Header Ads

UCHAGUZI MKUU BILA KATIBA MPYA?

Na Happiness Katabazi
UCHAGUZI Mkuu wa nchi ni njia kuu ya kuwashirikisha wananchi katika utawala na uongozi wa nchi.


Taifa lolote lenye uhai wa kisiasa na mategemeo ya kuwa na maendeleo shindani katika jamii ya kimataifa , uupa uchaguzi mkuu kipaumbele na uzito katika siasa na bajeti ya taifa.

Dunia ipo katika uwanja wa mashindano ya maendeleo.Mataifa yanayokimbilia fursa za kujipatia ustawi wa kasi kwa raia wake kuliko mataifa mengine.

Viongozi wa kisiasa wanaotamba duniani ni wale wanaoweza kuziongoza nchi zao kupata maendeleo makubwa na ya kasi kuyashinda mataifa mengine.

Afrika hatumo katika ulimwengu huo na kwa vyovyote vile Tanzania inashikiria nafasi za nyuma kabisa katika kasi ya maendeleo ya nyuma ya dunia.

Nchi zilizo na rasilimali duni kama Rwanda na Burundi ziko mbali kimaendeleo kuizidi nchi yetu .Mataifa yasiyo na rasilimali kama vile dhahabu ,almasi ,Tanzanite kama vile Malawi yako mbele kimaendeleo kuizidi nchi yetu.

Ni wazi kuwa hata kama yangegunduliwa mafuta ya Petroli bado Tanzania ingeendelea ‘kuchapa lapa’ katika umaskini.Kwa vyovyote vile tatizo la nchi yetu si upungufu wa rasilimali bali taifa letu ni fukara sana kiuongozi.

Hiyo ndiyo sababu kubwa ya umaskini wetu.Hatuna viongozi wenye upeo wa kuweza kuliongoza taifa kupata mageuzi ya haraka ya Sayansi na Teknolojia na kupata maendeleo ya haraka kiuchumi na kijamii.

Uchaguzi mkuu ni njia kuu ya Kikatiba ya kujikomboa katika hali kama hii ikiwa kila mwananchi analitambua hilo.

Tunaelewa fika kuwa tumeishaingia katika mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1992 .Na tumekuwa na nafasi ya kubadili serikali mara tatu sasa katika uchaguzi wa mwaka 1995,2000 na 2005.

Oktoba mwaka huu, tutapata tena fursa kwa mara ya nne kubadili uongozi wa nchi kwa njia ya kidemokrasia,kura ya kila mmoja wetu ina maana kubwa katika kuleta mabadiliko tunayoyatamani na kuyazungumzia.

Hakuna kura isiyo na thamani kwa muktadha wa hoja hii.Endapo kila mtanzania mwenye haki ya kupiga kura atapiga kura kwa kudhamilia kubadili uongozi wa nchi hii ili tuongozwe na watu wenye upeo wa kuleta maendeleo.Tutafika.

Endapo kila mwananchi mwenye upeo wa kuliongoza taifa hili kufikia maendeleo ataacha kuwa mbinafsi na badala yake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uogozi ama katika sehemu yake ya kazi akatimiza wajibu wake kikamilifu.Tutafika.

Naandika haya bila kujali kama Mtanzania atakayejitokeza ataamua kuwa mwanachama wa chama gani cha siasa. Kwa vyovyote vile, kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu ni chombo halali cha kutusaidia kupata viongozi makini.

Hakuna chama kinachoweza kudai ndicho chenye leseni ya kuliongoza taifa hili.Na wasii kukubali kubadilika na kukubali mabadiliko kama ambavyo mataifa mengine ufanya.

Wamarekani wamekiondoa chama cha Republican ambacho rais wake alikuwa George Bush.Na kwa mara ya kwanza wakampatia rais mwenye asili ya Kiafrika kupitia chama cha Democraty,Barrak Obama.

Hivi karibuni Waingereza wamekirejesha chama cha maafidhina wa kibepari kiitwacho Consecutive na kumpata Waziri Mkuu mpya aitwaye David Cameroon ambaye ni Waziri Mkuu kijana kwa kipindi cha miaka 200 iliyopita nchini Uingereza.

Siasa zilizomeleta rais Obama Ikulu ni siasa zile zililizo mleta David Cameroon madarakani.Wamarekani na Waingereza walichoshwa na uhafidhina wa kibepari usiojali utu na ustawi wa makabwera na walichoshwa na siasa za vita vyenye lengo la kupora mali asili katika mataifa kama vile Iraq na Afganistan.

Wamarekani na Waingereza walijitathimini wenyewe kama taifa na kuona ustawi wao wa kijamii na kiuchumi ukiporomoka wakati mataifa kama Japan,Taiwan,China na Korea yakisonga mbele kwa kasi ya kutisha.Na jibu la tathimini hiyo walilitoa kupitia uchaguzi mkuu wa nchi zao.

Je watanzania tunajifunza nini katika matukio hayo?Je ni mpaka taifa letu lisambaratike kama Somalia ndipo tuamke na kuanza kujua kwamba taifa limeingia mtoni?.

Hatuwezi ‘kujipiga kifua’ kwa kuwa wenyeji wa mkutano wa Kimataifa wa Uchumi Duniani (World Economic Forum) wakati mwananchi wa kawaida anaishi kwa pungufu ya mlo mmoja kwa siku.

Hatuwezi kuendelea kuwa na serikali ya viongozi wabadhirifu,walio jaa hila na husuda,wababaishaji kama inavyodaiwa sasa.Kila siku kwenye kashfa zinazoibuka na zile ambazo tunazishuhudia mahakamani.

Ni vyema tujue kwamba kuna mwisho katika kila jambo.Tunaitaji viongozi wapya ambao ni waadilifu na ambao hawatufanyii usanii wa kupeleka kesi mahakamani pale ambapo wanajua moyoni mwao hakuna ushahidi ili tu wajipatie sifa za uadilifu na uchapakazi .

Tunataka viongozi wa kweli kwenye vita ya ufisadi,wizi tuambiwe ukweli.Hatuko tayari kuona watu wasiyonahatia wakibambikiziwa kesi ili kujenga umaarufu wa kipuuzi kwa watu fulani.

Tunataka mabadiliko na mabadiliko hayo yaanzie kwenye Katiba ya nchi.Mabadiliko hayo yaonekane kwenye sheria za nchi.Na mwisho yaonekane kwenye mfumo wa dola letu. Tuache ubabaishaji .Madai haya yamekuwepo kwenye meza ya serikali toka mwaka 1992.

Baadhi ya wananchi walijiunga katika Kamati ya taifa ya Mabadiliko (National Committee for Constitution Reform-NCCR).Madai yao ya mabadiliko ya Katiba ni ya kweli na ni halali hadi leo.

Hayajafanyiwa kazi na badala yake serikali imebobea katika kupeleka viraka na kuvibandika ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.Sheria za nchi zimeendelea kuwa mbaya na zinazoendekeza uonevu ,zinazowanyang’anya wananchi haki na rasilimali zao.

Na kwa kweli taifa letu haliwezi kuendelea chini ya Katiba, sheria na mfumo mbovu wa dola .Navishangaa vyama vya upinzani havigusii tena suala la mabadiliko ya Katiba, sheria na mfumo wa dola.Vinaenda kwenye uchaguzi mkuu kama wasindikizaji huku vikijua wazi Katiba, sheria na mfumo wa dola haurusu uchaguzi huru na wa haki.

Vyama hivi vya upinzani navyo vimeishia kuwa vyama vya kisanii.Vinaendeleza mchezo ule ule na kuimba wimbo ule ule wa Chama cha Mapinduzi(CCM).

Kwa muktadha huu Watanzania tusitegemee maajabu kwani vyama vya upinzani vimesambaratika au vimesambaratishwa,chonganishwa na CCM na baadhi ya viongozi wa vyama hivyo vya upinzani ambao ni mapandikizi, walafi wa madaraka na fedha hali inayosababisha vyama hivyo kuchukiana na kushindwa kuwa na umoja wa ukweli.

Kila kimoja kinajiona ndiyo chama ,kinadharau chama chenzie badala ya kuungana, kushirikiana kwa nia njema na kuleta mageuzi.Sisi tunajua hata vyama vyote vingejifuta kikabaki chama kimoja mfano CHADEMA,NCCR-Mageuzi au CUF bado kisingeweza kushindana na CCM ambacho ni chama dola.

Tatizo la udhahifu wa vyama hivyo vya upinzani umo katika mfumo wa Katiba ,Sheria na mfumo wa dola.Kama vyama vya upinzani havitaki kutambua hilo , navitakia kila la kheri katika ushiriki mwema wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.Hilo ndiyo Fukuto la Jamii.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Mei 30 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.