Header Ads

MAJUMUISHO YAKWAMISHA KESI YA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwamba wameshindwa kuwasilisha majumuisho ya kesi hiyo kwa sababu mahakama haijawapatia majumuisho sahihi ya mwenendo wa kesi hiyo.


Wakili wa serikali, Ponsian Lukosi alidai mbele ya kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Edson Mkasimongwa, kuwa wameshindwa kuwasilisha majumuisho hayo jana kama walivyoamriwa na endapo watapatiwa watawasilisha mara moja.

Hakimu Mkazi Mkasimongwa alikiri kuwa nakala halisi ya mwenendo wa kesi hiyo bado haijatolewa na kwamba mahakama hiyo itafanya jitihada, ili Jumatatu ijayo pande zote zipatiwe mwenendo wa kesi hiyo na kuwa ifikapo Mei 13 mwaka huu, pande zote ziwasilishe mahakamani majumuisho yao.

Alisema kutokana na hali hiyo, kesi hiyo itatajwa Mei 21 na hukumu itatolewa Mei 24 mwaka huu.

Januari 26, mwaka jana, Liyumba na Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka hayo ya kuidhinisha mradi wa majengo ya minara pacha bila idhini ya bodi ya wakurugenzi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Mei 8 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.