Header Ads

BOSI WA RICHMOND AIBWAGA SERIKALI


*SERIKALI YADHAMIRIA KUKATA RUFAA KUPINGA
Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es salaam, imemwachiria huru mfanyabiashara Naeem Adam Gire aliyekuwa akikabiliwa na makosa ya kughushi, kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kuhusu kampuni ya Richmond LLC ya Texas ya Marekani kwasababu ushahidi ulitolewa na upande wa Jamhuri ni dhahifu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Waliarwande Lema ambaye alisema kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya mahakama hiyo kutoa uamuzi wa ama mshtakiwa huyo Gire aliyekuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea Alex Mgongolwa na Richard Rweyongeza ambapo Jamhuri ilikuwa ikiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Fredrick Manyanda na Shadrack Kimaro ana kesi ya kujibu au la.

Lema alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wote tisa na vilelelezo vilivyotolewa na upande wa Jamhuri, amebaini ushahidi na vielelezo hivyo ni dhahifu na una mapungufu ambao umeacha mashaka na maswali mengi na hivyo mahakama yake imefikia uamuzi wa kutumia kifungu cha 330 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambacho kinaipa mamlaka mahakama ya kumwona mshtakiwa hana kesi ya kujibu na kumwachiria huru.

“Hii kesi ambayo leo(jana) naitolea uamuzi ni wazi kabisa imejaa mapungufu mengi ya kisheria tena yapo wazi kabisa na simung’unyi maneno nasema wazi kabisa hii kesi ni miongoni mwa baadhi ya kesi za jinai zinazofunguliwa na Jamhuri ambazo mwisho wa siku mahakama inajikuta ikitupiwa lawama…na sheria za nchi zipo wazi zinaipa mamlaka mahakama kumuona mshtakiwa hana kesi ya kujibu pindi itakapobaini ushahidi ulioletwa na Jamhuri dhidi yake ni dhahidi na usio na mashiko”alisema Hakimu Lema.

Hakimu Lema alisoma uamuzi huo(ruling) uliokuwa ukisubiliwa kwa hamu na wananchi wengi kwa mtindo wa kuyaweka mashtaka yaliyokuwa yakimkabili mshtakiwa.Alisema Gile alikuwa akikabiliwa na makosa ya kugushi, kutoa hati ya uwakilishi iliyogushiwa(Power of Attorney), kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali ambao ni wajumbe wa Bodi ya Tenda ya Shirika la Umeme la Tanesco na Timu ya Tathimini.

Kwamba Januari 13 mwaka 2009 mahakamani hapo Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Stanslaus Boniface, alidai kuwa Machi 13 mwaka 2006 jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu , mshtakiwa huyo aligushi hati ya uwakilishi(Power of Attorney) ya Machi 13 mwaka 2006 iliyokuwa imeguhishiwa na kuonyesha Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas ya Marekani, Mohamed Gile ambaye ni kaka wa mshtakiwa anaishi Marekani alikuwa amemuidhinisha mshtakiwa kuiwakilisha hapa Tanzania.

Hakimu Lema alisema kuwa kwa mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, Jamhuri inadai kuwa Machi 20 mwaka 2006 katika eneo la Umeme Park Bara bara ya Morogoro jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu mshtakiwa huyo alitoa hati hiyo ya uwakilishi kwa maofisa hao wa serikali iliyokuwa ikionyesha imesainiwa na Mohamed Gile kuonyesha kuwa Mohamed amemteua mshtakiwa kuiwakilisha kampuni hiyo hapa nchini kinyume na kifungu cha 333, 335(e)(3),337,342 na 122(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Akitoa uamuzi wake kwa kuanza kulichambua kosa la kugushi ambalo ni kinyume cha kifungu cha 333 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, Hakimu Lema hati iliyogushiwa ni lazima iwe na udanganyifu ndani yake na katika kesi hiyo hati inayodaiwa kugushiwa na upande wa jamhuri ni Power of Attorney.

“Hivyo basi katika kutatua mgogoro huo wa hati hiyo ya uwakilishi , Jamhuri ilileta mashahidi watatu kwaajili ya kuutatua mgogoro huo miongoni mwa mashahidi hao ni mawakili wawili ambao ndiyo waliyoiandaa hati hiyo na shahidi sita ambaye ni mtaalamu wa maandishi toka Jeshi la Polisi, Hamis Hamad.

“Licha ya kuletwa kwa mashahidi hao watatu kwaajili ya kuutatua mgogoro huo, mahakama hii imebaini hakuna ushahidi walioutoa unaonyesha hati hiyo ya uwakilishi ilighushiwa, pia hakuna ushahidi uliotolewa unaonyesha mshtakiwa huyo kweli alighushi hati hiyo kwakuwa hata huyo shahidi wa sita ambaye ni mtaalamu wa maandishi toka Polisi, Hamad, hakuweza kutoa mapungufu yaliyokuwepo kwenye ile hati ya uwakilishi ambayo Jamhuri inadaiwa hati hiyo inasaini ambayo imegushiwa.

“Na mtaalamu huyo wa maandishi aliangalia saini zilizokuwa kwenye hati hiyo na hakuna sehemu shahidi huyo aliyoangalia saini ya mshtakiwa na ile saini iliyokuwa kwenye hati ile na mahakama hii inasema katika uchunguzi wake shahidi huyo wa sita (Hamad) alitakiwa achukue saini ya mshtakiwa ailinganishe na saini iliyosainiwa kwenye ile hati ya uwakilishi na kwakuwa shahidi huyo ameshindwa kufanyakazi yake yake hiyo ya kikamilifu, mahakama hii inasema jamhuri imeshindwa kuthibitisha kosa hilo kwasababu mtaalamu wa maandishi ameshindwa kuyaainisha mapungufu yaliyopo kwenye hati hiyo halisi na hati iliyogushiwa ”alisema Hakimu Lema.

Kuhusu shtaka la pili na tano ambalo ni la kuwasilisha hati iliyogushiwa kwa maofisa wa serikali, hakimu Lema alisema kwa kuwa kosa la kwanza la kughushi hati hiyo ya wakilishi Jamhuri imeshindwa kulithibitisha, ni wazi kabisa hati hiyo ya uwakilishi iliyowasilishwa kwa maofisa wa Tanesco haikuwa imegushiwa kwasababu Jamhuri imeshindwa kuleta mashahidi ambao wangeweza kuonyesha hati halisi ya uwakilishi ni na hati iliyogushiwa ni hipo hivyo basi katika kosa la pili na tano, jamhuri imeshindwa kuyathibitisha.

Aidha Hakimu Lema ambaye alikuwaa akiusoma uamuzi wake huo huku akionyesha umakini, akitolea uamuzi kuhusu kosa la tatu na la nne, ambayo ni kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kuwa kampuni ya Richmond inauwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100 huku akijua si kweli, alisema kwakuwa mashahidi wa tatu wa jamhuri walifika mahakamani hapo na kuieleza mahakama kuwa jumla ya makampuni nane yaliomba kupatiwa tenda ya kuzalisha umeme hapa nchini.

Lakini mashahidi hao wakaieleza mahakama kuwa katika kikao cha kwanza cha ufunguzi wa tenda hiyo kilichofanyika Machi 2 mwaka 2006, makampuni yote yalifanyiwa usaili na bodi na timu hiyo ikabaini hakuna kampuni hata moja iliyokidhi vigezo na ikaamuru usahili ufanyike upya kwa mara ya pili na hata ulipofanyika bado makampuni yote yalishindwa kukizi vigezo ndipo shahidi wa tatu Injinia wa Tanesco, Simon Jilima mwaka 2006 akateuliwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo Dk.Ibrahim Msabaha aende kusimamia ufungwaji wa mitambo ya Richmond.

“Kwa ujumla mahakama hii inasema jamhuri imeleta ushahidi dhahifu ambao umeshindwa kuishawishi mahakama imuone mshtakiwa ana kesi ya kujibu hakuna kabisa ushahidi unaonyesha nyaraka za kampuni ya Richmond zilizowasilishwa kwa Bodi ya Tanesco ziliwasilishwa na mshtakiwa ila kwa mujibu wa shahidi wa nne aliambia mahakama nyaraka hizo ziliwasilishwa kwenye bodi hiyo na mwenyekiti wa Richmond, Mohamed na siku hiyo Mohamed aliwatambulisha wajumbe wa bodi kuwa mshtakiwa ni mdogo yake na kwamba ndiye amempa jukumu la kuiwakilisha kampuni yake hiyo hapa Tanzania.

“Na kwakuwa Jamhuri ilidai mshtakiwa alighushi saini Mohamed Gile katika ile hati ya uwakilishi, Jamhuri ilipaswa imlete Mohamed hapa mahakama aje atoe ushahidi kwamba hakumpa mshtakiwa mamlaka ya kuiwakilisha kampuni yake hapa nchini kwasababu hilo Jamhuri imeshindwa kutekeleza jukumu lake ili mwisho wa siku mahakama ilaumiwe, mahakama hii inamwachiria huru mshtakiwa na inamfutia kesi hiyo”alisema Lema.

Baada ya kutoa uamuzi huo wakili wa serikali Shadrack Kimaro alisema Jamhuri haijaridhishwa na uamuzi huo hivyo inaomba ipatiwe mwenendo wa kesi hiyo ili iende Mahakama Kuu kukata rufaa.

Kwa upande wake Naeem Gire aliwaeleza waandishi wa habari nje ya viwanja vya mahakama, hiyo alisema amefurahishwa na uamuzi huo na kwamba mahakama imetenda haki.
Gile amefikishwa mahakamani Januari 13 mwaka 2009 ikiwa ni mwaka mmoja upite tangu aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mwenzake aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, mapema Februali mwaka 2008 viongozi hao walipolazimika kujiuzulu nyadhifa zao kwa kashfa hiyo ya Kampuni hiyo ya kufua umeme ya Richmond.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Julai 29 mwaka 2011.

1 comment:

Anonymous said...

00 Kids 12 & undеr Free All peгsons under 18.
Keep it simρle stuріd! Hiring of a destructive force dangerous to relationshiρѕ, hеalth care proѵiders to help peοple there іѕ
no waiting pеrіod is almost cartoonish in
character, attorneу feeѕ. The fouгth eхception tο this prіvilege is cancеleԁ by
a fеdeгal inνestigation intо fedеral bank frаuԁ
could comе bу the attorney fοr more than once, oг other ѕufficіent evіdence to substantiate
the caѕe. Οn Thursday, March
14, 2012.

Here is my page - http://sobr.anie.mk/notice/32001
My web page Look At This

Powered by Blogger.