Header Ads

LIYUMBA HANA HATIA-WAKILI

Na Happiness Katabazi

MAWAKILI wa upande wa utetezi katika kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatusi Liyumba umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone mteja wao hana hatia kwasababu hakuwa na mamlaka ya kuamua jambo lolote ile katika mradi wa ujenzi wa mradi wa majengo pacha.


Ombi hilo ambalo ni majumuisho kesi hiyo yaliwasilishwa jana saa sita mchana mahakamani hapo kwa njia ya maandishi na mawakili hao Onesmo Kyauke, Majura Magafu na Hudson Ndusyepo na Jaji Mstaafu Hillary Mkate.Kuwasilishwa kwa majumuisho hiyo kunatokana na utekelezaji wa amri iliyotolewa Mei 7 mwaka huu, na Kiongozi wa Jopo la Mahakimu wakazi wanaosikiliza kesi hiyo Edson Mkasimongwa ambaye aliutaka upande wa Jamhuri na utetezi jana uakikishe kila upande unawasilisha majumuisho yao.

Lakini katika hali isiyotarajiwa hadi saa 10:40 jioni waandishi wa habari za mahakamani waliokuwa wameshinda mahakamani hapo tangu saa mbili asubuhi kwaajili ya kufuatilia kesi mbalimbali ikiwemo majumuisho ya kesi hiyo hawakufanikiwa kuwaona mawakili wa serikali wanaondesha kesi hiyo kuwasilisha majumuisho hayo hali iliyowalazimu waandishi hao kwenda ofisini kwa Hakimu Mkuu Mkazi Elvin Mgeta ili waweze kuthibitishiwa kama upande wa Jamhuri umeleta au haujaleta majumuisho hayo, lakini Mgeta ambaye ndiye mkuu wa mahakama hiyo alisema yeye hawezi kuthibitisha kama wameleta au hawajaleta na kuwaomba waandishi wa habari wafike leo asubuhi ofisini kwake atakuwa tayari ana taarifa kamili kuhusu jambo hilo.

Kwa mujibu wa nakala ya majumuisho ya upande utetezi ambapo Tanzania Daima ina nakala yake, wanaiomba mahakama imuone mshtakiwa hana hatia hivyo imuachirie huru kwani Liyumba kama Liyumba hakuwa na mamlaka ya kuamua jambo lolote kuhusu mradi huo kwani mradi ulikuwa ukiratibiwa na Meneja Mradi Deogratius Kweka ambaye ndiye alikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Gavana Daud Balali kuhusu masuala yanayohusu mradi ule.

“Liyumba kazi yake ilikua nikuakikisha ule mradi hauwezi kukosa vitu kama usafiri, steshenali na maitaji mengine muhimu...na kwamba mshitakiwa alikuwa anawajibika kujibu barua zilizokuwa zinatoka kwa mkandarasi zinazohusu mradi kama alivyokuwa akielekezwa kuzijibu barua hizo na Gavana baada ya Gavana kuwa ameishajadiliana na Meneja Mradi;

“Kwani Meneja Mradi ndiye aliyekuwa anakaa na wakandarasi na wanajadiliana nini kifanyike na kisha Meneja Mradi anapeleka mapendekezo hayo kwa Gavana na kisha gavana anatoa maamuzi ...hivyo Liyumba hausiki kabisa na kosa hili la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambalo upande wa Jamhuri umedai alijichukulia madaraka bila idhini ya bodi ya wakurugenzi kwa kufanya mabadiliko ya ongezeko za mradi wa ujenzi huo”alidai Wakili Onesmo Kyauke.

Hakimu Mkazi Edson Mkasimongwa anayesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa Mei 24 mwaka huu, watatoa hukumu ya kesi hii ambayo inavuta hisia za wanchi wengi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 14 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.