Header Ads

KIBANDA AIBWAGA SERIKALI






Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemwachiria huru Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini Absalom Kibanda na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi kuandika na kuchapisha makala ya uchochezi na kusema kuwa mtu yeyote aliyeisoma makala ile na mwenye akili timamu hawezi kusema makala ile ni ya uchochezi wala kuwafungulia kesi ya uchochezi.

Hukumu hiyo ya iliyokuwa ikisubiriwa kwa shahuku na wadau wa habari hapa nchini na kusababisha jana asubuhi wanahabari kufurika katika viwanja vya mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alisema mbali na Kibanda washitakiwa wengine walikuwa ni aliyekuwa Mwandishi wa makala hiyo ilichopishwa katika gazeti la Tanzania Daima la Novemba 30 mwaka 2011, iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Wakala Maalum kwa askari wote’,Samson Mwigamba na  Meneja Uendeshaji  Biashara  wa kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophile Makunga waliokuwa wakitetewa na mawakili Isaya Matambo, Nyaronyo Kicheree, John Mhozya na Mabere Marando.

Hakimu Lema alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa hati ya mashitaka ilikuwa na jumla ya makosa mawili , kosa la kwanza likikuwa ni la kuandika makala ya uchochezi kinyume na kifungu cha  32(1) (c) na  31 (1) (a) cha Sheria ya Magazeti  sura ya 229  ya mwaka 2002 , ambalo lilikuwa likimkabili mshitakiwa wa kwanza na wa pili (Mwigamba na Kibanda) .

Na kwamba kwa makusudi washitakiwa hao Novemba 30 mwaka 2011 waliandika makala hiyo iliyodaiwa na upande wa jamhuri kuwa ni ya uchochezi  ambayo ilikuwa na nia ovu ya kuamasisha askari wasitii amri zinazotolewa na viongozi wao.Kosa la pili ni la kuchapisha makala hiyo iliyodaiwa kuwa ni ya uchochezi ambalo lilikuwa likimkabili Makunga peke yake, kwamba Kampuni ya Mwananchi ndiyo ilichapisha makala hiyo  na kwamba upande wa jamhuri ulileleta jumla ya mashahidi wa tatu na upande wa utetezi ulileta mashahidi wa nne.

Alisema katika haki jinai , ni jukumu la jamhuri kuthibitisha kesi yao bila kuacha mashaka yoyote na kwamba katika kesi ushahidi wote uliotolewa na jamhuri katika kesi hiyo ni wazi umeishawishi mahakama yake ione kuwa upande wa jamhuri uliokuwa ukiongozwa na mawakili wa serikali Prosper Mwangamila na Elizabeth Kaganda umeleta ushahidi dhahifu na hafifu ambao umeshindwa kuishawishi mahakama hii iwaone washitakiwa wote wana hatia katika kesi walishitakikwa nayo.

“Itakumbukwa kuwa Desemba mwaka jana washitakiwa walipomaliza kujitetea, mahakama hii ilitoa amri kwa pande zote katika kesi hii kuleta majumuisho ya mwisho kwa maandishi  lakini hadi hivi leo mahakama hii inatoa hukumu ya kesi hii ni upande wa utetezi tu ndiyo ulitekeleza amri hiyo na kuleta majumuisho yao ya mwisho na kwa masikitiko makubwa na kustaajabisha upande wa jamhuri hakutekeleza amri hiyo yaani haujaleta majumuisho yao na wala umeshindwa kuleta sababu ya kufanya hivyo lakini hilo hauzui mahakama kutoa hukumu yake”alisema Lema na kusababisha watu kushikwa  na butwaa.

Alisema ili makosa ya uchochezi ya thibitike ni lazima upande wa jamhuri ulipaswa uleta madhara yaliyotokea baada ya ile makala kuchapishwa na madhara yenyewe ni kama kulikuwa na kundi la watu lilipanga kufanya vurugu, au kuna askari kweli walikataa kutii amri za makanda wao lakini upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi wa madhara yaliyojitokeza ndani ya majeshi baada ya makala kuchapishwa na kwa mujibu wa mashahidi wa upande wa jamhuri ambao ni mlalamikaji wa kesi na mpelelezi wa kesi hiyo ofisa wa Polisi David Hizza, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, George Mwambashi walieleza mahakama hapakutokea madhara ndani ya majeshi yao yaliyosabishwa na makala hiyo kwani kuna askari wengi walikuwa hawajaisoma hiyo makala.

“Ukilisoma shitaka la kwanza ni la kuandika makala ya uchochezi linalomkabili Mwigamba na Kibanda.Na Mwigamba alivyojitetea na kueleza kuwa aliandika makala hiyo akiwa Arusha na kuituma katika chumba cha habari kinachochapisha gazeti la Tanzania Daima na upande wa jamhuri umeshindwa kuonyesha kuleta ushahidi unaonyesha makala hiyo kweli iliandikwa na Mwigamba, na alivyoiandika alikuwa na nia ovu, ya kutaka ufanyike uasi ndani ya majeshi na pia umeshindwa kuonyesha Kibanda alishiriki vipi kuiandaa makala hiyo kwa Kibanda katika utetezi wake alieleza kuwa wakati makala hiyo inachapishwa na kuhaririwa alikuwa nje ya Dar e Salaam na hakuna ushahidi wa jamhuri uliotolewa kupinga utetezi wa Kibanda”alisema hakimu Lema.

Alisema shahidi wa Jamhuri Hizza, katika ushahidi wake alidai yeye alipoisoma ile makala aliona ni ya uchochezi na akaenda kutoa taarifa kwa makamanda wake ambao nao waliisoma na kuiona ni ya uchochezi wakamtaka Hizza awe mpelelezi wa kesi na Hizza alimuita Kibanda katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kumhoji kisha baadae akawa shahidi katika kesi hiyo  lakini cha kustaajabisha shahidi huyo ameshindwa kuleta mahakamani maelezo aliyomuhoji Kibanda polisi na badala yake shahidi huyo akaeleza mahakama kuwa eti jeshi la polisi wameamua kukaa na maelezo hayo kwa manufaa yao na kwamba kisheria pale mtu zaidi ya mmoja anaposhitakiwa kwa kosa moja ni lazima upande wa jamhuri ulete ushahidi unaonyesha kila mshitakiwa alishiriki vipi kutenda kosa hilo lakini katika kesi hii upande wa jamhuri umeshindwa kufanya hivyo.

 Akilichambua kosa la pili la kuchapisha makala ya uchochezi lilokuwa likimkabili Makunga peke yake, pia hakimu Lema alisema upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi wa moja kwa moja unaonyesha Makunga ndiye aliyechapisha makala na kuongeza kuwa kwa bahati mbaya shahidi wa Jamhuri ambaye ni Msajili wa Magazeti Rafael Hokororo katika ushahidi wake alioutoa alishindwa kusema kuwa makala hiyo ni ya uchochezi na kwamba Hokororo hakuwai kumuita Kibanda ambaye alikuwa ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima lilochapisha makala hiyo kumuona kuwa makala ile ilikuwa ni ya uchochezi.

“Mimi kama hakimu ni maoni yangu kuwa washitakiwa walishitakiwa kwa hisia tu  na hisia zinakatazwa kumfungulia mtu kesi mahakamani ..kwani hata huyu mpelelezi wa kesi hii Hizza alipaswa alete ushahidi unaonyesha nani aliandika makala ,nani alihariri makala hiyo na ninani aliichapisha makala hiyo……mtu mwenye akili timamu ambaye aliisoma makala hiyo hawezi kusema makala hiyo ni ya uchochezi wala kuwafungulia washitakiwa hao kesi ya uchochezi mahakamani, ’alisema hakimu Lema.

Aidha alisema mwandishi wa makala hiyo Mwigamba aliandika makala hiyo kwania njema tu na alikuwa akiitumia haki yake ya kutoa maoni iliyainishwa kwenye Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977  na kwamba  makala alikuwa na nia njema ya kuyakumbusha askari wa majeshi ya Tanzania kutenda kazi zao kwa kufuata haki na kuheshimu haki za watu wengine za kushiriki maandamo ambazo na kwamba aliandika makala hiyo kwasababu alikuwa akikemea mauji yaliyofanywa na jeshi la polisi Januari 5 mwaka 2011 jijini Arusha ambapo polisi iliwaua watu watatu waliokuwa wakishiriki maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), hivyo nawaachiria huru washitakiwa wote chini ya kifungu cha 235 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

 Akizungumza nje ya viwanja vya mahakama, Kibanda ambaye kwa sasa ni Mhariri Mtendaji wa kampuni ya New Habari, alisema kwanza anamshukuru mungu kwa kushinda kesi hiyo ambayo imemsumbua kwa miaka miwili sasa na kwamba hukumu hiyo imeonyesha wazi kuwa kumbe ni kweli mahakama zetu zinatoa haki na kuwashukuru wanahabari na wadau wa habari waliokuwa nae bega kwa bega wakati wa kesi hiyo.

Naye wakili wa Kibanga, Nyaronyo Kichere alisema kesi hiyo ni ushindi kwa tasnia ya habari na kwamba waandishi wa habari wanayohaki ya kuandika makala za kuwakosoa askari wa majeshi yetu kwani ni kodi zetu ndiyo zinazowalipa mishahara.

Naye Meneja Maadili wa Baraza la Habari (MCT), Allan Lawa alieleza kuwa hukumu hiyo ni ushahidi tosha wa vita ya uhuru wa habari inayopiganwa na vyombo vya habari hapa nchini  ambayo imeanishwa wazi kwenye Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi.

Waandishi wa habari toka vyombo mbalimbali vya habari walifurika mahakamani hapo tangu asubuhi wengine wakisali kwa imani zao na baada ya hakimu Lema kutoa hukumu yake na kuwaachiria huru waandishi hao walikumbatiana kwa furaha na kumshukuru mungu na kumpongeza hakimu Lema kwa kutoa hukumu ambayo imerejesha faraja na amani kwa tasnia ya waandishi wa habari hapa nchini.

Itakumbukwa kuwa Mwigamba,Kibanda na Makunga walifikishwa mahakamani kwa siku tofauti.Mwigamba alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Desemba 8 mwaka 2011, Kibanda alifikishwa Desemba 20 mwaka 2011 na Makunga alifikishwa Machi 6 mwaka 2012 na washitakiwa wote walikanusha mashitaka.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 30 Mwaka 2014.

No comments:

Powered by Blogger.