Header Ads

VIGOGO BoT WAACHIWA,WAKAMATWA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, jana iliwafutia mashtaka ya uhujumu uchumi yaliyokuwa yakiwakabili wakurugenzi wanne wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Licha ya kuwafutia mashtaka, wakurugenzi hao walijikuta wakikamatwa tena baada ya kutuhumiwa mashtaka matatu ya matumizi mabaya ya ofisi za umma.

Washtakiwa hao ni Mkurungezi wa BoT, Simon Jengo, Naibu Mkurugenzi wa Fedha za Nje, Kisima Mkango, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kitengo cha Sheria, Bosco Kimela, na Mkurugenzi wa Huduma za Benki, Ally Bakari, waliondolewa jalada lao baada ya
mahakama kupokea ombi lililowasilishwa na Mkuregenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Agnes Mchome, wakili wa Serikali, Sedekia, alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa ya matumizi mabaya ya ofisi za umma wakiwa waajiriwa BoT.

Wakili Sedekia, alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu, ambapo kosa la kwanza walilifanya 2004, kwa kuchapisha noti zenye thamani ya sh milioni 500.

Wakili Sedekia, alidai shtaka la pili linafanana na la kwanza ambapo wanadaiwa kutumia nyaraka hizo kumdanganya mwajiri wao ili aweze kuongeza gharama za uchapishaji wa noti zenye thamani hiyo mwaka 2005.

Aidha, wakili alidai shtaka la tatu ni la kutumia madaraka yao vibaya, ambapo watuhumiwa hao kwa pamoja wakiwa na nafasi zao, waliongeza gharama za uchapishaji wa noti zenye thamani ya sh bilioni 1.4 mwaka 2007.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Mei 8 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.