Header Ads

SIMBA KUCHAGUANA LEO

.KORTI KUU YABATILISHA AMRI YA KISUTU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana jioni ilibatilisha amri ya muda ya kuzuia uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba unaofanyika leo ambayo ilitolewa Alhamisi wiki hii na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kubaini dosari katika amri hiyo.


Amri hiyo ilitolewa jana saa 1:10 jioni na Jaji Agustine Mwarija baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili zilizokuwa zinavutana katika kesi iliyokuwa imefunguliwa na Michael Wambura dhidi ya mwenyekiti wa klabu ya Simba, Hassan Dalali, kuruhusu uchaguzi huo kuingiliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Jaji Mwarija ametoa uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja za walalamikaji Othuman Hassan ‘Hassanoo’ na Aden Rage ambao ni wagombea wa nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi huo waliokuwa wakitetewa na mawakili wa kujitegemea, Richard Rweyongeza na Peter Swai, dhidi ya Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali, aliyekuwa akitetewa na wakili Majura Magafu na Wambura ambaye hakuwa na wakili.

Baada ya Jaji Mwarija kusikiliza hoja za pande zote kwa zaidi ya saa mbili mfululizo, aliahirisha shtaka hilo kwa muda ili kuandaa uamuzi kabla ya kurejea saa 1 usiku na kutoa uamuzi wake.

Akisoma uamuzi huo ambao ulichukua dakika zisizozidi tano na bila kuchambua, alisema amebaini mwenendo wa kesi iliyofunguliwa Kisutu ambayo ilisababisha hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Aniceth Wambura, kutoa amri ya muda ya kusitishwa kwa uchaguzi huo, ulikuwa batili.

“Nimepitia kwa kina hoja za pande zote mbili, mahakama hii kwanza imekubaliana na ombi la waombaji (Rage na Hassanoo) kutaka mahakama hii itoe amri ya kutengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu.

“Hivyo mahakama hii inatengua amri ya mahakama hiyo ya chini na inaagiza jalada la kesi hiyo lirudishwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na ipangiwe hakimu mwingine,” alisema Jaji Mwarija na kusababisha Wakili Swai na Rweyongeza kukumbatiwa kwa furaha na wafuasi walalamikaji.

Awali, majira ya saa 10 jioni, wakili Rweyongeza akiwasilisha hoja zake, aliomba mahakama itengue uamuzi wa Kisutu kwa sababu wateja wake hawakuwa wamepewa haki ya kusikilizwa na uamuzi huo tayari umeishawaathiri kwa sababu hawawezi kugombea nafasi hiyo ya uenyekiti kwani uchaguzi umesimamishwa wakati wao hawakushtakiwa, isipokuwa mwenyekiti wa Simba ambaye kwa mujibu wa Katiba ya Simba, aliyepaswa kushtakiwa ni Bodi ya Wadhamini ya klabu hiyo.

Kwa upande wake Magafu aliyekuwa akimtetea Dalali alipinga hoja hiyo kwa maelezo kwamba anayepaswa kushtakiwa ni mwenyekiti wa Simba na kwamba katika kesi iliyofunguliwa Kisutu aliyeshtakiwa ni mwenyekiti, waombaji wala hawakuwa wameshtakiwa, hivyo hakimu Wambura asingeweza kuwasikiliza waombaji hao kwa sababu hawakuorodheshwa kwenye hati ya kiapo katika kesi ya msingi.

“Mheshimiwa Jaji Mwarija, naomba siasa isiletwe hapa mahakamani katika kuamua kesi hii, msimamo wangu ni kwamba Hakimu Mkazi wa Kisutu, Wambura, alikuwa sahihi, hajakosea mahali popote na ndiyo maana waombaji katika hati yao ya madai hawajaonyesha hakimu huyo amekosea wapi na ikumbukwe sheria inataka anayelalamikia uamuzi wa mahakama ya chini ni lazima aonyeshe mapungufu yaliyofanywa na hakimu husika, lakini msomi mwenzangu (Rweyongeza) ameshindwa kuainisha mapungufu.....tusilete siasa katika masuala ya kisheria,” alidai Magafu.

Kwa upande wake Wambura ambaye hakuwa na wakili, alidai kuwa yeye anaiomba isitengue uamuzi wa Kisutu kwa sababu haki zake zimevunjwa na uchaguzi huo haukufuata katiba.

Naye wakili Swai alisema anasikia furaha ombi lao kukubaliwa ila hataisahau kesi hiyo kwani tangu aanze kazi ya uwakili hajawahi kukumbana na kesi kama hiyo ambayo imewatesa mno; walitumia muda kidogo mno kujiandaa na kesi hiyo.

Kwa upande wake Hassan Hassanoor aliliambia gazeti hili mahakamani hapo kwamba amefurahishwa na uamuzi wa mahakama hiyo na anawaomba mashabiki wake wafike kwa wingi katika uchaguzi na wampigie kura za ndiyo ili aweze kushinda na kuiongoza klabu hiyo na kuongeza kuwa endapo atapata fursa ya kuchaguliwa kuiongoza Simba atahakikisha analeta maendeleo katika klabu hiyo kongwe hapa nchini.

Juzi, Jaji Mfawidhi Njengafibhili Mwaikugile aliitisha jalada la kesi iliyofunguliwa Mahakama ya Kisutu na kesi iliyokuwa imefunguliwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala na kupokea lalamiko la Rage na Hassanoo kwa ajili ya upekuzi na alimuagiza Naibu Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha, Jumatatu, ayapeleke kwa Jaji Agustine Mwarija ili aweze kupanga tarehe ya kuziita pande zote mbili na kuzisikiliza.

Hata hivyo, juzi usiku uongozi huo wa mahakama ulitoa maelekezo kwa watendaji wake kuandaa hati za kuziita pande zote mahakamani hapo jana saa sita mchana na pande zote zilipata hati za wito wa mahakama na jana saa tatu asubuhi zilifika mahakamani hapo.

Wakati huo huo, uchaguzi wa klabu hiyo unafanyika leo katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oyesterbay jijini Dar es Salaam kwa jumla ya wagombea 16 kushindana katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Akizungumza na waandishi wa habari hata kabla ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Ndumbaro alisema maandalizi yalikuwa yamefikia asilimia 99 na uchaguzi utaanza saa tatu asubuhi.

Wagombea nafasi ya mwenyekiti ni Hassan Othman ‘Hassanoo’ na Ismail Aden Rage huku Geofrey Nyange ‘Kaburu’ akiwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.

Nafasi ya ujembe wa kamati ya utendaji itawaniwa na Joseph Kinesi, Francis Waya, Yassin Mwete, Damian Manembe, Hassan Mnyenye, Said Juma, Maulid Said, Hamis Mkoma, Sued Nkwambi, Boniface Wambura, Suleiman Kigodi, Ibrahim Masoud na Hassan Mtenga.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Mei 9 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.