Header Ads

KULIKONI DUKA LA VITABU LA SERIKALI?

Na Happiness Katabazi
DUKA la Vitabu la serikali ambalo wajibu wake ni kuuza nakala za sheria zinazotungwa na Bunge , halitekelezi wajibu wake ipasavyo.
>Duka hili la serikali kwanza linatakiwa liwe na matawi wilaya zote na mikoa yote ya hapa nchini, kwasababu msingi mkuu wa sheria za nchi yetu ni kwamba kila raia ana wajibu wa kujua sheria na kutojua sheria siyo utetezi.

Kwa hiyo wajibu wa kuchapisha sheria na kuzisambaza kwenye maduka yote ya serikali nchini ni wajibu wa kwanza wa dola linaloendeshwa kwa mujibu sheria.

Hii ina maana gani?Moja;Ina maana kwamba kwana gazeti la serikali na taarifa za sheria zinazotungwa na bunge litoke kila mwezi , hili halifanyiki ipasavyo kwani wakati mwingine linachelewa kutoka.Na hii ina maana kwamba serikali yetu haizingatii msingi wa uwazi ambao ni msingi mkuu wa utawala bora.

Pili; sheria zinazotungwa na bunge hazipatikani ,kila tunapokwenda kwenye duka la vitabu la serikali lililopo Mtaa wa Jamhuri jijini Dar es Salaam, unaambiwa sheria hizo zimekwisha na hawajui lini zitachapwa na ofisi ya Mpigachapa wala lini zitafikishwa dukani hapo.

Mfano mzuri ni nakala Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 2002,Sheria ya Madai,Katiba kwa kipindi cha miezi mitatu sasa hazipo na haijulikanizitapatikana lini.

Tatu;duka hilo halina matawi nchi nzima bali lina maduka madogo Iringa,Mwanza,Arusha,Zanzibar na kwingineko , hii inamaanisha hata duka hilo lingekuwa na nakala za kutosha,mtandao wa maduka ya vitabu vya serikali ni finyu mno.Je !haiyumkiniki mwananchi kutoka kijiji cha Nyakayanja Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, kusafiri kutoka huko kuja Dar es Salaam kununua sheria za nchi?

Kwa mujibu wa dhana ya sheria kwamba kila mwananchi ana wajibu na haki ya kujua sheria , basi ni wajibu wa serikali kuwa na maduka ya vitabu vya serikali katika kila wilaya.

Ikiwa hili halifanyiki ni makosa na ikiwa wananchi hawajatambua ni haki yao kupata nakala za sheria basi ni matokeo ya ujinga.Ama sivyo kama utaratibu huu utaendelea itabidi kutunga msingi mpya wa sheria unaomwezesha raia kujitetea kwamba hajui sheria kwa kuwa hazipatikani madukani kwa wakati.

Wanasheria waliobobea na mahakimu , majaji hata waendesha mashtaka waliofanyakazi mikoani,wanasemaga huko hakuna sheria kwa kuwa hata baadhi ya mahakimu wenyewe hawana nakala za sheria wanazotakiwa wazitumie kuamria baadhi ya kesi.

Baadhi ya Waendesha mashitaka hawana nakala ya sheria anayoitumia kuendeshea mashtaka kwa maana hii watendaji wote hawa wanajikuta ni wababaishaji wasiyo na uhakika na kile wanachokifanya au wanaishia kuazima sheria hizo.Kwa mantiki hiyo wapo wananchi wengi ambao wamejikuta wakipoteza haki zao au hata kutumikia vifungo jela kwa makosa ambayo hayamo kwenye sheria za nchi.

Na mfano hai ambao si wa kutafuta ni kesi ya ubakaji na kulawiti watoto wa shule ya msingi inayomkabili Mwanamuziki mahiri wa dansi nchini Nguza Viking(Babu Seya) na wanawe watatu ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliwahukumu kutumikia kifungo cha maisha jela baadaya kuwatia hatiani kwa makosa hayo.Lakini mapema mwaka huu, Majaji watatu wa mahakama ya rufaa nchini , Jaji Nataria Kimaro, Mbarouk Mbarouk na Salum Massati iliwafutia washitakiwa mashitaka yote sita ya kulawiliti na kubakiza mashitaka matano ya ubakaji.

Jopo hilo la majaji wa tatu lilisema limefikia sababu ya kuyawafutia mashtaka hayo ya kulawiti kwasababu Tanzania haitambui kosa la kulawiti kwa kushirikiana(gang sodomie).Kwa uamuzi huu wa mahakama ya rufani ambao uliwaachiria huru mrufani wa tatu na wanne na kuwatia hatiani mrufani wa kwanza na wapili, mtakubaliana nami kwamba mahakama hizo za chini ziliwahukumu warufani adhabu hiyo kwa makosa hayo ya kulawiti ambayo hayapo kwenye sheria za nchini yetu.

Kwa hiyo maduka ya serikali ni muhimu mno katika kufanikisha utawala bora.Maduka hayawezi kuachwa holela holea lazima sasa itungwe sheia itakayotawala uendeshaji wa maduka ya serikali kwa dhana nzima ya utawala itategemea ufanisi wake.

Dhana dhima ya haki itategemea ufanisi wa maduka hayo.Wananchi hawawezi kujua wana haki gani kama hawana nakala za sheria kwasababu eti hazipatikani .Hataishiwa kuonewa tu.

Sasa sheria za uendeshaji wa maduka ya vitabu vya serikali iweke masharti ya maduka hayo, yatengewe fedha katika bajeti ya kutosha ya serikali kila mwaka ili kuakikisha sheri zote zinachapishwa na zinapaikana kwa urahisi kote nchini.

Ieleweke kwamba kuendeleza hali hii ya uahidimu wa machapisho ya sheria za nchi ni kichocheo kikubwa cha rushwa kwa kuwa mwananchi anajikuta hajui hazi zake kila mara.Pia kukosekana kwa machapisho ya sheria za nchi ni chanzo cha utawala usiojali haki na sheria kwa kuwa watawala wanajificha maovu yao katika ujinga wa wananchi.

Hicho pia ni chanzo cha umaskini wetu kwasababu kwa kutojua sheria haki za wananchi zitaporwa kila siku na baadhi ya watendaji wa serikali ni manyang’au na miungu watu na kuwasababishia wananchi umaskini.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Mei 2 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.