Header Ads

MDEE AKWAA KISIKI KORTINI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi lilowekwa na Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA),Halima Mdee lililokuwa likitaka hati ya madai katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu mwaka 2010 iliyofunguliwa na aliyekuwa Mgombea Ubunge kwa tiketi ya (NCCR-Mageuzi), James Mbatia ifanyiwe marekebisho kwa maelezo kuwa haina msingi wa kisheria.


Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji John Utamwa ambaye baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alifikia uamuzi wa kukubaliana na hoja za wakili wa mlalamikaji, Mohamedi Tibanyendela aliyetaka pingamizi hilo litupwe na mahakama.

Jaji Utamwa alisema kwa mujibu wa hati ya madai, mlalamikaji ameeleza malalamiko yake yote kwa mapana dhidi ya mdaiwa na maelezo hayo yanajitosheleza kumfanya mdaiwa kujibu tuhuma hizo zilizoelekezwa kwake.

“Hivyo mahakama hii haikubaliani na pingamizi la mdaiwa anayetetewa na Wakili Edson Mbogoro anayetaka hati ya madai ifanyiwe marekebisho kwa vile hawezi kujibu baadhi ya tuhuma alizotuhumiwa nazo kwasababu zinamkera, kumtia kichefuchefu…..kwa hiyo mahakama hii leo inasema tuhuma hizo hazikeri wala kutia kichefuchefu hivyo ina muamuru mdaiwa kuzijibu na inatupilia mbali pingamizi la mdaiwa”alisema Jaji Utamwa.

Jaji Utamwa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba Mosi mwaka huu, ambapo kesi hiyo itakuja kwa ajili ya kutajwa na kuangalia muda wa jinsi ya kuendelea nayo kwani Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010 inataka kesi za uchaguzi zimalizike ndani ya mwaka mmoja tangu zilipofunguliwa. Kesi hiyo ilifunguliwa Novemba mwaka 2010.

Uamuzi huo unatokana na pingamizi lilowasilishwa na wakili wa Mdee, Mbogoro la kuiomba mahakama hiyo imwamuru mlalamikaji aifanyie marekebisho hati yake ya madai na kuyaondoa baadhi ya madai ambayo Novemba 25 mwaka 2010 Mbatia alifungua kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo ambayo yalimtangaza Halima Mdee(CHADEMA) kuwa mshindi.

Mbatia anadai kuwa katika mikutano ya kampeni, Mdee alimwita yeye kuwa ni fataki anayefanya mapenzi na watoto wa shule, kibaraka wa CCM na kila wiki analipwa sh milioni 80 na chama hicho, hivyo kuwataka wapiga kura wa jimbo la Kawe wasimchague Mbatia.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 29 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.