KESI YA SIMU YA LIYUMBA YAKWAMA
Na Happiness Katabazi
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na simu ya mkononi gerezani inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu(BoT), Amatus Liyumba(63) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ulishindwa kutimiza ahadi yake kumsomea maelezo ya awali(PH) mshtakiwa huyo kwa madai kuwa wamegundua mapungufu kwenye ushahidi uliopo kwenye jalada la kesi hiyo.
Hayo yalielezwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga na wakili wa serikali Ladslaus Komanya na Cecilia Mkonongo ambapo walianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya upande wa Jamhuri kumsomea mshtakiwa huyo maelezo ya awali lakini kutokana na sababu hiyo wakashindwa kuandaa maelezo ya kesi hiyo kwasababu wamegundua mapungufu kwenye ushahidi uliokuwa umekusanywa na polisi kwenye jalada la kesi hiyo.
“Kwa sababu hiyo, tunaiomba mahakama hii iiarishe kesi na tunaomba tupewe wiki mbili kuanzia leo tutakuwa tumerekebisha mapungufu hayo baada ya wiki mbili tutakuwa tayari tumeishakamilisha …kwahiyo leo tumeshindwa kumsomea maelezo ya awali Liyumba kwa sababu ya mapungufu hayo ambayo yamesababisha tushindwe kuandaa maelezo ya kesi ambayo tungekuwa tumeyaandaa ndiyo tungemsomea leo”alisema wakili Komanya.
Baada ya kumaliza kutoa sababu hiyo wakili huyo wa serikali, wakili wa utetezi Majura Magafu anayesaidiwa na Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke alidai kimsingi sababu zilizotolewa na wakili huyo wa Jamhuri hazina mantiki kwani Septemba 8 mwaka huu,siku ambayo ndiyo kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda alimsomea mashtaka mshtakiwa na kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na akaomba apangiwe tarehe ya jana kwaajili ya kuja kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo hivyo hiyo sababu ya eti wamegundua ushahidi uliokusanywa kwenye jalada la kesi una mapungufu,walipaswa waiseme sababu hiyo siku ile waliyojigamba kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
“Mheshimiwa hakimu kama utakumbuka hata siku ya kwanza kesi hii ilipofunguliwa ni sisi upande wa utetezi ndiyo tuliusaidia upande wa Jamhuri kuwaonyesha kuwa hati yao ina mapungufu ya kisheria hadi wewe hakimu siku hiyo hiyo ukatoa amri ya kuutaka upande wa Jamhuri uende ukaifanyie marekebisho hati yao mashitaka na wakaenda kuifanyia marekebisho na saa chache walivyorudi wakadai upelelezi umekamilika .
“Sasa sisi upande wa utetezi tunaona hizo wiki mbili walizoomba ni ndogo, tunaomba mahakama iwapatie muda wa mwezi mmoja ili kama wanaenda kumpikia kesi mpya Liyumba waende kuipika kabisa ila tunaomba Jamhuri ifahamu kuwa tayari sisi upande wa Jamhuri tumeishawasilisha kwa maandishi mahakamani hapa taarifa ya kuwasilisha pingamizi la awali na upande wa Jamhuri tumeishawapatia nakala ya pingamizi hilo na tunaiomba mahakama hii siku kesi hii itakapokuja kwaajili ya usikilizwaji wa awali basi siku hiyo hiyo ndiyo pingamizi letu nalo lisikilizwe” alidai wakili Magafu kwa sauti ya juu.
Wakili Ndusyepo alieleza pingamizi hilo la awali waliloliwasilisha kwa uongozi wa mahakama hiyo, ni wanadai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba sababu zote watazitoe siku hiyo ya pingamizi litakapokuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa.
Hakimu Mkazi Sanga alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili amekubaliana nazo na kwamba anaiarisha kesi hiyo hadi Septemba 28 mwaka huu, ambapo siku hiyo upande wa Jamhuri itakuja kwaajili ya kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo na pingamizi hilo la upande wa utetezi litasikilizwa na mahakama hiyo.
Septemba 23 mwaka huu, Liyumba alitoka gerezani la Ukonga jijini Dar es Salaam, alikokuwa akiishi baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake ya kifungo cha miaka miwili gerezani.
Septemba 8 mwaka huu, kwa mara nyingine tena Liyumba alifikishwa mbele ya hakimu Sanga akikabiliwa na kosa la kukutwa na kitu kilichokatazwa gerezani chini ya kifungu cha 86 (1,2) cha Sheria ya Magereza kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Wakili Kaganda alidai kuwa Liyumba ambaye wakati huo alikuwa ni mfungwa mwenye Na.303/2010, Julai mwaka huu, ndani ya gereza la Ukonga, alikutwa na simu ya Nokia Na.1280 nyeusi iliyokuwa na laini yenye Na. 0653-004662 na IMEI Na. 356273/04/276170/3 ambayo alikuwa aikiitumia kufanyia mawasiliano binafsi wakati ni kinyume cha sheria. Hata hivyo alipata dhamana baada ya kujidhamini kwa bondi ya Sh 50,000.
Desemba mwaka 2010 , Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Emilian Mushi alitupilia mbali rufaa iliyokatwa na Liyumba iliyokuwa ikiiipinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu iliyomuhukumu kwenda jela miaka miwili baada ya kumtia hatiani kwa kosa moja la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo jaji huyo alisema akubaliana na hukumu ya Kisutu kwani ilikuwa sahihi kisheria.
Mei 23 mwaka 2010, Mahakimu wawili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa walitoa hukumu ya kumtia hatiani Liyumba kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma, na hakimu mkazi mmoja Edson Mkasimongwa ambaye ndiye aliyekuwa akiliongoza jopo hilo kusikiliza kesi hiyo alitofautiana na mahakimu hao wawili na akatoa hukumu ya peke yake ambayo ilimwachiria huru mshtakiwa huyo.
Lakini hata hivyo hukumu iliyotolewa na mahakimu hao wawili ndiyo ilibaki kuwa ni hukumu ya mahakama ya Kisutu na hukumu ya Hakimu Mkasimongwa ikabaki kwenye kumbukumbu za mahakama na haikutumika kwaajili ya kumpatia adhabu Liyumba.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 30 mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment