Header Ads

GODBLES LEMA AREJESHEWA UBUNGE WAKENa Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Rufaa nchini imetengua hukumu  ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyotolewa Aprili 15 mwaka huu ambayo ilimvua ubunge, mbunge wa Arusha Mjini(Chadema), Godbles Lema kwa maelezo kuwa hukumu hiyo ilikuwa na mapungufu ya kisheria.

Hukumu hiyo ilisomwa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya rufaa Elizabeth  Mkwizu kwaniaba ya jopo watatu waliokuwa wakiongozwa na Nataria Kimaro, Salum Massati na Bernad Ruhanda saa tatu asubuhi na kusema kuwa jopo hili lilisikiliza hoja 18 zilizowasilishwa na Lema lakini mahakama hiyo imeamua kuitolea uamuzi hoja moja tu na hoja nyingine 17 haijazijadili.

Mkwizu alisema hoja ambayo mahakama iliifanyia kazi ile hoja ya Lema iliyokuwa ikidai kuwa wajibu rufaa(wanachama wa CCM), hawakuwa na haki ya kumshtakiwa Lema, ambapo jopo hilo limekubalina na mawakili wa Lema, Tundu Lissu na Method Kimomogoro na wakili wa Mwanasheria Mkuu wa serikali Timon Vitalis kuwa ni kweli wajibu maombi hawakuwa na mamlaka ya kumshtaki Lema kwani vitendo vinavyodaiwa kufanywa na Lema havikuwaathiri wajibu rufaa.
‘Pia hakuna ushahidi kama wajibu rufaa kwenye ni wapiga kura wa jimbo la Arusha mjini na kwasababu hiyo mahakama hii inatengua hukumu ya mahakama kuu ilimvua ubunge Lema, na badala yake inamrejeshea ubunge wake Lema tena kwa gharama”alisema Mkwizu.

Baada ya kumaliza kusoma hukumu hiyo, umati wa wafuasi wa Chadema ambao ulikuwa umeongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ulilipuka kwa shangwe na mayowe ya furaha na hali wengine kusimama juu ya viti vya ukumbi wa wazi wa mahakama hiyo ambao ulitumika kuendeshea rufaa hiyo na kuisikiliza.

Na wafuasi wengine walikimbilia kumbemba juu Lema na kusababisha Lema kutoa sauti ‘mtaniua mtania’.Kisha Mbowe na wabunge wengine vijana wa chama hicho walipanda kwenye gari la wazi aina ya Toyota Hilux yenye namba za usajili T 910 ARF na kuanza kuhutubia mamia ya wafuasi wake ambapo Mbowe alisema wamefurahiwa na hukumu hiyo  ambayo imerejesha heshima ya mahakama ambayo ilikuwa imeanza kupotea na kisha kuwataka wananchama hao waliokuwa wamefunga njia na kusababisha magari yasipite katika barabara hiyo iliyopakana na mahakama ya rufaa na kuwataka waondoke barabarani hapo na waanze safari ya kuelekea Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni kwaajili ya kushangilia ushindi wa kesi hiyo.

Kwa upande wake wakili wa Alutha Mugwai alisema ameshangazwa na hukumu hiyo kwani wakati kesi hiyo ikikisilizwa na mahakama kuu, suala la wajibu maombi kuwa walikuwa ni waliandikishwa kuwa ni wapigakula wa jimbo la Arusha Mjini halikubishaniwa  na kwamba kadi zao za kupiga kura za wanachama hao zilitolewa mahakama kuu.

Katika hatua nyingine,baadhi ya mawakili na wananchi wa kawaida wamezungumza na mwandishi wa habari hizi wakati wakitoa maoni yao kuhusu hukumu hiyo walisema kitendo cha mahakama hiyo kushindwa kutolea uamuzi hoja nyingine 17 ,huko tuendako kinasababisha tabu ya kupata mwongozo sahii katika mashauri mbalimbali ambayo yatakuja kujitokeza yanayofanana na hoja zilizokuwa zimewasilishwa na Lema na wakili wa wajibu Rufaa.

“Hatujashangazwa sana na kauli ya mahakama kusema kuwa jopo halijazitolea uamuzi hoja nyingine 17 kwani mara kwa mara mahakama ya rufaa wamekuwa wakifanya hivyo, hali inayotupa ugumu sana sisi mawakili wa kujitegemea,serikali katika mashauri mbalimbali ambayo yanatutaka tutumie maamuzi ya mahakama ya rufaa ili tuweze kutetea hoja zetu katika kesi zetu”alisema wakili mmoja kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Desemba 4 mwaka huu, mahakama ya rufaa ilisikiliza rufaa ya Lema  ambapo Lema aliwasilisha sababu 18 za kupinga hukumu ya mahakama kuu ambapo aliomba mahakama hiyo itengue hukumu ya mahakama kuu kwasababu haina hadhi ya kuitwa hukumu na mawakili wa wajibu Rufaa, aliomba mahakama isitengue hukumu ile kwasababu hukumu ile ni  imekidhi matakwa yote ya kisheria.

Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Desemba 22 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.