Header Ads

MAHAKAMA:MARANDA,FARIJALA WANAKESI YA KUJIBU

Na Happiness Katabazi
KWA mara nyingine tena Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemuomwona Kada wa CCM, Rajabu Maranda na mpwa wake Farijala Hussein kuwa wanakesi ya kujibu katika kesi ya pili inayowakili ya wizi wa Sh bilioni 2.2 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania.


Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo la Mahakimu wakazi watatu wanaoongozwa na jaji Fatma Masengi anayesaidiwa na mahakimu wakazi Projestus Kahyoza na Katarina Revocate ambao walisema kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya jopo hilo kutoa uamuzi wake utakaowaona washtakiwa hao wanakesi ya kujibu au la.

Hakimu Mkazi Recovate ndiye aliyesoma uamuzi huo kwaniaba ya jopo hilo ambapo alisema jopo hilo baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa jamhuri na vielelezo, majuisho ya upande wa utetezi na majumuisho ya kesi hiyo yaliyowasilishwa na wakili wa serikali Arafa Msafiri, jopo hilo kwa kauli moja limefikia uamuzi wa kuwaona washtakiwa wote wanakesi ya kujibu.

Revocate ambaye alisoma uamuzi huo kwa kifupi kwa kutumia takribani dakika tano, na bila kuweka wazi vigezo vilivyotumiwa na jopo hilo kufikia uamuzi huo, alisema jopo hilo limetosheka na kuridhika na hoja zilizotolewa na upande wa jamhuri kwani ndiyo zimeweza kuilishawishi jopo hilo lifikie uamuzi wa kuwaona washtakiwa wote wanakesi ya kujibu.

“Jopo hili kwa kauli moja linasema limeridhishwa na ushahidi wa upande wa jamhuri kwani ushahidi huo umefanya mahakama hii uweze kukukubali kuwa jamhuri imeweza kuthibitisha kesi yao hivyo mahakama hii imewaona washtakiwa wote wanakesi kesi ya kujibu hivyo hawana budi kupanda kizimbani kuanza kujitetea”alisema Hakimu Revocate.

Kwa upande wake wakili wa washtakiwa hao, Majura Magafu alieleza mahakama wanakubaliana na uamuzi huo wa mahakama na kwamba wateja wake watajitetea kwa njia ya kiapo na kwamba wanakusudia kuleta jumla ya mashahidi sita.Mashahidi sita hao miongoni mwao ni washtakiwa wenyewe.

Aidha Hakimu Revocate alisema washtakiwa hao wataanza kujitetea katika kesi hiyo mfululizo kuanzia Novemba 7,8,9 na 10 mwaka huu na kuamuru washtakiwa hao warejeshwe gerezani kwasababu wanaendelea kutimikia adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela, baada ya Mei 23 mwaka huu, mahakama hiyo kuwatia hatiani katika kesi ya kujipatia ingizo la sh bilioni 1.6 isivyohalali kutoka katika akaunti ya EPA.

Novemba 4 mwaka 2008, Jamhuri ilidai mahakamani hapo kuwa Maranda na Farijala wanadaiwa kuiibia BoT , Sh 2,266,049,041.25 baada ya kudanganya kuwa kampuni yao ya Money Planners & Consultant imepewa idhini ya kudai deni BoT na kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani huku wakijua si kweli. Kwa sasa jumla ya kesi tatu zinawakabili washtakiwa hao ndiyo bado hazijatolewa hukumu wakati kesi moja tu ndiyo ilikwishatolewa hukumu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 26 mwaka 2010.

No comments:

Powered by Blogger.