Header Ads

ELIAS GOROI : SULUHU YA VITA YA KOO,WIZI WA MIFUGO RORYA


Na Happiness Katabazi

WILAYA ya Rorya iliyopo Mkoani Mara  ni miongoni mwa wilaya mpya hapa nchini ambayo pamoja na mambo mengine imekuwa ikisifika kwa baadhi ya wananchi wake kushiriki katika matukio ya wenyewe kwa wenyewe, wizi wa mifugo  n.k
Fuatana na Mwandishi wa makala hii   ambaye mapema mwaka huu alifika katika ofisi ya  Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Elias .G. Goroi , iliyopo Ingri Juu, Kata ya Mirare  Tarafa  ya Girango wilayani Rorya na kufanya nae mahojiano kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu wilaya hiyo

Swali: Hali ya ulinzi na usalama katika Wilaya ya Rorya ikoje kwasasa ukilinganisha  na miaka ya nyuma?

Jibi:Wilaya ya Rorya ni moja ya Wilaya tano (5) za Kiutawala Mkoani Mara na ni Halmashauri ya Wilaya miongoni mwa Halmashauri saba (7) zilizopo Mkoani Mara.  Mazingira ya Wilaya ya Rorya yanashabihiana na Wilaya nyingine na tabia za wakazi ni zile zile.  Hata hivyo kumekuwepo na matukio ya uhalifu unaolingana kwa muda mrefu, Wilaya ya Rorya na Tarime ni Wilaya zilizokuwa na matukio mengi na makubwa ya uhalifu huko nyuma kama vile; vita vya Kikabila na Koo, Wizi wa kupora mifugo kwa kutumia silaha za moto (Bunduki) na mauaji ya kisingizio cha ushirikina. 

Hali hii ilisababisha Serikali kulitangaza eneo hii la Tarime/Rorya kuwa Kanda Maalum ya Kipolisi.  Hii inamaanisha ongezeko la huduma za Kipolisi na kuimarika kwa hali ya Ulinzi na Usalama unalenga kupunguza matukio hayo ya kihalifu,  ukilinganisha na huko nyuma. 

Swali:Mmejipanga vipi kutokomeza  matukio ya mauaji?
Jibu:Wilaya imejipanga kutokomeza matukio ya mauaji kwa njia tatu (3) kubwa.Mosi; uhakikisha kuwa Ulinzi unaimarika katika ngazi zote kwa kutumia Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi husika.Pili Kuimarisha upashaji wa habari za matukio na taarifa za kiintelijensia.Tatu ni Kusimamia utawala wa Sheria na utoaji haki pamoja na kuimarisha Utawala Bora.

Swali:Hali ya uporaji  wa mifugo  kwa kutumia  silaha ikoje kwa sasa?
JIbu:Kama Wilaya majibu ya hapo juu, hakuna matukio makubwa.  Hali ya uhalifu mkubwa na hasa wizi na uporaji wa mifugo kwa kutumia silaha za moto nzito (bunduki) na silaha  za jadi naweza kusema umeisha.  Wizi wa kawaida wa kutumia silaha nao umepungua sana na wizi wa mifugo wa kawaida nao unaelekea kwisha na pale unapotokea unakuwa ni wizi wa ndani na mara nyingi umedhibitiwa na vyombo vya Dola.  Mifugo inayoibiwa kwa njia ya kawaida karibu yote imefanikiwa kukamatwa na kurejeshwa kwa wenyewe.  Watuhumiwa wengi hufikishwa mahakamani na kwa ujumla uhalifu hasa wizi wa mifugo, kwa kipindi cha miaka miwili (2012/2013), niliyokuwa hapa, umeonyesha kupungua kwa asilimia (82%) tofauti na miaka ya 2004 – 2011.  kwa miaka miwili hiyo hapajatokea uporaji wowote wa mifugo kwa kutumia silaha.  Haya ni mafanikio makubwa katika kipindi kifupi.

Swali:Hali ya ugomvi  kati ya Koo na Koo  iliyokuwa ikijitokeza huko  nyuma  ikoje?Mlitumia mbinu gani hadi mkafanikiwa kupungumza matukio hayo?

Jibu:Katika Wilaya za Rorya na Tarime, ukiweza kuthibiti wizi wa mifugo, kwa kiasi kikubwa, umethibiti vita na ugomvi wa Kikabila na Koo.  Kwa Wilaya ya Rorya, baada ya kuthibitiwa wizi wa Mifugo, ugovi wa Koo na Kikabila umepungua sana.  Pia ugomvi huu husababishwa pia na kugombea mipaka na Ardhi ya malisho na kilimo kati ya majirani ambao nao umeshashughulikiwa na kupungua sana.  Kwa miaka miwili hii hakujatokea vita vya ugomvi wa kikabila wa Koo.
Suala hili ni pana sana na siyo rahisi kuainisha mikakati yote tuliyotumia kama Serikali   na Mbinu zote tulizotumia hadi kufanikisha/kupunguza matukio hayo.  Hata hivyo nitaelezea machache ya msingi;-Mosi; Ushirikiano kati ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na vyombo vya Dola hasa Polisi na nyenzo Kuu iliyosaidia kupunguza matukio.  Hii iliongeza usimamizi wa pamoja na wa karibu.
Pili;Dhana ya ushirikishwaji wa Jamii, Vikundi vya Ulinzi na Ulinzi shirikishi ilipewa Mkazo wa hali ya juu.  Hii iliimarishwa doria za pamoja kati ya Polisi na Jamii (Polisi Jamii).  Hii imesaidia sana kuimarisha Amani na Utulivu katika Wilaya ya Rorya na kwa kutumia mpango wa Komandi za Wilaya, matukio makubwa yamethibitiwa kwa kiwango kikubwa sana.  Kupitia mpango huu makosa yote yamethibitiwa kwa zaidi ya asilimi 85% kulinganisha na asilimia 15% ya hapo awali (2004 – 2010).

Tatu, Kwa kuwa kiini kikubwa cha migogoro, ugomvi na vita ulijikita katika wizi na uporaji wa mifugo, Wilaya ilibuni dhana ya mazizi ya pamoja, ambapo Wananchi walishauriwa kuweka mifugo pamoja kwenye zizi la pamoja ili kurahisisha na kuimarisha Ulinzi, jumla ya mazizi takribani 20 yaliungana hasa katika Tarafa ya Girango (Kata za Bukwe, Koryo, Mirare, Goribe, Ikoma na Kitembe).

Nne; Kwa matukio mengi ya ugomvi na mapigano isiyo ya wizi wa mifugo, kwa kutumia dhana ya usuluhishi wa migogoro (Conflict Resolution) mapigano yamepungua sana.  Vita vya mwisho vya Kikabila/Koo ulitokea Kata ya Ikoma mwishoni mwa mwaka 2011 na kuisha kabisa mwaka 2012.
Mbinu hii pia imetumika kuelimisha watu juu ya madhara ya ushirikina, kuchomeana nyumba moto kwa madai hayo na kujichukulia sheria mikononi.  Hii imeenda sambamba na kutoa elimu juu ya Katiba,  sheria na kanuni za Utawala bora ili kupambana na tabia ya matumizi ya nguvu na kujichukulia sheria mkononi.  Shughuli ya utatuzi wa migogoro ni endelevu na inayohitaji mbinu mbali mbali na uzoefu ikiwepo kushauriana na kuelekezana na matunda yake ili yawe ya kudumu yanahitaji muda.  Kwa juhudi czote hizi Wilaya ya Rorya (Kata ya Bukwe) ilitunukiwa cheti cha kuwa Wilaya Salama Nchini mwaka 2012/2013, na I.G.P. SAID MWEMA.

Swali:Wilaya ya Rorya  ipo mpakani na nchi ya Kenya .Je kuna tatizo  la wahamiaji haramu  kutoka nchi jirani?

Jibu:Kama zilivyo Wilaya zote za Mipakani, Rorya nayo inayo majirani na mahusiano mazuri kati yao.  Katika mahusiano hayo inakuwa sio rahisi kutambua au kubaini nani mhamiaji na ni wakati gani uhamiaji na mahusiano yanapoanzia na kukomea.  Kwa uchunguzi uliofanywa na Idara ya Uhamiaji,Wilaya ya Rorya, wapo wahamiaji wapatao 107 Kata ya Ikoma pekee; (58 Kijiji cha Kogaja; Kijiji cha Ikoma wapo 31, na Kijiji cha Nyamasanda wapo 18) imebainika wahamiaji wengi waliingia Nchini muda mrefu uliopita na wengine kukaribishwa na jamaa zao kuishi nao bila kufuata taratibu za Nchi.  Tathimini inaendelea kubaini wengine sehemu nyingine.

Pamoja na ujirani, undugu na mahusiano ya Kijamii watu waliyonayo au wengine kuishi kwa muda mrefu, kwa mujibu wa sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995 kipengele cha 7, hatua zifuatazo za uhamiaji zinachukuliwa.

Mosi ni kuwaandisha  raia wote wa Kenya waishio Kata ya Ikoma kwenye daftari la wageni wakazi (kwa mujibu wa sheria).

Pili ni kuwafikisha mahakamani na kuwafungulia mashtaka baadhi ya raia wa Nchi mbali mbali walioingia bila Vibali.

Tatu,kuwafukuza raia wote wasio Watanzania walioingia hivi karibuni bila kibali kwa kuwapatia “Prohibited Immigrant Notice”.  Kazi hizi zote zinafanyika pamoja.  Kwa kazi inayoendelea,  pamoja na changamoto yake, hatujafikia kusema kuwa tunapata matatizo katika hili kwa sasa na tunaomba uzalendo utumike kwa wenyeji ili kufanikisha, kubaini watu hao.  Changamoto kubwa ni ushirikiano duni tunaopata kutoka kwa viongozi ngazi mbalimbali katika kuwafichua wahalifu wa uhamiaji.  Idara ya Uhamiaji Wilaya ikisaidiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya inaendelea kubaini wote wasio raia wa Tanzania.

Swali:Kuna madai kuwa baadhi ya wavuvi wa samaki katika Ziwa Victoria eneo la Rorya   wanatumia  nyenzo  haramu  ikiwemo  sumu kuvulia  samaki,hili unazungumziaje madai haya?

Jibu:Ndio, madai hayo ni ya kweli. Kama ilivyo tabia ya wavuvi wote kutaka kupata samaki wengi na kwa urahisi, tatizo hili linakabili sana uvuvi wa Ziwa Victoria ikiwepo Wilaya ya Rorya, kwa Mfano; katika doria “Operesheni Maalum” ya mwezi wa Desemba, iliyofanywa Mkoani Mara kwa ajili ya kuondoa zana zote harama za uvuvi zinazotumika kwenye maji ya Ziwa Victoria, katika Wilaya za Bunda, Butiama, Musoma na Rorya,  jumla ya zana haramu za uvuvi 11620 kamba (Kokoro) zenye urefu wa mita 53020, samaki wachanga kilo 1830, na jora moja la wavu wa dagaa  vilikamatwa.  Kwa Rorya pekee, zilipatikana kokoro 32, Timba 1139, nyavu za Makila 1240, nyavu za Tupa tupa 29, majora ya wavu wa dagaa 9, na kamba za kuvuta kokoro mita 11920.  katika doria ya Operehsni hiyo samaki wachanga  aina ya Sangara wa Rorya walikamata kilo 120 na Sato kilo 21.

Takwimu kama hizi zinaonyesha uwepo wa tatizo lakini pia rasilimali ya uvuvi kuwa katika hatari ya kutoweka iwapo hatua za maksudi hazitachukuliwa haraka kukabiliana na hali hiyo hatari.  Natoa  wito kwa kila mdau wa tathnia ya uvuvi wa walaji kushirikiana kuchukua hatua stahiki na endelevu.  Hii ni pamoja na kupambana na matumizi ya sumu (mabomu) katika uvuvi Ziwani ambao pia ni hatari kwa Afya ya walaji.  Kikosi cha Askari Wanamaji, kushirikiana na Askari Polisi wa kawaida na nyakati mbali mbali kushirikisha vikundi vya “Beach Management Units” (BMU) kwa nyakati tofauti hufanya doria Ziwani,  ingawa hukabiliwa na ukosefu wa nyenzo za kazi kama vile mafuta ya Boti.

Swali:Wewe Kama Mkuu wa Wilaya ya Rorya , tueleze ni kwanini  baadhi ya watu wa wilaya yako wamekuwa wakisifika kwa kujichukulia sheria mkononi  kwa kuwaua wenzao. Je  hilo linasababishwa na umbumbumbu wa sheria?

Jibu: Nimekaa Rorya kwa muda mfupi (miaka mmoja na nusu) muda ambao hautoshi kuzoea na kuzifahamu tamaduni zote za watu.  Lakini ni na kubaliana nawe kuwa Rorya, kama Wilaya nyingine Mkoani Mara, zipo tabia za baadhi ya watu kujichukulia sheria mikononi na kusababisha mauaji ya binadamu.

Kwamba ni umbumbumbu wa sheria yaani ni kutofahamu sheria ni suala la kutafakari na utafiti wa kina.  Rorya ni Wilaya ya Vijiji (Rural District) kama Wilaya nyingi Tanzania.  Tabia hii unayoulizia, kama ingekuwa ni kutojua sheria, basi ligekuwa ni tatizo la Nchi nzima yaani Wilaya nyingi. 

Sikatai kuwa umbumbumbu wa sheria unachangia, bali siyo sababu pekee.  Wakati mwingine tatizo hili linachangiwa na ushiriki au hamasa toka kwa baadhi ya viongozi.  Ikitokea hivyo hatuwezi kusingizia umbumbumbu wa kutojua sheria.  Lakini pia linaweza kuchangiwa na imani mbalimbali hasa zile za kishirikina na hapa ndipo kazi ya elimu inapotakiwa kuhimizwa ili watu waelimike waache imani hizi za kipuuzi na hatari.  Ili tuondokane na hali hii vizuri kila kiongozi kupiga vita tabia hii na sote kufuata na kusimamia Utawala Bora na Utawala wa sheria.

Swali: Hivi karibuni  pametokea  mgongano  kati ya viongozi  wa serikali na viongozi wa kisiasa  hapa Rorya , tatizo nini?

Jibu: Migogoro ya kazi na uelewa duni wa majukumu lazima unaleta matatizo  mahali popote pa kazi.  Matatizo yanayosababisha aina za migogoro ni mengi yakiwemo, labda, ufahamu mdogo wa mipaka ya kazi na wajibu wa kila mmoja.  Lakini pia yanaweza kusababishwa na pale maslahi ya watu, (siyo ya Chama/Vyama) yanapo hatarishwa kwa njia moja ama nyingine.  Lakini pia migongano ya mifumo kati ya Utawala bora na mifumo ya ubabe katika Uongozi vinaweza kuwa tatizo kisiasa.  Hivyo siyo rahisi mimi kueleza tatizo linalopelekea kuwepo migogoro mpaka nijue ni kati ya nani na nani, katika ngazi gani na uhalisia (nature) wa mgogoro. Kubwa hapa ni kuwataka viongozi kujua mipaka ya kazi na majukumu yao.

Swali:Rekodi zinaonyesha  mapato ya Halmashauri  ya Rorya  yalikuwa  chini ,lakini  hivi sasa yanaonekana kuongezeka .Je mlitumia  mbinu  gani kuongeza  mapato?

Jibu:Ni kweli mapato ya ndani (Proper Own Source) ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya yalikuwa chini kwa mfano; mwaka 2011/2012 ongezeko lilianza kuonekana ambapo makusanyo yalikuwa Sh. 282,988,921/= mwaka 2012/2013 mapato yakafikia Sh. 327,964,125/=.  Hii ni ongezeko la Sh. 44,975,284/= ongezeko hili ni kubwa ukichukulia kuwa linatokana na mbinu ya muda mfupi (mwaka mmoja) mbinu iliyotumika ni kuthibiti ukusanyaji wa mapato hasa kwenye Mialo ya Samaki.  Wilaya ilifanya tathimini upya ya vyanzo vyake vya mapato vyote na kubaini kwamba baadhi ya vyanzo vilikuwa vilitozwa ushuru aidha mdogo au chini ya uhalisia, hivyo viwango vilirekebishwa.  Pia ilionekana kuwa vipo vyanzo ambavyo havijabainishwa hivyo viliongezwa kama vyanzo vipya.

Kwa mikakati hii, pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji, mwaka huu katika kipindi cha nusu mwaka Julai – Desemba,2013/2014 makusanyo yamefikia Sh. 201,838,652/= ongezeko la Sh. 81,150,269/=. Ili kuongeza mapato zaidi tunatarajia kuimarisha vyanzo vingine kama vile Minada ya Mifugo na kumpata mtalaam Mshauri aliyebobea katika masuala ya ukusanyaji mapato atufanyie tathimini ya jinsi ya kuboresha vyanzo vya mapato ya ndani kwa kupata uhalisia wa mapato na vyanzo.  
Swali: Hali ya kisiasa wewe kama Mkuu wa Wilaya  ya Rorya  na mjumbe  wa Kamati ya siasa ya wilaya.Vipi  hali  ya Kisiasa ya Rorya ikoje?

Jibu: Ni kweli mimi ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Chama cha Mapinduzi kwa mujibu wa Katiba ya CCM. Kama Mjumbe mimi siyo msemaji wa Kamati wala wa Chama (CCM). 
Lakini kama mwanachama na Kada mzoefu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), nami nitahitaji pia kuuliza kwa wasemaji wa Chama  Wilaya, Jee hali ya kisiasa Rorya ikoje? (Kama Mkuu wa Wilaya, hawezi kusema kuwa, hali ya Kisiasa kwa ujumla ndani ya Halmashauri ya Wilaya ni nzuri.  Upo ushirikiano wa Viongozi wa vyama vyote , hasa Waheshimiwa Madiwani, katika uendeshaji wa shughuli za maendeleo.  Kwa ufupi, tukiacha mambo ya ndani ya vyama vyenyewe, ambayo yana wasemeji wa kila Chama, hali ya jumla ya Kisiasa imekuwa shwari muda mrefu.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 19 Mwaka 2014.

No comments:

Powered by Blogger.