Header Ads

KESI YA AMATUS LIYUMBA HATUA KWA HATUA HADI LEO HUKUMU YAKE

Na Happiness Katabazi
KWA mara nyingine tena Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) nchini, chini ya serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete leo (Mei 24 ) itaendelea kuandika historia ya ama kushinda au kushindwa kesi zake za jinai inazozifungua na kuziendesha katika mahakama mbalimbali hapa nchini.


Leo Jopo la Mahakimu Wakazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, linaloongozwa na Edson Mkasimongwa, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa wanatarajia kukaa kwenye viti vitatu vya enzi na kutoa hukumu kesi Na.105/2009 yenye shtaka moja tu la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma kwamba katika kipindi cha mwaka 2001-2004 aliidhinisha mabadiliko ya ongezeko wa mradi wa ujenzi wa minara pacha ‘Twin Tower’bila idhini ya bodi ya wakurugenzi wa BoT,inayomkabili inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba(62), anayetetwa na mawakili wa kujitegemea Jaji Mstaafu Hillary Mkate, Onesmo Kyauke, Majura Magafu na Hudson Ndusyepo.

Kesi hii imekuwa ikivuta hisia za watu wengi wa kada tofauti.Hivyo ungana na mwandishi wa makala hii ambaye ni mwandishi wa habari za mahakamani ambaye aliifuatilia kwa karibu kesi hii tangu ilipofunguliwa hadi leo inatolewa hukumu ili aweze kukupa mtiririko mzima wa kesi hii tangu ilipofunguliwa hadi leo inapomalizika kwa kutolewa hukumu.

Januari 27 mwaka 2009:Liyumba na Meneja mradi wa majengo ya Minara Pacha, Deogratius Kweka walifikishwa kwa mara ya kwanza saa nane mchana mbele ya Hakimu Mkazi Hadija Msongo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, na kusomewa hati ya mashtaka Na.27/2009.Shitaka la kwanza lilikuwa ni matumuzi mabaya ya ofisi ya umma baada ya kufanya upanuzi wa mradi huo bila idhini ya bodi ya Wakurugenzi wa BoT na shtaka la pili ni la kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 221.

Hata hivyo Hakimu Mkazi Msongo siku hiyo alisema ili washtakiwa wapate dhamna ni lazima kila mmoja atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh bilioni 55, kutotoka nje ya jiji bila kibali cha mahakama, kuwasilisha hati ya kusafiria mahakamani.Walishindwa kutimiza masharti hayo siku hiyo.

Februali 17 mwaka 2009: Hakimu Mkazi Msongo alimpatia dhamana iliyozua utata Liyumba peke yake ambaye aliwasilisha hati ya kusafiria iliyoisha muda wake, hati ya nyumba yenye thamani ya Sh milioni 800, kinyume kabisa na masharti aliyoyatoa hakimu huyo huyo Januari 27 mwaka jana.Na Liyumba baada ya kupewa dhamana hiyo alitoka gerezani na kurudi nyumbani kwake huku Kweka akiendelea kusota rumande kwa kushindwa kutumiza masharti ya dhamana.

Februali 20 mwaka 2009: Hakimu Mkazi Msongo , saa nane mchana aliwaita kwa dhalula wadhamini wawili wa Liyumba na kuwaeleza kuwa ameifuta dhamana ya mshitakiwa baada ya kubaini kuna dosari na akatangaza kuufuta uamuzi wake wa kumpatia dhamana Liyumba ambao aliutia Februali 17 mwaka jana.Hata hivyo siku hiyo Liyumba hakuwepo mahakamani kwani siku hiyo haikuwa ni tarehe ya kesi yake.Hali iliyosababisha wananchi na vyombo kueneza uvumi kwamba mshitakiwa huyo ametoroka.

Machi 2 mwaka 2009: Mawakili wa mshitakiwa huyo waliwasilisha kwa maandishi ombi mbele ya Hakimu Mkazi Msongo la kutaka mahakama hiyo itumie kifungu cha 225(1-4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai 2002, kinachotamka kuwa, ndani ya siku 60, upelelezi kesi husika uwe umekamilika, vinginevyo ifutwe

Machi 13 mwaka 2009:Hakimu Mkazi Msongo aliyekuwa anasilikiza kesi hiyo aliamua kujitoa kwa madai kuwa mwenendo wa kesi hiyo umekuwa ukilalamikiwa na waendesha mashtaka na wakili kupitia vyombo vya habari.

Machi 20 mwaka 2009: Uongozi wa Mahakama ya Kisutu, ilimpangia Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema,kusikiliza kesi hiyo ikiwa ni siku chache baada ya hakimu Msongo kujiondoa kwa madai kuwa jamii kupitia vyombo vya habari , imekuwa ikilalamikia dhamana aliyompatia Liyumba..

Machi 30 mwaka 2009:Hakimu Mkazi Lema alianza kuiendesha kesi hiyo.
Aprili 2 mwaka 2009: Hakimu Mkazi Lema amesikiliza ombi lilowasilishwa na wakili wa utetezi Majura Magafu liloiomba mahakama iifute kesi hiyo kwasababu siku 60 zimepita na Jamhuri haijakamilisha upelelezi wa kesi hiyo.

Aprili 23 mwaka 2009: Hakimu Mkazi Lema alitoa uamuzi wa ombi hilo na alisema baada ya kupitia hoja za mawakili wa pande zote mbili, amebaini kuwa licha ya siku 60 kupita na ni kweli upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, haona kama haki za msingi za washtakiwa
zimevunjwa, hivyo akatupilia mbali ombi la mawakili wa utetezi lilotaka kesi hiyo ifutwe.

Mei 27 mwaka 2009:Hakimu Lema aliwafutia kesi washtakiwa wote wawili baada ya kukubaliana na ombi la mawakili wa washtakiwa kwamba hati ya mashtaka ina dosari za kisheria.Lakini wakati Liyumba na mwanzeke wakifurahia uamuzi huo, walikamatwa tena na makachero wa polisi waliofurika mahakamani hapo, muda mfupi baada ya kuachiwa na kupelekwa katika kituo cha polisi Salender.

Mei 28 mwaka 2009:Saa nane mchana Liyumba alikifishwa peke yake mahakamani hapo na kusomewa hati mpya ya mashtaka Na.105/2009 na wakili wa serikali Prosper Mwangamila aliyekuwa anasaidiana na Wakili Kiongozi Justus Mulokozi na John Wabuhanga mbele ya hakimu mkazi Nyigumalila Mwaseba ambapo alidai mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ya matumuzi na mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 221.

Mei 29 mwaka 2009:Hakimu Mwaseba alitoa uamuzi wa kulegeza masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo.Alisema ili apate dhamana atatakiwa atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya Sh milioni 300, wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh milioni 50 kila mmoja,kutotoka nje ya jiji hadi kwa kibali maalum na kusaliminisha hati ya kusafiria mahakamani.

Masharti hayo ni tofauti na awali, ambapo masharti ya dhamana yake yaliangukia chini ya kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambayo yanamtaka mshtakiwa atoe nusu ya fedha au hati ya mali yenye thamani ya Sh bilioni 110.Upande wa Jamhuri haukulizika uamuzi huo wamekata rufaa Mahakama Kuu.

Juni 1 mwaka 2009:Jaji Geofrey Shaidi alisikiliza ombi la kupinga kulegezewa masharti dhamana mshtakiwa huyo liliwasilishwa mbele yake na Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP),Eliezer Feleshi dhidi ya Liyumba, ambapo kwa mujibu wa ombi hilo, DPP anapinga masharti ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama ya Kisutu.

Juni 15 mwaka 2009:Jaji Shaidi alitoa uamuzi kuhusu ombi hilo la DPP na akasema anakubalina na ombi la DPP la kutaka mahakama hiyo itengue masharti ya hakimu Mwaseba na akaamuru kuwa mshtakiwa anapaswa apewe dhamana yatakayoangukia kwenye kifungu cha 148(5)(e) cha sheria ya Makosa ya jinai ya mwaka 2002 ambao Liyumba alitakiwa atoe fedha au hati ya bilioni 110.Na akaamuru jarada la kesi hiyo lirudishwe Kisutu na apangiwe hakimu mwingine.Na Liyumba alishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana hivyo kulazimika kusota jela hadi leo.

Julai 28 mwaka 2009:Uongozi wa mahakama ya Kisutu ulimpanga hakimu mwingine Eva Nkya kuendelea na kesi hiyo huku ikisiburi Jaji Mkuu Agustino Ramadhani aipangie jopo la mahakimu wakazi kwaajili ya kuanza kuisikiliza kesi hiyo.Na wakili kiongozi wa serikali Justus Mulokozi aliambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Agosti 25 mwaka 2009: Hakimu Mkazi Nkya alisema jaji mkuu tayari ameishawapanga jopo la mahakimu wakazi kwaajili ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba jopo hilo litaongozwa na Mkasimongwa atakayesaidiwa na Mlacha na Mwingwa.

Septemba 7 mwaka 2009: Kesi hiyo ilikuja kwaajili ya upande wa jamhuri kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa lakini hata hivyo mshtakiwa siku hiyo hakuweza kufka mahakamani kwani alikuwa akiugua gerezani,hivyo usikilizwaji wa awali uliarishwa.

Septemba 25 mwaka 2009: Wakili wa serikali Mulokozi mbele ya jopo hilo, alimsomea maelezo ya awali mshtakiwa.

Oktoba 1 mwaka 2009: Upande jamhuri ulianika orodha ya mashahidi wake 15 na kwamba inakusudia kuleta vielelezo 13.

Oktoba 19 mwaka 2009: Kesi ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa mfululizo hadi Oktoba 23 ,lakini siku hiyo haikeweza kusikilizwa kwasababu shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka hakuweza kutokea mahakamani kwababu ni mgonjwa hivyo ikaairishwa.

Oktoba 22 mwaka 2009:Shahidi wa kwanza ambaye ni Mchunguzi kutoka(TAKUKURU), Seif Mohamed (50), aliambia mahakama kuwa mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi wa Minara Pacha (Twin Tower), yaliidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa BoT.

Oktoba 23 mwaka 2009: Shahidi wa pili ambaye ni Meneja wa Masuala ya bodi ya Wakurugenzi wa BoT, Justo Tongola (46),alieleza kuwa hajawahi kuona wala kusikia bodi hiyo ikilalamikia utendaji kazi wa Liyumba.

Novemba 18 mwaka 2009:Shahidi wa tatu ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha BoT, ruta Angelo(50),aliambia mahakama kuwa mshtakiwa huyo hakuwa na uamuzi wa mwisho katika mradi wa ujenzi ‘Twin Tower”.

Novemba 24 mwaka 2009: Shahidi wa tano ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mjumbe wa bodi ya BoT, Dk.Natu Mwamba(49), alidai kuwa hana kumbukumbu ya idadi ya maombi na kiasi cha fedha za nyongeza kilichokuwa kikiletwa na menejimenti kwenye bodi ya wakurugenzi ili ipate idhini.

Novemba 26 mwaka 2009: Shahidi wa saba ambaye ni mkadiliaji wa gharama za majengo,Harold Herbert Webb(78),aliambia mahakama kuwa kuwa hapakuwepo na hasara iiyopatikana katika ujenzi wa majengo pacha katika benki kuu.

Webb ambaye ni raia wa Uingereza, alidai hapakuwepo hasara yoyote licha ya kuwapo kwa mabadiliko ya ujenzi na kiasi cha fedha kuongezeka kutoka dola milioni 73 hadi dola 357,568, kiasi chote hicho kilitumika kwenye mradi wa ujenzi huo.

Januari 26 mwaka 2010:Shahidi wa nane ambaye ni Naibu Gavana wa Benki Kuu (BoT), Juma Reli (54), alisema ameshindwa kuithibitishia mahakama hiyo kuhusu hasara iliyopatikana katika mradi huo kwa sababu hadi sasa ripoti ya mwisho ya matumuzi ya fedha za mradi huo haijakamilika.Sambamba na hilo, katika hali isiyotarajiwa, upande wa mashitaka katika kesi hiyo ulisema unakusudia kupunguza idadi ya mashahidi wake kutoka 15.

Machi 15 mwaka 2010:Kesi ilikuja kwaajili mashahidi wa upande wa Jamhuri kuendelea kutoa ushahidi lakini katika hali iliyoshtusha waudhulaji wa kesi hiyo Wakili mwandamizi wa serikali, Juma Mzarau aliambia mahakama kuwa baada ya wao kupitia kwa kina nakala ya mwenendo wa kesi hiyo ulionyesha ni mashahidi wanane waliotoa ushahidi na vielelezo 13 vilitolewa mahakamani hapo na wamefikia hatua muafaka ya kuifunga kesi yao kwa mujibu wa kifungu cha 231 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

Ombi hilo la kuifunga kesi yao lilikubaliwa na mahakama na Kiongozi wa jopo Edson Mkasimongwa akatoa amri kwa upande wa utetezi yake kwa njia ya maandishi mahakamani Machi 22 , upande wa Jamhuri nao uwasilishe majumuisho yake mahakamani Machi 29 na Aprili 9 mwaka huu, mahakama hiyo itatoa uamuzi wa mshtakiwa huyo ana kesi ya kujibu au la.

Machi 22 mwaka huu: Mawakili wa Liyumba wawasilisha majumuisho yao kwa maandishi na wameiomba mhakama imuone mteja wao hana kesi ya kujibu na imuachirie huru kwasababu upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi yao.

Machi 29 mwaka huu: Mawakili wa upande wa jamhuri uliwasilisha majumuisho saa 9:21 alasiri na uliomba mahakama imuone mshtakiwa ana kesi ya kujibu kwasababu wameweza kuithibitisha kesi yao.

Aprili 9 mwaka huu:Kiongozi wa jopo Edson Mkasimongwa kwaniaba ya wenzake alitoa uamuzi wa majumuisho hayo na alimfutia shtaka la pili ambalo ni la kusababisha hasara na mahakama ikamuona Liyumba ana kesi ya kujibu katika shtaka la kwanza ambalo ni la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma.

Aprili 16 mwaka huu:Mawakili wa Liyumba waliwasilisha mahakamani majina ya mashahidi watano wanaokusudia kuja kumtetea mshtakiwa.

Aprili 22 mwaka huu: Amatus Liyumba alitoa utetezi wake na akadai kuwa serikali haijui itendalo dhidi ya kesi iliyomfungulia.Na akaiomba mahakama izingatie ukweli wakati wa kutoa hukumu dhidi yake Mei 24 (leo)badala ya kuwasikiliza watu wasiojua watendalo.

Maneno hayo mawili ‘hawajui watendalo’ yanafanana na yale aliyotumia Yesu Kristo, anayeaminika kuwa ni Mwokozi wa waumini wa Kikristo wakati akieleza kitendo cha Wayahudi waliokuwa wakimsulubisha (Luka 23:34).

Alipomaliza kujitetea alipanda kizimbani shahidi wake ambaye alikuwa Kaimu Katibu wa BoT na Katibu wa Bodi ya benki hiyo ambaye ni mwanasheria kitaaluma, Bosco Kimela (52), aliieleza mahakama kuwa shitaka linalomkabili Liyumba hastahili kushtakiwa nalo kwani hajalitenda.Na wakili Magafu akasema kutokana na ushahidi wa mashahidi hao wawili , upande wa utetezi unafunga kesi hayo.

Hivyo hakimu Mkazi Mkasimongwa akaamuru pande zote mbili Mei 7 mwaka huu, zilete kwa njia ya maandishi majumuisho yao ya kuiomba mahakama imuone mshtakiwa ana hati au la.Lakini hata hivyo tarehe hiyo ilipofika na kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kutajwa wakili wa serikali Ponsian Lukosi alimweleza hakimu mkazi Mkasimongwa kwamba Jamhuri imeshindwa kuwasilisha majumuisho yake kwasababu mahakama haijawapatia mwenendo wa kesi hiyo na hakimu huyo alikubaliana na ombi hilo na kuziongezea pande zote mbili muda ambapo aliziamuru ifikapo Mei 13 mwaka huu, ziwasilishe majumusho hayo.

Mei 13 mwaka huu: Wakili wa utetezi Onesmo Kyauke aliwasilisha majumuisho yao upande wa utetezi ambapo waliomba mahakama imuone mshtakiwa hna hatia kwasababu hakuwa na mamlaka ya kuamua jambo lolote lile katika mradi wa majengo pacha.

Hata hivyo waandishi wa habari za mahakama kwa jitihada walizozifanya kwa siku mbili mfululizo za kuakikisha wanapata nakala ya majumuisho ya upande wa jamhuri, hazikuzaa matunda baada ya kukosa ushirikiano kutoka kwa mawakili hao wa upande wa mashtaka ambao wakati kesi hiyo inafunguliwa , inaendelea mahakamani walikuwa wakiwaatia ushirikiano waandishi wa habari za mahakama.

Mei 24 mwaka huu:Ambayo ni leo ndiyo mahakama ya kisutu inaitimisha jukumu lake la kisheria la litakalobaki kuwa historia kwa watanzania la kutoa hukumu ya kesi hiyo ambayo ilidumu mahakamani hapo kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi minne sasa.

0716 774494
Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu,Mei 24 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.