Header Ads

MAHALU AFICHUA BEI UNUNUZI JENGO LA UBALOZI ,ROME ITALIA


Na Happiness Katabazi
ALIYEKUWA balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa ripoti ya bei ya ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania mjini Roma aliyokuwa ameipendekeza yeye ilikuwa ni ya bei ya chini ukilinganisha na ripoti ya ununuzi wa jengo hilo iliyokuwa imependekezwa na serikali kupitia Wizara ya Ujenzi.


Profesa Mahalu alitoa maelezo hayo jana mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Elvin Mugeta wakati mshtakiwa huyo anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wa zaidi ya Euro milioni mbili akiongozwa na Wakili wake Mabere Marando, Alex Mgongolwa, Beatus Malima na Cuthebert Tenga kutoa utetezi wake.

Profesa Mahalu alidai kuwa mujibu wa kielelezo cha saba kilichotolewa na shahidi wa Jamhuri ambaye ni Mchunguzi toka TAKUKURU, hakijakamilika alidai kuwa kielelezo kile ni barua ya Februalia 2 mwaka 2002 ambayo akiwa Balozi aliandika yeye kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa na nakala ya barua hiyo ilikwenda kwa Waziri wa wizara hiyo Jakaya Kikwete ambaye ni rais wa nchi kwa sasa, Waziri wa Fedha, Basil Mramba, Katibu Mkuu Kiongozi, Kamishna wa Bajeti Wizara hiyo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo akiwaarifu viongozi hao wa serikali kuhusu shughuli za ununuzi wa jengo la ofisi za Ubalozi mjini Roma,Italia hatua aliyofikia sasa ni ya kulipia jengo lenyewe ili liweze kuwa letu na hatimaye kuhamia na kwamba malipo ya jengo hilo kwa ujumla ni dola za Kimarekani 2,788,862.24 au Euro 3,098,741.38 sawa na Shilingi 2,534,770,448.80.

“Ni kweli barua hiyo iliyotolewa na shahidi huyo wa Jamhuri ilikishwapokelewa na mahakama hii kama kielelezo cha saba kweli kielelezo hicho ni barua ambayo niliandika mimi kwenda kwa mkuu wangu wa kazi lakini barua nilikuwa nimeambatanisha na viambatanisho kumi na moja vikiwemo ripoti tatu za uthamini wa majengo ambapo ripoti A ni ropiti iliyoandaliwa na Kaimu Mkurugenzi-Idara ya Majengo wa Wizara ya Ujenzi M.T.Kimweri, Ripoti B, ilikuwa ni ripoti ambayo ambayo nilikuwa nimeiandika kama balozi ambapo nilipendekeza jengo hilo linunuliwe kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 2.7 sawa na Sh bilioni 2.5 ambayo mwisho wa siku ndiyo ilikuja kutumiwa na serikali kununulia jengo jipya la Ubalozi na ripoti C, ilikuwa ni ya mwenye jengo F.Morelli, viambatanisho hivyo havimo kwenye barua hiyo”alidai Profesa Mahalu.

Alieleza kwa mujibu wa safari ya Roma nchini Italia ya Julai 15-26 mwaka 2001 iliyoandaliwa na Kimweri toka Wizara ya Ujenzi baada ya kuyachunguza majengo matatu la Via Colli della, Via Continad ‘ Appezo 185-Rome ambapo kila jengo lilikuwa likiuzwa kwa dola za kimarekani milioni tatu wakati jengo la Via San Marno 25 Rome ambalo lilikuwa likiuzwa kwa dola za Kimarekani milioni 2.25 ambapo katika ripoti yake baada ya uchunguzi huo , Kimweli alitoa mapendekezo yake akiitaka serikali ikubali kununua jengo la Via Continad’ Apezzo 185-Roma kama itashindikana kulinunua hilo jengo la Via Colli della 128-Roma kwa kuwa majengo hayo yapo maeneo mazuri.

Hata hivyo kwa mujibu wa barua hiyo ya Mahalu kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, yeye alipendekeza jengo hilo la Via Continad Appezzo 185 –Rome ninunuliwe kwa bei ya chini ya jumla ya dola za kimarekani 2,788,862.24 sawa na Shilingi 2,534,770,448.80 ambazo serikali ilizilipa kwa awamu kwa mmiliki wa jengo hilo F.Morelli.

“Kwa kuwa mimi ndiyo mwandishi wa barua hiyo ,ndiyo ninayefahamu wakati naituma barua kwa viongozi wangu wa serikali nilikuwa nimeambatanisha na viambatanisho vyote hivyo ambapo nashangaa shahidi ametoa barua hii pekee yake bila viambatanisho hivyo na kushindwa kwake kuleta viambatanisho hivyo hapa mahakamani ambapo mimi ninazo nakala ya hivyo viambatanisho na ninaiomba nivitoe hivyo viambatanisho kama vilelezo mahakamani”alidai Profesa Mahalu.

Hata hivyo baada ya Mahalu kuomba viambatanisho hivyo mahakama hiyo ivipokee kama vielelezo , Wakili Mwandamizi wa Serikali Lukosi ,ghafla aliomba mahakama iarishe kesi hiyo hadi leo ili waweze kupata nafasi ya kulinganisha viambatanisho vivuli hali iliyosababisha hakimu Mgeta kumhoji wakili huyo wa serikali kuwa anaenda kulinganisha viambatanisho hivyo na nyaraka zipi kwasababu hapo awali Jamhuri ilishasema haina nyaraka halisi za nyaraka hizo anazozitumia Mahalu katika utetezi wake kwasababu serikali siyo mwandishi wa barua hiyo hali iliyosababisha wakili huyo kujibu kuwa wanaomba muda ili waweze kwenda kuzipitia nyaraka hizo na siyo kwenda kuzilinganisha(cross check).

Hakimu Mgeta alikubali ombi hilo la kuarishwa kwa kesi hiyo akaiarisha kesi hiyo hadi leo saa tatu asubuhi.

Chanzo; Chanzo Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 19 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.