Header Ads

SERIKALI YAJICHANGANYA KESI YA MAHALU

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi wa zaidi ya euro milioni mbili, inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Prof. Dk. Costa Mahalu na Grace Martin, jana umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuwa imepata nyaraka halisi za mawasiliano yaliyokuwa yakifanywa kati ya mshitakiwa huyo na serikali licha ya awali ulidai kutokuwa na nyaraka hizo.


Kesi hiyo ambayo jana ilikuwa imekuja kwaajili ya kuendelea kusikilizwa huku Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ponsia Lukosi, akitarajiwa kuieleza mahakama amebaini nini kwenye zile nyaraka 11 zilizotolewa juzi na Prof. Mahalu ambaye aliomba zipokewe kama vielelezo, adala yake wakili huyo aliomba mahakama kabla ya kuvipokea, kesi hiyo iahishwe hadi jana ili upande wa Jamhuri uweze kupata nafasi ya kuzipitia nyaraka hizo.

Mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Elvin Mugeta , wakili Ponsian jana alishindwa kueleza amebaini nini baada ya kuvipitia vielelezo hivyo na matokeo yake akaomba kesi hiyo ihairishwe.

Sababu ya kuomba kuahrishwa kwa kesi hiyo ni kwamba, juzi wakati kesi hiyo inaendelea, aliletewa bahasha kubwa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo ndani yake kulikuwa na nyaraka kadhaa zikiwemo zile ambazo Prof. Mahalu alizitoa juzi mahakamani hapo kama vielelezo.

Kwamba vile vile ndani ya bahasha hiyo kulikuwa na barua iliyokuwa ikimjulisha kuwa serikali imeshapata nyaraka za mawasiliano yaliyokuwa yakifanywa kati ya Mahalu na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kuhusu ununuzi wa jengo la ualozi mjini Rome,Italia.

“Baada ya kupata ujumbe huo toka wizara ya Mambo ya Nje, nilifanya jitihada za kwenda wizarani hapo na kuendelea kukusanya nyaraka nyingine kwa jili ya kuja kuzilinganisha na nyaraka vivuli ambazo zinatolewa na Mahalu mahakamani kama vielelezo na kwa kuwa bado tunaendelea kukusanya nyaraka hizo na kesi hii imepangwa leo na kesho kwaajili ya mshtakiwa kuendelea kujitetea tunaona si busara kesi hii ikaendelea kusikilizwa,” alisema.

Wakili Lukosi aliongeza kuwa kwa sababu upande wa Jamhuri unaendelea kukusanya nyaraka hizo ambazo zimepatikana, wanaomba kesi iahrishwe kwa siku chache ili waweze kuzikusanya nyaraka zote.

Baada ya wakili Ponsian kutoa ombi hilo, wakili wa utetezi, Beatus Malima,alieleza mahakama kuwa hana pingamizi na ombi hilo.

Naye Hakimu Mugeta, alisema kwa kuwa hakuna uhakika hadi kufikia jana upande wa Jamhuri utakuwa umeishamaliza kukusanya nyaraka hizo na vile vile ilikuwa imepangwa kusikilizwa mfululizo kuanzia juzi, ana na leo, kwa sababu hiyo anaiahisha hadi Novemba 15,16,17 na 18 mwaka huu, kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa mfululizo.

Mapema mwaka huu, mawakili wa Mahalu na Martin;Mabere Marando, Alex Mgongolwa na Beatus Malima waliuandikia barua upande wa Jamhuri kuomba uwapatie nyaraka halisi ambazo wateja wao walikuwa wakikusudia kuzitumia kwa ajili ya kujitetea, lakini wakili wa serikali Lukosi kwa kujiamini mbele ya Hakimu Mugeta aliwajibu kuwa serikali haina nyaraka hizo na haiwezi kuwapatia.

Hatua hiyo ilimfanya Prof. Mahalu kupanda kizimbani kujitetea kwa kukutumia nyaraka vivuli na mahakama kulazimika kuzipokea kama vielelezo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Oktoba 20 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.