumwongoza Patrick aitoe simu hiyo kama kielelezo na si utambulisho,  lakini wakili huyo alishindwa kufanya hivyo,” alisema Hakimu Mbando.
Hakimu huyo alisema kwa udhahifu huo, ulioonyeshwa na Serikali katika kesi hiyo ni faida kwa Liyumba ambaye alikuwa akitetewa na mawakili wa kujitegemea, Hudson Ndusyepo na Majura Magafu.
Kutokana na ushahidi huo, hakimu huyo alitangaza kumwachia huru Liyumba baada ya kumuona hana hatia katika kesi hiyo iliyokuwa ikivuta hisia za wengi tangu ilipofunguliwa.

Mwaka 2011 ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Liyumba akiwa gerezani Ukonga, Dar es Salaam, wakati akitumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka, alikutwa akiwa na simu hiyo gerezani kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kuwa Julai 27, mwaka 2011 katika Gereza la Ukonga, Liyumba alikutwa na simu kinyume cha kifungu namba 86, kifungu kidogo cha kwanza na cha pili cha Sheria ya Magereza iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Januari 17 mwaka 2014

No comments:

Powered by Blogger.