Header Ads

KESI YA JEETU PATEL DHIDI YA MENGI YATUPWA



Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeifuta kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na mfanyabiashara Jayantkumar Chandubai ‘Jeetu Patel’ na wenzake watatu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) kwa maelezo kuwa kesi hiyo haina mantiki ya kisheria na Kikatiba.


Uamuzi huo wa kesi hiyo Na. 30/2009 ulitolewa jana asubuhi na jopo la majaji watatu Jaji Kiongozi wa Fakihi Jundu, Semistocles Kaijage na Profesa Ibrahim Juma ambao walisema licha wanaifuta kesi hiyo kwa sababu haina mantiki ya kisheria, pia walisema madai ya Patel kuhusu tamko la Mengi alilolitoa Aprili 23 mwaka 2009 kwa vyombo vya habari kuwa yaliingilia uhuru wa Mahakama Mkazi Kisutu na kuidharau mahakama hiyo kwa kuwa hukumu walalamikaji ambao wanakabiliwa na kesi nne za EPA kupitia vyombo vya habari kuwa ni ‘Mafisadi Papa’ yalipaswa yapelekwe katika mahakama hiyo ya chini kwani mahakama za chini zimepewa nguvu za kuwaadhibu wale wote wanaotenda makosa ya kuidharau mahakama na endapo uamuzi wa mahakama hiyo ya chini asingelidhika nao ndiyo Jeetu Patel angekatia rufaa uamuzi huo wa mahakama ya Kisutu katika Mahakama Kuu.

Mdaiwa wa kwanza(AG) na wa tatu walikuwa wanatetewa na Wakili Kiongozi wa Serikali Stanslaus Boniface na mdaiwa wa pili(Mengi) alikuwa anatetewa na Michael Ngaro.
Jaji Jundu alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, jopo hilo lilijiuliza kwa mujibu wa Sheria ya Utekelezaji ya mwaka 2002 (Basic Rights and Eforcement Act,Cap 3; 2002) inayo mamlaka ya kutengua Ibara ya 59(B) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kuzifuta kesi nne za jinai zinazowakabili washtakiwa katika Mahakama ya Kisutu ambazo zimefunguliwa na DPP kwa kutumia Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kwasababu kesi iliyokuwa mbele yao ni kesi ya Kikatiba.

“Jibu tulilolipata baada ya kujiuliza swali hilo ni kwamba jopo hilo lilikuwa halina mamlaka ya kutengua ibara hiyo ya 59(B) ya Katiba ambayo inataja majukumu ya DPP na haiwezi kuzifuta kesi hizo zilizopo mahakama ya Kisutu na hivyo imekubaliana na hoja ya wakili wa Mengi(Ngaro) kuwa Mengi ni mtu binafsi na hivyo hana mamlaka ya Kikatiba wa kisheria wa kuimwelekeza DPP wala mahakama kuzifuta kesi hizo zinazowakabili walalamikaji katika kesi hiyo ya Kikatiba.

“Hivyo jopo hili linakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kuwa Mengi ni mtu binafsi hakupaswa kuunganishwa kwenye kesi hiyo kwasababu Mengi siyo taasisi na hana nguvu za kisheria wala Katiba za kuingilia kazi za DPP wala mahakama”alisema Jaji Jundu.

Jaji Jundu alisema madai ya Jeetu Patel dhidi ya Mengi hayakupaswa kuangukia kwenye kesi hiyo ya Kikatiba bali walalamikaji kama waliona Mengi amewakosea walitakiwa kumshtaki kwa kutumia sheria ya Madai au ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 kuwa alitoa matamshi ya kuwakashfu au kuidhara mahakama kwa kutoa maneno yanayowahukumu kabla ya mahakama ya Kisutu kutolea hukumu kesi nne za EPA zinazowakabili.

Awali katika mapingamizi ya awali yaliyotolewa na mawakili wa utetezi Michael Ngaro na Stanslaus Boniface, wakili Boniface aliomba mahakama hiyo iifute kesi hiyo kwasababu viapo vilivyoapwa na walalamikaji wakati wanafungua kesi hiyo ni batili na havina hadhi ya kisheria. Huku wakili Ngaro aliomba jina la Mengi liondolewe kwenye hati ya madai au likibaki basi kesi ifutwe kwasababu Mengi hakupaswa kushtakiwa binafsi.

Aidha pingamizi la pili, mawakili hao walidai kesi hiyo ilikuwa ni kesi ya Kikatiba kwa hiyo mahakama hiyo ya Kikatiba haitakuwa na mamlaka ya kupokea,kujadili wa kutolea maamuzi mgogoro wowote unaoangukia kwenye Sheria ya madai wala jiani badala yake itabakia kuwa na mamlaka ya kujadili, kusikiliza na kutolea maamuzi mgogoro wa Kikatiba peke yake.

Aidha katika madai ya msingi ya Jeetu Patel alidai Mengi amemvunjia haki yake ya Kikatiba ya ambayo Katiba inakata mtu asichukuliwe na hatia hadi pale mahakama itakapomtia hatiani na kwamba AG na DPP wameshindwa kumchukulia hatua za kisheria Mengi kwa kitendo chake cha kuingilia uhuru wa mahakama bila kumshtaki.

Novemba 2008,Jeetu Patel na wadaiwa wenzake Davendra Vinodbhai Patel,Amit Nandy na Ketan Chohan walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi nne za wizi katika akaunti ya Madeni ya Nje(EPA). Kesi hizo ni kesi Na. 1153,1154,1155 na 1157 za mwaka 2008.

Julai mwaka 2009 mawakili wa Patel, Martin Matunda aliwasilisha maombi katika Mahakama ya Kisutu ya kuomba kesi zote hizo nne zisimame kusikilizwa kwasababu washtakiwa hao walifungua kesi hiyo ya Kikatiba iliyotolewa uamuzi jana itakapotolewa uamuzi. Na kwa kipindi chote hicho kesi hizo zote zilikuwa zimesimama kusikilizwa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 26 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.