Header Ads

WATUHUMIWA WA MAUAJI WAACHIWA HURU

Na Happiness Katabazi

MWEKEZAJI wa Hoteli ya South Beach ya Kigamboni, Salim Nathoo ‘Chipata’ (53), na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kijana Lila Hussein (25), wameachiwa huru kufuatia Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Eliezer Feleshi kuwasilisha hati ya kuiondoa kesi hiyo mahakamani.


Nathoo aliyeshtakiwa pamoja na Meneja wake Bhushan Mathkar na John Mkwanjiombi (32) waliachiwa wiki hii na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Kassim Mkwawa.

Mwendesha mashtaka katika kesi hiyo, Dunstun Kombe, aliliambia Tanzania Daima kwamba amri ya kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao ilitolewa Oktoba 10 na DPP kwa kutumia kifungu 91 (1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2002, inayompa madaraka ya kuondoa kesi mahakamani ikiwa ataona ushahidi wa kesi husika hautoshelezi bila kuhojiwa na mtu wala taasisi yoyote.

Ndugu wachachamaa, wataka maelezo

Hata hivyo, kuachiwa kwa mwekezaji huyo kumezua utata mkubwa kwa baadhi ya ndugu wa marehemu na wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliokuwa wakifuatilia kwa makini kesi hiyo tangu kutokea kwa mkasa huo, usiku wa April 9, mwaka huu.

Akizungumza kwa niaba ya ndugu wa marehemu, Abdullah Saiwaad, alisema wamesikitishwa na hatua ya serikali ya kuwaachia huru watuhumiwa wa mauaji ya ndugu yao, bila kujali madhara makubwa yaliyopatikana.

Alisema kitendo cha kuachiwa kwa mwekezaji huyo tena kwa muda mfupi tu tangu kukamatwa na kufikishwa mahakamani, bila kujali athari waliyopata ndugu wa marehemu, kimewafanya waamini kwamba mwenye pesa yuko juu ya sheria.

“Ndugu yetu ameuawa kinyama kwa kuchomwa moto kama kuku, alafu leo hii watu hawa wanaachiwa huru katika mazingira yenye utata namna hii..inasikitisha sana,” alisema Saiwaad.

Aliiomba serikali kurudia upya uchunguzi huo na kufungua mashtaka mapya dhidi ya watuhumiwa hao na kwa kuzingatia zaidi ushahidi wa marehemu alioutoa kabla hajafariki.

Mkasa mzima wa kifo

Lila anadaiwa kukumbwa na mkasa huo Aprili 11 mwaka huu majira ya kati ya saa 5:00 na 6:00 usiku akidaiwa kuingia katika ukumbi wa muziki hotelini hapo bila kulipa kiingilio.

Inadaiwa kwamba marehemu alikamatwa na kupigwa vibaya na askari wanaolinda usalama kwa amri ya meneja na mwekezaji huyo, kabla ya kufikia uamuzi wa kumvua nguo na kummwagia mafuta ya petroli na kumchoma moto.

Habari zinaongeza kuwa wafanyakazi wawili walioshuhudia ukatili huo, walilazimika kupeleka taarifa za tukio hilo kwa ndugu zake, kijiji cha Mjimwema waliofika na kumkimbiza hospitalini.

Lila aliyelazwa wodi namba 7 katika Hospitali ya Temeke akiwa hajitambui akiwa amejeruhiwa vibaya kuanzia magotini hadi shingoni, alifariki dunia Aprili 17 mwaka huu, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Watuhumiwa hao walikamatwa na kufunguliwa kesi ya kujeruhi ambayo iliunguruma katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, kabla ya kubadilishiwa mashtaka na kuwa ya mauaji kufuatia kifo cha kijana huyo.

Sababu za kuondolewa kwa kesi

Nayo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, imetoa ufafanuzi wa kina wa kile kilichosababisha kufutwa kwa kesi hiyo.

Akizungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalum, Mkurugenzi Msaidizi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Stanslaus Boniface, ofisi hiyo iliifuta kesi hiyo baada ya kubaini upungufu mkubwa ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa ushahidi kwa washtakiwa.

Bonifasi aliongeza kuwa ofisi yake ilifikia uamuzi wa kulikagua jalada hilo, baada ya kupokea malalamiko mengi toka ndugu wa washtakiwa waliodai kubambikiziwa kesi ya mauaji.

Katika barua ya maamuzi kwenda kwa mwanasheria wa Kanda ya Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi huyo alisema ushahidi uliokuwa ukitarajiwa kuijenga kesi hiyo ulikuwa ni wa aina mbili: ushahidi wa kwanza ni tamko linalodaiwa kutolewa na marehemu kabla hajakata roho na ushahidi wa mazingira.

Barua hiyo (nakala tunayo) inasema ushahidi uliomo katika jalada la kesi hiyo ulikuwa na mapungufu mawili. “Kama ni kweli marehemu aliwaeleza maneno hayo hao mashahidi wawili Aprili 10 mwaka huu saa 6:30 usiku, kwa nini mashahidi hao hawakutoa maelezo hayo polisi siku ya kwanza kabisa walivyokuwa wakichukuliwa maelezo yao na polisi Aprili 10 mwaka huu saa 5:30?

“Kitendo cha miezi miwili kupita bila ya polisi kuarifiwa na mashahidi hao kile walichoelezwa na marehemu, pia kimesababisha ushahidi uliopo kwenye jalada hilo kuwa na mapungufu makubwa na sababu hiyo ya kwanza pia ndiyo imenisukuma kuifuta kesi hiyo kwani ofisi ya DPP haiwezi kuendelea kuwashtaki watu pindi inapobaini ushahidi uliopo ndani ya jalada hautoshelezi kuendelea kuwashtaki,” alisema Boniface.

Boniface alichambua ushahidi ambao ni tamko lililotolewa na marehemu kabla ya kifo na ulidhibitishwa na Salum Ally, Saidi Kau Sahan, marehemu mwenyewe na G.5975 PC Saidi.

Salum Ally na Said Kau Sahani ndiyo walikuwa watu wa kwanza kukutana na marehemu katika hoteli ya Sunrise baada ya kuchomwa moto.

Na katika maelezo ya nyongeza waliyoyatoa polisi Juni 7, 2011, Salum Ally kwa mara ya kwanza walisema:

“Niliambiwa naye (marehemu) wakati tulipokutana naye kuwa amechomwa moto huko South Beach.”

Sababu ya pili, hata kama wataamua kuhisi kuwa ni hicho ndicho marehemu alichowaeleza mashahidi hao, ni wazi maelezo hayo hayasababishi mshtakiwa yeyote kushtakiwa kwa kesi ya mauji kwa kuwa maelezo ya mashahidi hao yanatofautiana na ushahidi wa Saidi Kau Sahani ambaye ana uhusiano katika kesi hiyo.

Katika ushahidi wake, Sahani alisema, “Kuhusiana na mtu aliyemchoma moto mimi sifahamu ila nilisikia toka kwa Lila (marehemu) kuwa ni Mkurugenzi wa Hoteli aitwaye Chipata na Wahindi wa hapo Hoteli ya South Beach.”

Wakati Salum Ally, Sahani katika maelezo yao walienda mbali na kulitaja jina la mshtakiwa wa kwanza “Chipata” kuwa ni miongoni mwa watu waliomchoma moto marehemu, maelezo hayo yalileta mkanganyiko na sheria katika hali hiyo inasema kama kuna mashahidi wawili wanatoa ushahidi wa kusikia mtu akiwaelezea migogoro miwili tofauti kuwa hicho ndicho alichoelezwa na mtu huyo, basi ushahidi utakaotolewa na mashahidi wa aina hiyo hautakubaliwa na utakuwa hauna thamani.

“Kwa hiyo maoni yetu kutokana na ushahidi tuliouchambua kwenye jalada la kesi hii umesababisha ofisi ya DPP kuamini kuwa marehemu hakuwaeleza mashahidi hao yaani Ally na Sahani jambo lolote lilompata yeye na hivyo tunakubaliana na na ushahidi wa shahidi Fatuma Hussein ambaye ni dada wa marehemu ambaye alitoa maelezo yafuatayo polisi:
“Nilijaribu kumuuliza huyo mtu aliyemleta (yaani Saidi Kau Hassan) ilikuwaje naye akanijibu naye hajui lolote kwani naye alifuatwa na kijana aitwaye MBAVU (Salum Ally,) wakati huo huyo marehemu hakuweza kuniambia lolote zaidi ya kupiga kelele akiomba maji.”

Wakili Boniface alisema kabla ya marehemu kufariki alichukuliwa maelezo na G.5975 Pc Saidi ambapo marehemu katika tamko lake alisema alikwenda kucheza muziki South Beach Resort na kwamba mmiliki wa hoteli hiyo alimwita mwizi na akampiga kwa kutumia fimbo na kisha akamvalisha tairi na kumchoma moto.

Marehemu anadai kwamba ili kuiokoa ngozi yake alikimbia katika Bahari ya Hindi na katika tamko lake hilo alihitimisha kwa kusema hamfahamu ni nani aliyempeleka nyumbani kwao.

“Ofisi ilijiuliza kama kweli marehemu aliacha tamko ambalo linaungwa mkono na ushahidi wa PC Saidi ambaye ndiye aliyemchukua maelezo Lila kabla hajafa Aprili 10 mwaka huu saa 7:15 mchana kwa mtindo wa maswali na majibu ….. na PC Saidi wakati akimchukua maelezo Lila hospitalini alisema ‘…nilijaribu kumhoji kama anaweza kunieleza mkasa mzima uliompata alitoa maelezo yake kwa taabu sana…”

Wakili Boniface alisema pia baadhi ya mashahidi waliendelea kusema, “Ukweli maneno yake hayo aliyatoa kwa taabu sana huku akipoteza kumbukumbu sahihi ya alichokuwa anakieleza.”

“Sasa kwa mazingira yanayotatanisha namna hiyo ofisi ya DPP inaamini kulikuwa na uchelewaji wa kuchukuliwa tamko la marehemu hivyo kufanya tamko hilo kutokuwa na thamani kwa sababu halionyeshi ukweli wowote katika umakini hivyo kufanya tamko hilo kuonekana siyo la kweli …hivyo katika kesi hii hilo tamko la marehemu halina maana yoyote na tunakihesabu ni kipande kidogo sana cha ushahidi ambacho hakiifikishi mahali popote upande wa Jamhuri na hata ushahidi wa nyongeza haupo ndani ya jalada hilo na hivyo kufanya kesi hiyo kubakiwa na ushahidi wa mazingira tu ambao nao pia ni dhahifu,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Aidha, alisema Ofisi ya Mwanasheria wa Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa maoni yake kuwa kuna haja ya kuendelea kwa kesi hiyo mahakamani kwa sababu mbili ambapo sababu ya kwanza ushahidi uliopo kwenye jalada hilo unatosheleza na sababu ya pili , kesi hiyo ilikuwa na maslahi kwa umma.

‘Ni kweli ofisi ya DPP inakubaliana na ofisi ya mwanasheria wa kanda , lakini ieleweke kwamba hicho mnachokiita maslahi ya umma peke yake bila ya kuwepo kwa ushahidi wa kutosha katika kesi hiyo kamwe haiwezi kuchukuliwa kuwa ni kigezo ambacho kitailazimisha ofisi ya DPP isiondoe kesi hiyo mahakamani,” alisema Wakili Boniface.

Hata hivyo, kufutwa kwa mashtaka hayo, hakuzuii kufunguliwa upya kwa kesi hiyo, iwapo utapatikana ushahidi mwingine makini unaoweza kuishawishi Jamhuri kufungua upya shauri hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Oktoba 21 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.