LIYUMBA AFUNGWA MIAKA MIWILI JELA
*MAHAKIMU WATOFAUTIANA
*HAKIMU MMOJA AMUONA HANA HATIA
*ATOKWA MACHOZI KIZIMBANI
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana imemuhukumu kwenda jela miaka miwili, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba baada ya kumtia hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi za umma.
Hata hivyo, mahakama hiyo iliandika historia mpya kwa jopo la mahakimu wakazi, lililokuwa likiongozwa na Edson Mkasimongwa aliyekuwa akisaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa, kutoa hukumu mbili zilizotofautiana kimaamuzi.
Kiongozi wa jopo, Mkasimongwa alisema wakati wanaandaa hukumu ya kesi hiyo, walijikuta wanatofautiana kimtazamo. Mlacha na Mwingwa walifikia uamuzi wa kumtia hatiani mshtakiwa, wakati Mkasimongwa alikuwa na mtazamo tofauti wa kumwachia huru.
Alidai baada ya kuupitia ushahidi wa upande wa mashtaka, alibaini unaning’inia na kueleza kuwa hata hukumu itakayotumiwa na mahakama ni ile iliyoandaliwa na mahakimu wenzake wawili na aliyoiandaa yeye itahifadhiwa kwenye kumbukumbu za mahakama.
Baada ya kutoa maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mlacha alianza kusoma hukumu hiyo iliyochukua saa tatu, ambapo alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi wanane na vielelezo 13 vya upande wa mashitaka na ushahidi uliotolewa na mashahidi wawili wa upande wa utetezi, mahakama hiyo imekubalina na upande wa jamhuri kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Alidai kuwa mahakama iliukataa utetezi uliotolewa na mshitakiwa pamoja na shahidi wake ambaye alikuwa Kaimu Katibu wa BoT, Bosco Kimela kwa sababu ushahidi wao umeonekana ni kama hadithi ya kutunga.
“Jopo hili limeona utetezi wa Liyumba na shahidi wake ni kama hadithi ya kutunga baada ya kuuchunguza, hivyo tunaukataa ushahidi wao, tulipata mashaka kuamini ushahidi wa upande wa utetezi, kwanza Liyumba na Bosco walikuwa wakiishi pamoja gereza la Keko na walikuwa wakikabiliwa na makosa yanayofanana, hivyo mahakama inakubaliana na upande wa mashtaka kwani ushahidi wake ulikuwa ni wa moja kwa moja,” alisema Mlacha.
Akichambua hoja ya Liyumba, aliyodai kwamba aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Balali ndiye aliyempa madaraka kwa mdomo ya kusimamia mradi ule, Hakimu Mlacha alisema wameona kuwa taasisi ya BoT ni kubwa na nyeti, hivyo haiwezi kuendeshwa kwa maelekezo ya mdomo.
Kuhusu maelekezo ya barua zilizokuwa zinasainiwa na Liyumba kwenda kwa mkandarasi wa mradi wa majengo pacha, alisema mahakama inaona maelekezo hayo yalikuwa ni kinyume cha sheria kwani bodi ya BoT ndiyo yenye maamuzi ya kuidhinisha chochote kile kifanyike.
Akichambua ushahidi huo, alisema hakuna ubishi kwamba gharama za ongezeko la ujenzi wa mradi ziliongezeka hivyo mabadiliko hayo yalisababisha BoT itumie fedha zaidi, ambazo zingetumika kwa ajili ya shughuli nyingine.
Alisema ushahidi uliotolewa unaonyesha mabadiliko hayo yalikuwa yakifanyika kabla ya kupata idhini ya bodi na kwamba walichobaini bodi hiyo ilikuwa ikiburuzwa na mshtakiwa na marehemu Balali.
Hata hivyo, wakili wa Liyumba, Majura Magafu aliomba mahakama kabla haijafikia uamuzi wa kutoa adhabu izingatie mshitakiwa kuwa ni mgonjwa, na mtu mzima ambaye ana familia inayomtegemea.
“Tulichokibaini katika kesi hii ni kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya BoT ilikuwa ikiburuzwa na mshtakiwa na marehemu Gavana Balali... na kwa mujibu wa ushahidi tumeona Liyumba alikuwa na uhuru sana na alikuwa hafuati sheria... hivyo, kwa kuwa nchi hivi sasa ipo kwenye vita dhidi ya wabadhirifu wa fedha za umma na kosa la matumuzi ambalo limeainishwa kwenye kifungu cha 96(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kifungu hiki hakitaji adhabu sasa mahakama inatumia kifungu 35 cha Sheria ya Adhabu, ambacho kinaipa nguvu mahakama hii kutoa hukumu ama ya fine au kifungo.
“Sasa kwa kuwa Tanzania hivi sasa ipo kwenye vita dhidi ya wabadhirifu wa fedha za umma mahakama hii haitampatia mshitakiwa adhabu ya kulipa faini, hivyo inampatia adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema Mlacha huku Liyumba akitokwa na machozi kizimbani na baadhi ya ndugu na watoto wa mshtakiwa kububujikwa na machozi muda wote.
Nao mawakili wa utetezi, Majura Magafu, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo waliomba mahakama iwapatie nakala ya hukumu hiyo ili waende kukata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Kwa upande wa Mkasimongwa akisoma hukumu yake mbele ya umati mkubwa uliofurika ndani na nje ya mahakama, alisema yeye anamwachiria huru mshtakiwa kwa sababu ushahidi wa upande wa mashitaka unaning’inia.
Akichambua ushahidi huo alisema hakuna ubishi kwamba Liyumba alikuwa mtumishi wa BoT na barua za maelekezo kuhusu mradi ule zilizokuwa zinakwenda kwa mkandarasi alikuwa akiziandika kwa niaba ya BoT na si yeye binafsi.
Mkasimongwa alisema kwa mujibu wa hati ya mashtaka haionyeshi hayo maamuzi makubwa wanayodai Liyumba aliyafanya yeye binafsi, kwani hakuna barua zilizoletwa zikionyesha zimeandikwa na mshtakiwa binafsi kwenda kwa mkandarasi bali zilizoletwa mahakamani ni barua zinazoonyesha BoT ndiye alikuwa akimwandikia mkandarasi na mshitakiwa akawa anatia saini kwa niaba ya taasisi hiyo na kushindwa kwa jamhuri kuleta barua hizo kunaacha mashaka makubwa.
“Meneja yeyote wa BoT uteuliwa na Gavana hivyo alikuwa akifanyakazi kama anavyoelekezwa na Gavana afanye.Kama alivyoeleza na mashahidi wote kwamba mshtakiwa hakuwa na mamlaka ya kufanya mabiliko hayo na kwamba idhini zote zilitolewa na bodi na hata kama idhini zilitolewa na bodi kabla au baada ya mabadiliko hayo kutekelezwa bado idhini hizo zitakuwa idhini halali kwani zilitolewa na bodi.
“Kwahiyo mtu kusema kwamba Liyumba alivunja sheria kwa kusaini zile barua si kweli kwani Liyumba aliteuliwa na Gavana na haingii akilini kwamba alitenda mambo hayo bila maelekezo ya Gavana na Bodi.Huo ndiyo uamuzi wangu shtaka dhidi yake halijathibitshwa na ninaamuru apewe manufaa yote na ninamwachilia huru”alisema Mkasimongwa huku ndugu na jamaa wakiendelea kububujikwa na machozi na mahakama ikiwa kimya.
Hata hivyo, ilipofika saa tisa alasiri, Wakili Magafu akizungumza na gazeti hili alisema tayari ameishawasilisha kwa maandishi hati ya nia ya kukata rufaa kwa uongozi wa mahakama hiyo na kupeleka nakala katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Januari 27, mwaka huu, Liyumba na Meneja Mradi, Deogratius Kweka walifikishwa mahakamani hapo, wakikabiliwa na makosa mawili ya matumuzi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.
Lakini, Mei 27 mwaka jana mahakama hiyo iliifuta hati ya mashitaka baada ya kubaini ina dosari za kisheria na ikawaachia washtakiwa ingawa walikamatwa muda mfupi tu na kesho yake Liyumba peke yake ndiye alifikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa hayo.
Aprili 9, mwaka huu, mahakama hiyo ilimfutia shitaka la pili la kusababisha hasara na kumfanya abaki na shitaka moja la matumizi mabaya.
Na kwa kipindi chote hicho alikuwa akisota katika gereza la Keko kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka atoe fedha taslimu au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani ya sh bilioni 110.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 25 mwaka 2010

1 comment:
dada tunakushukuru kwa mchango wako wa habari za mahakamani unaandika vizuri sana.sisi wa ulaya unatusadia sana.
Post a Comment