Header Ads

LIYUMBA AKATA RUFAA KORTI KUU

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba(62) ambaye Jumatatu wiki hii, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimhukumu kwenda jela miaka miwili baada ya kumkuta na hatia la kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, jana amekata rasmi rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akipinga hukumu hiyo.


Rufaa hiyo iliwasilisha jana saa tatu asubuhi na kupewa Na.56 ya mwaka huu,katika Mahakama Kuu na mawakili wa mrufani(Liyumba), Majura Magafu, Onesmo Kyauke, Jaji Mstaafu Hillary Mkate na Hudson Ndusyepo.

Kwa mujibu wa rufaa hiyo ambayo gazeti hili imefanikiwa kuiona nakala yake, mrufani ametaja sababu 12 za kukata rufaa ya kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakimu wa Kazi wawili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa ambao ndiyo waliomtia hatiani mrufani Wakati aliyekuwa kiongozi wa jopo hilo la mahakimu hao wakazi Edson Mkasimongwa alitoa hukumu yake peke yake na akamwachiria huru mrufani na hukumu ya hakimu huyo imeifadhiwa na kwenye kumbukumbu za mahakama hiyo.

Sababu ya kwanza ya kukata rufaa, mrufani anadai mahakama ya Kisutu ilishindwa kuchambua ushahidi uliotolewa mahakamani kikamilifu na matokeo yake jopo hilo la mahakimu wakazi wa tatu likajikuta linatoka na hukumu mbili tofauti.

Sababu ya pili, mrufani anadai kwamba mahakimu hao wawili (Mla ilifanya makosa kwa kushindwa kwake kukubali mabadiliko ya ujenzi wa mradi wa ujenzi wa Minara Pacha yalifanywa baada ya Meneja Mradi huo Deogratius Kweka kuketi kwenye kikao na timu ya wataalamu wa ujenzi na kujadili shughuli za mradi huo,kwani kwa mujibu wa ushahidi uliopo kwenye rekedi za mahakama hauonyeshi Liyumba alikuwa akiudhuria kwenye kikao hicho cha wataalamu wa masuala ya ujenzi wa mradi.

Mrufani katika sababu ya tatu anadai mahakimu hao wakazi wawili(Mlacha na Mwingwa) walifanya makosa kwa kushindwa kwao kukubali kwamba shughuli zote za uendeshaji wa mradi ule zilikuwa chini ya Meneja Mradi Deogratius Kweka ambaye alikuwa akiwajibika moja kwa moja kwa Gavana na si kwa mrufani(Liyumba).

Katika sababu ya nne, mrufani anadai mahakimu hao wawili walifanya makosa kwa uamuzi wao wa kuutupilia mbali ushahidi uliotolewa na Liyumba na shahidi wake ambaye alikuwa Kaimu Katibu wa Benki Kuu, Bosco Kimela kwa maelezo kuwa mashahidi wote walikuwa wakiishi pamoja katika gereza la Keko.

“Sababu ya tano, mahakimu hao walifanya makosa kwa kusema kwamba Liyumba na Kimela ushahidi wao ulikuwa kama hadithi ya kutunga....sisi tunapinga hoja hiyo ya mahakama kwa kusema ushahidi huo haukuwa hadithi ya kutunga.

“Sababu ya sita ni mahakama ya Kisutu ilifanya makosa iliposema malipo ya mradi huo yalikuwa yakiidhinishwa na Liyumba...sisi tunapinga hoja hiyo ya mahakama kwani ni wazi kwa mujibu wa ushahidi uliopo kwenye rekodi ya mahakama hauonyeshi Liyumba alikuwa akiidhinisha malipo ya mradi huo, sasa ushahidi huo hao mahakimu wameupata wapi?alidai mrufani.

Aidha aliitaja sababu ya saba ni kwamba mahakama ya kisutu ilifanya makosa kusema Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ilipoteza mwelekeo na kwamba Liyumba na aliyekuwa Gavana marehemu Daud Balali walikuwa wakiiburuza bodi hiyo.Magafu anadai hoja hiyo ya mahakama ni ya kufikirika na hata ushahidi uliopo kwenye rekodi ya mahakama hauonyeshi mahali popote kwamba bodi hiyo ilikuwa ikiburuzwa na mrufani.

Alidai sababu ya nane ni mahakama hiyo ilifanya makosa kusema idhini za mabadiliko ya ujenzi wa mradi wa Minara Pacha zilitolewa baada ya utekelezaji kufanyika hazikubariki kisheria, wakili huyo anadai kuwa hoja hiyo ya mahakama si ya kweli kwasababu idhini zote zilizokuwa zikitolewa zinaruhusiwa na Kanuni za Fedha za Benki Kuu(BoT Financial Regulation).

“Sababu ya tisa ni kwamba mahakama ya Kisutu ilifanya makosa iliposema mrufani hakuwa na mamlaka ya kusaini zile barua ambazo zilikuwa zimeandikwa na mrufani kwaniaba ya BoT ambazo zilikuwa zikienda kwa mkandarasi ambazo ni kielelezo cha 5-12 na kwamba alifanya hivyo kinyume cha sheria....sisi mawakili wa mrufani tunasema hilo si kweli.

“Sababu ya kumi,mahakama hiyo ilifanya makosa iliposema kwamba mabadiliko ya mradi ambayo yalisababisha ongezeko la gharama katika mradi ule yalikwenda kinyume na matakwa ya bodi na kwamba bodi iliathirika”alidai mrufani.

Sababu ya 11, mrufani anadai mahakama ilikosea kusema kwamba upande wa Jamhuri katika kesi hiyo uliweza kuthibitisha kesi yake bila kuacha mashaka yoyote dhidi ya mrufani, wakili wa Liyumba anadai hilo si kweli kwani ushahidi ule wa upande wa mashtaka umeacha mashaka makubwa.

Aidha sababu ya 12, mrufani anadai mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilifanya makosa kwa kushindwa kwake kufuta taratibu zilizoainishwa kisheria katika kutoa adhabu.

Jumatatu ya wiki hii, mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu yaani mahakimu wawili(Mingwa na Mlacha)ilimhukumu mrufani kwenda jela miaka miwili baada ya kumtia hatia kwa kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma.Na hadi sasa mrufani anaishi katika Gereza la Ukonga.

Lakini wakati mahakimu hao wakimtia hatiani hakimu mmoja ambaye ndiye aliyekuwa kiongozi wa jopo la mahakama hiyo alikataa kumtia hatia mrufani na akamuachiria huru kwasababu alibaini ushahidi wa upande wa mashtaka unaning’inia.

Hali hiyo ya mahakimu kutofautiana na kusababisha kutoa hukumu mbili kulifanya mahakama hiyo kuandika historia mpya ya kesi moja iliyokuwa ikiendeshwa katika mahakama ya hakimu mkazi imekuwa na hukumu mbili tofauti.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Mei 29 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.