Header Ads

CHADEMA YAILIZA CCM UBUNGO



Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Rufani jijini Dar es Salaam, imetoa amri ya kuiondoa rufaa iliyokuwa imekatwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Ubungo(CCM), Hawa Ng’umbi  dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo(Chadema) na wenzake bila gharama baada ya kuridhia maombi ya pande zote mbili zilizokuwa zimeiomba mahakama hiyo iiondoe rufaa hiyo mahakamani.

Amri ya kuindoa rufaa hiyo ilitolewa jana na kiongozi wa jopo la majaji wa tatu wa mahakama ya Rufani iliyoketi Dar es Salaam, Natalia Kimaro,Salum Massati na Catherine Oriyo ambapo jaji Kimaro alisema anaiondoa rufaa hiyo iliyokuwa ikipinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, katika kesi ya kupinga ubunge wa Mnyika iliyokuwa imefunguliwa na Ng’umbi ambapo Jaji wa Mahakama Kuu Upendo Msuya mwaka huu, katika hukumu yake alitupilia mbali kesi hiyo ya Ng’umbi kwa madai kuwa alishindwa kuleta ushahidi thabiti ambao unaonyesha taratibu na sheria za uchaguzi zilikiukwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambao ulimtangaza Mnyika kuwa ni mbunge halali wa jimbo hilo.

“Kwa kuwa mwomba rufaa (Ng’umbi) na mjibu rufaa(Mnyika) kabla ya leo kuja hapa mahakamani walikuta nje ya mahakama na kufikia uamuzi wa kuliondoa bila gharama  rufaa hii ambayo leo ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa na leo mawakili wao wamekuja kuwasilisha ombi hilo mbele ya mahakama hii, basi mahakama hii inakubali ombi lao hilo na linatoa amri ya kuiondoa rufaa hii chini ya 102(3) na (4) cha Kanuni za Mahakama ya Rufaani nchini”alisema Jaji Kimaro.

Awali kabla ya kutolewa kwa amri hiyo ya mahakama,wakili aliyekuwa akiwawakilisha wajibu rufaa wengine ambao ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ubungo, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao walikuwa wakitetewa na wakili wa seriakali Obadia Kameya wakaji mjibu rufaa wa kwanza alikuwa akitetewa na Edson Mbogoro waliianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kusikilizwa rufaa na kwamba wapo tayari kwaajili ya kuendelea.

Lakini wakili wa Ng’umbi alisimama na kujitambulisha na kisha akaeleza kuwa ni kweli rufaa hiyo iliyokuwa imekatwa na mteja wake ilikuwa imekuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa ila siku mbili zilizopita N’gumbi na Mnyika walikuta  na kufanya mazungumzo ambayo yaliitimishwa kwa kukubaliana kuwa rufaa hiyo waiondoe mahakamani bila gharama na kwamba mteja wake amemwelekeza awasilishe ombi hilo la kuomba rufaa hiyo iondolewe mahakamani bila gharama.

Baada ya kuwasilisha hilo wakili wa Kameya na Mbogoro walieleza kuwa hawana pingamizi na ombi hilo na kwamba wanaiachia mahakama iamue na ndipo mahakama ikafikia uamuzi wa kuliondoa rufaa hiyo mahakamani jana.

Baada ya Jaji Kimaro kumaliza kutoa amri hiyo ,Mnyika ambaye jana alikuwepo mahakamani hapo licha Ng’umbi hakuwepo mahakamani hapo, Mnyika  nje ya mahakama aliwaeleza waandishi wa habari kuwa amefurahishwa na uamuzi huo na kwamba.

“Ni wakili wa Ng’umbi ndiye alimpigia simu wakili wangu Mbogoro wakutane ili wazungumzie ombi la Ngu’mbi la kutaka kuiondoa rufaa yake aliyoikata dhidi yangu na kisha mawakili wetu wakaja kunikutanisha mimi na Ng’umbi tukazungumzia ombi hilo la Ng’umbi na tukakubaliana na ombi lake lilotaka aiondoe rufaa yake”alisema Mnyika huku akiwa amezingirwa na umati wa wafuasi wake.

Aidha wafuasi wa Mnyika wengine wakiwa wamebeba ndera za chama cha Chadema, waliondoka katika eneo la mahakama ya rufaa kwa maandamano huku wakiimba nyimbo za kupongeza uamuzi huo na kumsifia Mnyika ambaye kwasasa atakuwa hakabiliwi tena na kesi ya kupinga ubunge wake katika mahakama ya yoyote hapa nchini.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Desemba 8 mwaka 2012.

 

No comments:

Powered by Blogger.