Header Ads

JERRY MURRO HANA HATIA-WAKILI

Na Happiness Katabazi

WAKILI wa aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Jerry Murro anayekabiliwa na kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya sh milioni 10, Richard Rweyongeza ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,imwachilie huru mshtakiwa huyo kwasababu hana hatia katika kesi hiyo inayomkabili.


Wakili Rweyongeza aliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo kwa njia ya maandishi nakala yake (gazeti hili inayo) kufuatia amri iliyotolewa na Hakimu Mkazi Frank Moshi aliyoitoa Oktoba mwaka huu ambapo alizitaka pande zote mbili kuwasilisha majumuisho yao kuwaona washtakiwa wana hatia au la kwa njia ya maandishi ambapo upande wa Jamhuri utawasilisha majumuisho yao kesho.

Wakili Rweyongeza alidai kuwa alisikilizwa kwa makini ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri lakini hajasikia kitu chochote kinacho muunganisha Murro na washtakiwa wengine wasiojulikana kula njama kutenda kosa hilo kama shtaka la kwanza kwanza linavyodai kuwa Murro na washtakiwa wenzake ambao ni Deo Mugassa na Edmund Kapama na watu wengine wasiyofahamika walitenda kusa la kushawishi ili wapewe rushwa Sh milioni 10 toka kwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage Karoli , Januari 20 mwaka 2010 ili asiwe kurusha tuhuma zake za ubadhilifu wa fedha za umma katika kipindi cha Usiku wa Habari kinachorushwa na Televisheni ya TBC1.

“Shtaka la kwanza katika hati ya mashtaka, linasomeka kuwa kosa lilitendeka Januari 28 mwaka 2010.Lakini ushahidi ulitolewa na Jamhuri ulionyesha kosa lilitendekea Januari 29 mwaka 2010…na hadi mapema Oktoba mwaka huu washtakiwa walimaliza kujitetea na hivyo kesi upande wa utetezi ikawa imefungwa , hati ya mashtaka ilikuwa ikisomeka Murro alitenda kosa hilo Januari 28 mwaka 2010 ndipo upande wa Jamhuri siku hiyo kabla ya utetezi kufunga kesi yao ukaamua kubadilisha hati ya mashtaka na mahakama ilikubali hati hiyo kubadilishwa kutokana na utofauti uliopo kati ushahidi na maelezo yaliyokuwa yameandikwa kwenye hati ya mashtaka.

“Kwa hali hiyo naona upande Jamhuri hauna maelezo ya uhakika yanayoonyesha mteja wangu alitenda makosa hayo na badala yake ikaamua kuleta ushahidi wa kuungaunga na matokeo yake ndiyo maana Murro aliyakana mashtaka yote yanayomkabili mahakamani hapa”alidai Rweyongeza.

Alidai kuwa kesi ya Jamhuri imesimama na kutegemea ushahidi wa shahidi wa tatu (Michael Wage) jambo linawapotosha kwa sisi upande wa utetezi tunamuona Wage siyo shahidi wa kuaminika na wanaoimba mahakama iupuuze ushahidi wake.

Wakili Rweyongeza alidai kuwa katika ushahidi mashahidi wa Jamhuri walidai kuwa shahidi wa tatu(Wage) kwakuanzia aliwapatia washtakiwa wote rushwa ya Sh 9,000,000 katika sehemu ya rushwa ya Sh milioni 10 aliyokuwa ameombwa na washtakiwa, na wakili huyo akadai kuwa kama hivyo ndivyo ni kwanini polisi wasingesubiri Murro apokee rushwa hiyo ndiyo wakamkamate na kuongeza ni kwanini polisi ilifanya haraka kumkamata Murro wakati bado hajapokea rushwa hiyo ya Sh milioni?

“Tunaomba mahakama hii imwachilie huru Murro kwasababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yao bila kuacha mashaka yoyote hivyo namalizia kwa kuiomba mahakama hii imuone Murro hana hatia”alidai Rweyengeza.

Februali 15 mwaka 2010, ilidaiwa mahakamani na upande wa Jamhuri kuwa washtakiwa wote walitenda makosa ya kula njama, kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa Wage na kujipachika kuwa wao ni wa Maofisa ya TAKUKURU.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 22 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.