Header Ads

UTAWALA BORA TANZANIA U WAPI?


Na Happiness Katabazi
WAPENZI wasomaji wa makala zangu napenda kuwaarifu kuwa kuanzia Jumapili ya leo na Jumapili zijazo nitakuwa na safu yangu ambayo itatambulika kwa jina la FUKUTO LA JAMII, hivyo mtakuwa mkizisoma makala zangu kupitia safu hiyo.Karibuni.

Serikali ya awamu ya nne ,imejivika joho la utawala bora .Katika matendo yake ndani na nje ya nchi serikali hii imekuwa ikidai kwamba imebobea katika utawala bora.

Ieleweke wazi kwamba utawala bora siyo tu utawala wa kufuata Katiba na sheria,uwazi na uwajibikaji bali kutenda mambo na kuendesha serikali kwa ufanisi na uweledi unaostahili.

Inapokuwa kwamba sheria inatoa haki au kupiga marufuku jambo fulani , ni wajibu watendaji wa serikali kuakikisha haki hiyo ina wafikia wadau wake.Haki kutowafikia wadau inaweza ikasababishwa na serikali kutowaamasisha wadau kutojua haki zao kwa kutumia elimu ya uraia au serikali kwa chombo kikuu cha uvunjaji wa haki.

Pale ambapo sheria inapiga marufuku jambo fulani lisitendeke , ni wajibu wa serikali kupitia elimu ya uraia kwa kuwaamasisha raia wake wasitende jambo hilo na pia ni wajibu wa serikali kuweka mfumo wa watendaji wenye taaluma na weledi wa kutosha ili kuwawajibisha wakiukaji wa sheria hizo.

Hapa nchini hayo yote hayafanyiki ,serikali haina mfumo wa elimu ya uraia wala haina utaratibu unaofaha wa kuajiri watendani wenye taaluma na weledi wa kutosha.

Kwa hiyo ukienda mahakamani utakutana na waendesha mashtaka wasio na weledi wa kutosha wa kuweza kuandaa hati za mashtaka na kuyawasilisha mahakamani.

Kesi nyingi ushindwa kwasababu baadhi ya waendesha mashtaka wanaanda hati mashtaka vibaya au wameendesha mashtaka vibaya.Katika kesi nyingi mtu wa kawaida ambaye ajasomea sheria anaona wazi mshitakiwa kaonewa au kabambikiwa kesi.Kila mara serikali inaposhindwa kesi katika kesi hiyo ni aibu kwa dola la Jamhuri ya Muungano.

Ukienda mahakamani utakutana na baadhi ya majaji na mahakimu, hao hawatakiwi kabisa kuamua kesi bila shinikizo, upendeleo,wanatakiwa wawe waaminifu na wenye weledi wa kutosha.Lakini huko huko mahakamani tunashuhudia baadhi ya watuhumiwa wakipatikana na hatia pasipo stahili au wahusika kwenye kesi za madai kupoteza haki zao ama kwasababu jaji au hakimu hana utaalamu na weledi wa kutosha au kapokea rushwa.

Lipo jambo linalosikitisha zaidi unaposikia tetesi kwamba katika kesi fulani baadhi ya vigogo wa serikali wametoa maelekezo kwa wakili wa serikali au mahakama kesi iamuliwe kwa misingi ya kulinda maslahi ya serikali au watu fulani badala ya misingi ya haki.

Tunaona wazi mambo hayo yakifanyika, wafanyakazi wakinyimwa haki za ajira kwa kuwa serikali imeagiza maslahi ya wawekezaji yalindwe.Kwa maana hiyo wafanyakazi,wafugaji,wakulima au wananchi kwa ujumla wamepoteza haki zao ama za ajira, maeneo waliyokuwa wakiyamiliki kwa kuwa serikali imeagiza mslahi yalindwe.

Kaumua kesi kwa misingi hiyo ya ‘vimemo’ siyo sawa na kuamua kesi kutokana na vishawishi vya rushwa na inawezekana baadhi ya mahakimu na majaji wanaotenda hivyo wanajua wazi hawatendi haki kwa kuwa tu ni waoga wa kupoteza kazi au wameaidiwa vyeo na marupurupu mengine.

Aina hii ya uendeshaji wa serikali si utawala bora na ni chanzo cha wananchi kukosa imani na mhimili wa mahakama,dhuruma inayoletea wananchi umaskini.

Tumesikia na ni kweli kwamba kunaucheleweshwaji wa kesi wa makusudi wakati mwingine ni wa makusudi jambo ambalo linasababisha kero na umaskini mkubwa.

Wahusika katika kesi za madai na jinai ushindwa kuendeleza shughuli zao kwasababu ama wapo rumande ama mahakama haijaamua kesi husika kwasababu upelelezi haujakamilika au mashahidi hawatokei mahakamani .Yote hayo ukwamisha shughuli zinazowaingizia vipato kwa watu ambao mwisho wasiku mahakama inawaona hawana hatia.

Serikali haina budi kurekebisha ali za wananchi hao auhata kuwafidia hasara waliyoipata maishani mwao.Tayari zipo kesi ambazo zimefuguliwa kwa mbwembwe kama kesi ya EPA,matumizi mabaya ya ofisi ya umma inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi wa utumishi na utawala wa Benki, Amatus Liyumba ambayo hukumu yake itatolewa Mei 24 mwaka huu, kesi ya mauji inayomkabili Ramadhani Mussa na mama yake mzazi ambapo Ramadhani anadaiwa kukutwa na kichwa cha mtoto marehemu Salome Yohana iliyopo mahakama ya Kisutu, na kila kukicha waendesha mashtaka wamekuwa wakidai jarada la kesi hiyo lipo kwa DPP hivyo kesi inapigwa kalenda, utafikiri ofisi ya DPP ipo mbinguni ambapo kufika kwake lazima mtu afe kwanza.

Kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma inayomkabili Mkurugenzi wa BoT, Simon Jengo ,Kisima Mkango,Bosco Kimela na Ally Bakari na wenzake wawili, ambapo hata hivyo vigogo hao walifunguliwa kesi ya kusababisha hasara y a Sh bilioni 104 katika Mahakama ya Ilala, Septemba mwaka jana.

Lakini Mei 7 mwaka huu, DPP aliwasilisha hati ya kuifuta kesi hiyo lakini muda mfupi washitakiwa watatu kati ya wanne walikamatwa tena na kufunguliwa kesi nyingine mpya ya matumizi mabaya, na aliyekuwa mshitakiwa watatu Bosco Kimela aliachiriwa huru baada ya DPP kusema hana nia tena ya kumshtaki.Washtakiwa wote watatu wanaendelea kusota rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Utaratibu rufaa katika kesi zilizokwisha amliwa mara zote ni mgumu hasa ule wa kukata toka Mahakama Kuu kwenda Mahakama ya Rufaa nchini.Ilivyo hivi sasa kanuni za uendeshwaji wa rufaa katika mahakama ya rufaa ni za kiufundi mno kuliko za utendaji wa haki.

Mfano hai ni Mahakama Kuu imekuwa ikisoma hukumu yenye tarehe isiyoendana na tarehe ya siku iliposomwa hukumu husika na kwa dosari hiyo tu waombaji rufaa wengi zilizokosewa tarehe , mahakama hiyo ya juu nchini inazitupa na inabidi sasa waombaji wa rufaa waanze upya mchakato wa kupata hukumu na amri yenye tarehe sahihi na na kuwasilisha ombi la kuongezewa muda wa kukata rufaa, zoezi hilo kwa pamoja linaweza likachukua hadi kipindi cha mwaka mmoja.

Je kwa utaratibu huo haki iliyochelewa hivyo ni haki?Na hao waomba rufaa hawatafilisika kweli.?

Mfano wa mahakamani ni mmoja tu katika mifano mingi ambayo tunaweza kutoa katika utendaji wa serikali yetu .Tunachotaka kusema kwamba nchi yetu ina miaka 46 toka ilivyopata uhuru , na nchi yetu inawataalamu wa kutosha.

Ni wakati sasa wa kutathimini utendaji kazi wa serikali yetu,ubora wa sheria zetu, ubora wa mifumo ya utawala na sheria an utendaji haki kwa ujumla ili turekebishe na kujenga upya dola la Kikatiba na Sheria zilizobora.

Mungu ibariki Tanzani, Mungu Ibariki Afrika.

0716 774494:
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili la Mei 23 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.