Header Ads

SITA WAACHIWA KESI YA MAUJI NMB TEMEKE

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewaachiria huru washtakiwa sita kati ya 15 waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya watu wawili katika Benki ya Makabwera (NMB) Tawi la Temeke Dar es Salaam.


Hatua hiyo inakuja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi kuwasilisha ombi la kuiomba mahakama hiyo iwafutie kesi washtakiwa hao kwasababu amebaini hana ushahidi unamshawishi kuendelea kuwashtaki washtakiwa hao kwasababu amebaini hana ushahidi wa kuendelea kuwashtaki.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji Na. 22/2011 inayosikilizwa na Jaji Dk.Fauz Twaibu ni Richard Muhanza “Leonard’, Mwanzo Bunga, Alimeshi Bibuka, Yusufu Mlete, Japo Salum, Issack Abdul ‘Swai’,Said Hamisi ‘Katikati’, Antony Solya ‘Matonya’, Richard Tawete ‘Anwari’, Shafii Abdala, Boniface Makai.

Wengine ni Fabian Mchome ‘Fabi’, Selemani Nzowa, Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), MT.55935 Mathew Mwangunga na Deogratius Massawe ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Amour Khamis.

Washtakiwa waliochiliwa huru ni mshtakiwa wa (2) Bunga, (3)Bibuka (10)Abdalah (12)Mchome(13)Nzowa na mshtakiwa wa (15)Massawe.

Jaji Twaibu alisema amefikia uamuzi wa kuwachilia huru washtakiwa hao kufuatia ombi lilowasilishwa mbele yake jana mchana na Mkurugenzi Msaidizi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Stanslaus Boniface ambaye aliwasilisha ombi la kuwataka washtakiwa hao sita kati ya 15 waachiliwe huru chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, kwasababu DPP hana haja ya kuendelea na kesi dhidi yao kwasababu umekosekana ushahidi wa kuendelea kuwashtaki.

“Kwakuwa kesi hii imefunguliwa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri na upande huo wa Jamhuri leo umewasilisha ombi la kuiomba mahakama iwafutie kesi, mahakama hii inakubali ombi hili na inawaachiria huru washtakiwa sita tu, washtakiwa waliosalia wataendelea kubaki kuwa washtakiwa katika kesi hii”alisema Jaji Dk.Twaibu.

Sekunde chache baada ya washtakiwa hao kuachiliwa huru na kutolewa na askari wa jeshi la Magereza nje ya kordo ya Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, baadhi ya washtakiwa hao walioachiliwa huru walianza kuzungumza kwa sauti ya juu hali iliyosababisha askari Magereza kutoka nje na kuwataka wakae kimya.

Baada ya Jaji Dk.Twaibu kutoa uamuzi huo, Mkurugenzi Msaidi katika ofisi ya DPP, Boniface aliambia mahakama hiyo kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao ambapo alianza kuwasomea maelezo hayo kwa kudai kuwa Julai 31 mwaka 2009 katika Benki ya NMB Tawi la Temeke, watu wawili wasiliyo na hatia mmoja akiwa ni askari wa Jeshi la Polisi, E.329 Koplo Josephat Milambo na mlinzi mwingine wa benki hiyo Seif Mkwike waliuwawa kwa kupigwa risasi na majambazi waliokuwa wamevamia benki hiyo.

Boniface ambaye pia ni Wakili Kiongozi wa Serikali, alidai tukio hilo lilitokea saa 4:30 asubuhi ambapo majambazi hao walivamia benki hiyo kwa nia ya kuiba fedha na kabla ya kufanya jambo lolote , majambazi hao walitoa silaha zao na kuwaelekezea moja kwa moja maofisa wa polisi ambao walikuwa wamekaa kwenye chumba cha walinzi.

Alidai baada ya majambazi hao kuwaelekezea polisi hao silaha, maofisa hao wa polisi nao walilazimika kuingia kwenye mapambano ya silaha dhidi ya majambazi hao na matokeo ya mapambano hayo ya silaha yalisababisha marehemu hao wawili kufariki dunia na majambazi hao wakafanikiwa kuingia ndani ya benki hiyo na kuondoka na kiasi cha fedha kisichofahamika.

“Katika eneo la tukio majambazi watatu yaani mshtakiwa aitwaye Yusufu Mlete, Issack Abdul ‘Swai” na MT 55935 Sajenti Mathew Mwangunga walitambuliwa na baadaye mashahidi walikuja kuwatambua na baada ya majambazi hao watatu kukamatwa wakitambuliwa tena na mashahidi katika gwaride la utambuzi lililokuwa limeandaliwa na Jeshi la Polisi”alidai wakili Boniface.

Aliendelea kueleza kuwa kadri majambazi wale hao waliohusika katika tukio hilo walivyokuwa wakizidi kukakamatwa na kisha wakahojiwa na polisi , majambazi katika maungamo yao walikiri kutenda makosa hayo ya mauji ya watu wawili .

Wakili Boniface aliwataja majambazi hao (washtakiwa) ambao walikiri kutenda kosa hilo katika maungamo yao ni Richard Muhanza, Mlete, Matonya, Tawete Salum, Said Hamiusi ‘Katikati’ na Makai. Na kwamba washtakiwa hao waliokiri kutenda kosa hilo walikamatwa kwa pamoja huko Mbagala Kuu wakati wakijiandaa kupanga njama za kufanya tukio jingine la uhalifu.

“Na mtukufu Jaji maungamo yao waliyoungama polisi waliungamba mbele ya ASP-Ndagile Makubi kuwa walihusika kutenda kosa la mauji ya watu wa wiwili katika NMB Tawi la Temeke, Julai 31 mwaka 2009”alidai wakili Boniface.

Aidha alidai kuwa miili ya marehemu hao ilifanyiwa uchunguzi na wataalamu na ripoti ya uchunguzi ikaonyesha marehemu Seif Athuman Mkwike aliuwa kwa shinikizo la damu na marehemu Koplo Milambo naye aliuwa kutokana na mlipuko wa bomu la mkono lililorushwa na washtakiwa hao siku ya tukio.

Hata hivyo wakili wa utetezi Amour Khamis alidai kuwa washtakiwa wote wanakanusha maelezo hayo ya awali waliyosomewa na upande wa Jamhuri na kwamba wanachokubali ni majina yao tu.

Baada ya pande hizo mbili kutoa maelezo hayo, Jaji Twaibu aliutaka upande wa Jamhuri kuleta orodha ya mashahidi na vielelezo watakavyovitumia kwenye kesi hiyo Novemba 22 mwaka huu, na kwamba anaiarisha kesi hiyo hadi Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, atakapoipanga tena.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Oktoba 25 mwaka 2011.
mwisho.

No comments:

Powered by Blogger.