RAIS KIKWETE TANGAZA VITA DHIDI YA UGONJWA HUU
Na Happiness Katabazi
JUMATATU ya wiki hii mimi na mwandishi mwenzangu wa habari za mahakamani Regina Kumba(Habari Leo), tulikwenda Wodi ya watoto wenye maradhi ya vichwa vikubwa vilivyojaa maji kitaalamu unajulikana kama Hydrocethalus katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwaajili ya kumjulia hali mwanataaluma mwenzetu(jina naliifadhi) ambaye mtoto wake mchanga amelazwa katika wodi hiyo akisumbuliwa na maradhi hayo.
Tulipofika hapo tulimkuta mwanataaluma mwenzetu akiwa na mama yake mzazi na mtoto wake ambaye tayari ameishafanyiwa upasuaji wakiendelea kumuuguza kichanga hicho. Tuliwajulia hali na kuwafariji na kwakweli walishukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo wanajitahidi kadri ya uwezo wao kutoa matibabu mazuri kwa watoto waliolazwa wodi hapo kwaajili ya matibabu.Nifarijika sana na kauli hiyo.
Pia nilishuhudia nje ya wodi hiyo ndugu na jamaa hasa wanawake wakiwa wamekaa chini ya miti na watoto wao wenye maradhi yao wakipunga upepo na kubadilishana mawazo na ndugu na jamaa zao waliofika hapo kwaajili ya kuwajulia hali.
Pia kwa macho yangu niliwashuhudia watoto zaidi ya saba ambao wanasumbuliwa na maradhi hayo wakiwa wamepakatwa na wazazi wao na watoto wengine wakiwa wamekarishwa kwenye baiskeli za walemavu wakipunga upepo na kunywa vinywaji baridi.
Niwe muwazi baada ya kuishuhudia hali hiyo kwa macho, nilijisikia uchungu, mwili ulisisimka, nikakosa raha na nikajiuliza swali moja moyoni , hivi wale watoto wamekosa nini kwa mungu?Lakini nikaishia kwakumaliza kwa kujibu mwenyewe kimoyo moyo kuwa yote hayo yanayowapata watoto hao ni mipango ya mungu.
Tatizo hilo lilinilazimu kuwasiliana na baadhi ya madaktari kuwauliza chanzo hasa cha tatizo hilo ni nini lakini ili kama wazazi wakiwa wajawazito au watoto waliozaliwa wakiwa wazima lakini baada ya muda wakaja kupata tatizo hilo, wachukua hatua gani za taadhari ili waweze kujiepusha na janga hilo, kwa kweli madaktari hao wanne walishindwa kunipatia jibu.
Hivyo basi kutokana na kushuhudia hali hiyo nikiwa kama mama, mwanahabari nimelazimika kuandika mtazamo huu kuiamasisha serikali, sekta binafsi na sisi waandishi wa habari na wanajamii wengine kila mmoja kwa nafasi yake kuona wakati umefika sasa kwa taifa letu kuanza vita ya kuutokomeza ugonjwa huo ambao unawasumbua watoto wengi wasiyokuwa na hatia.
Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii walifanikiwa kusaka fedha za miradi waliyoibuni ya kutokomeza ugonjwa wa ukimwi na wakaupa kauli mbiu isemayo ‘Tanzania bila ukimwi inawezekana’, mradi wa kutokomeza maralia ambapo kaya nyingi zilipewa vyandarua kwaajili ya kuzuia mbu wasiwaambukie maralia, mradi wa afya ya uzazi salama kati ya mama na mtoto na miradi mingine mingi tu ambayo ilipata mwitikio mkubwa na jamii.
Tena kupitia mradi wa kampeni ya afya ya uzazi salama kutoka kwa mama na mtoto imesababisha taasisi mbili za nchini Marekani wiki iliyopita kumtunukia tuzo mbili kwa mpigo rais Jakaya Kikwete tuzo kwa kazi nzuri ya kusimamia kampeni hiyo.
Na situ serikali imekuwa ikiendesha kampeni kama hizo za kutokomeza magonjwa kadhaa, pia taasisi nyingine za kiraia nazo zimekuwa zikipambanua kuyapiga vita baadhi ya maradhi kama Saratani ya matiti kwa wakina mama na kweli kampeni hizo zimekuwa zikifanikiwa kwasababu ya wasamalia wema kujitokeza kuchangia fedha katika miradi hiyo na hatimaye waathirika wa maradhi hao wanafuatwa walipo na kupatiwa tiba.Napongeza katika hili.
Lakini kuhusu ugonjwa huo wa watoto kujaa vichwa maji,kimsingi tukubaliane kuwa jamii yetu ya Tanzania, bado hatutaki kutambua ugonjwa huu kadri siku zinavyozidi kwenda idadi ya watoto wanaopata tatizo hilo wanaongeza, na si viongozi wa kitaifa, dini, kijamii wala sisi vyombo vya habari hatujajitokeza adharani kupaza sauti au kutoa misaada ya kuwezeshwa kupanuliwa kwa wodi au kujengwa hospitali maalum kwaajili ya watoto wenye matatizo hayo au Taifa kuamua kufanya kampeni ya ama ya kuutokomeza au kuuzuia ugonjwa huu usiwapate watoto wetu.
Ndiyo maana nasema ushawishi ule ule uliotumiwa na serikali ya Kikwete kuomba fedha kwa wafadhili au kuchukua fedha kwenye bajeti ya serikali na fedha hizo wakaziingiza kwenye kampeni zile na kwa kiasi Fulani zikafanikiwa, basi tunataka kuona sasa ushawishi huo huo wa kiongozi wetu wanchi pamoja na serikali yake wakiutumia kwaajili kuamasisha jamii kuukataa ugonjwa huo kwamba kwa kila mzazi anapona mtoto wake anaanza kunyemelewa na maradhi hayo ya kujaa maji amkimbize haraka hospitali, pia madaktari waliobobea katika ugonjwa huo wawezeshwe ili waweze kupewa fursa ya kutoa elimu kwa umma kuhusu ugonjwa huo kupitia vyombo vya habari.
Nimemuomba rais Kikwete na serikali yake atumie ushawishi wake wa kuanza mikakati ya kuupiga vita ugonjwa huo kwasababu naamimi akifika katika ile wodi ya wototo wanaosumbuliwa na maradhi hayo na akafanikiwa kuwaona watoto wale naamini kabla ya kuondoka madarakani mwaka 2015, atatumia fursa alizonazo kuakikisha nguvu za kitaalamu, madawa, ujenzi wa wodi katika za watoto wenye maradhi kama hayo katika hospitali zenye hadhi ya mikoa hapa nchini zitajengwa.
Kama serikali yetu imeweza kuelekeza nguvu zake na kuomba misaada kwenye taasisi za kimataifa kwaajili ya waathirika wa ukimwi na ikafanikiwa kupata misaada ya ujenzi wa wodi maalum za wagonjwa hao na matabibu wakapelekwa kuudhulia kozi mbalimbali kwaajili ya kuwahudumia wagonjwa wa ukimwi, basi ni wazi serikali yetu ikiamua kulivalia njuga ugonjwa huo wa watoto wenye vichwa vikubwa vinavyojaa maji ambao mtaani wanauita ‘mabichwa maji’haishindwi.
Ili nisianze kuamini kwamba katika miradi ile ya maralia, ukimwi, Kifua Kikuu, Saratani ambazo bado mnaendeleza kampeni zake kuwa mnafaidika binafsi, naomba uzalendo na shauku ile iliyowasukuma kuanzisha miradi hiyo, sasa muielekeze kwakuanza kusaka fedha kwaajili ya kuanzisha kampeni ya kuupunguza au kuutokomeza ugonjwa huo wa Hydrocethalus.
Napenda kuitimia moyo serikali yetu sasa ione haja ya kuanzisha kampeni ya kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo ili kama unaepukika watu wauepuke, kuutokomeza ugonjwa huo ambao ni wazi kabisa kwanjia moja au nyingine nao unachangia umaskini ndani ya familia ya watu ambao wanamtoto anayesumbuliwa na tatizo hilo.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716 -774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba mosi mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment