Header Ads

SANGOMA ANASWA NA MATUNGULI MAHAKAMA YA KISUTU
Na Happiness Katabazi

KIFAA  maalumu kinachotumiwa na wanausalama kuwapekua watu wanaoingia kwenye eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, siku ya kesi ya  uchochezi na wizi wa Sh milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49 inapokuja kusikilizwa mahakamani hapo, kimefanikiwa kumnasa mganga wa kienyeji akiwa na vifaa vyake vya kiganga ‘ matunguli’ ambaye alikuja kufanya  mambo ya kishirikina mahakamani hapo ambayo yangeweza kumsaidia mteja wake anayekabiliwa na kesi ya jinai mahakamani.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana saa mbili katika geti kuu la kuingia ndani eneo la mahakama hiyo ambapo askari kanzu na wale waliovalia sare za Jeshi la Polisi siku za kesi ya Ponda inapokuja kuendelea mahakamani, wanausalama hao ufika asubuhi na kuweka kambi kati eneo la geti hilo huku wakiwa na kifaa maalum cha kuwapekulia watu na kisha kuakikisha wanampekua mtu mmoja baada ya mwingine na kisha ndiyo wanamruhusu aingie ndani ya eneo la mahakama hiyo kwaajili ya kuimaliza ulinzi na usalama katika eneo hilo.
Jana kesi ya Ponda na wenzake ilikuja kwaajili ya kutajwa ndiyo maana wanausalama hao walikuwepo mahakamani hapo kwaajili ya kuimalisha ulinzi.
Wakati wanausalama hao wakipekuwa watu waliokuwa wakitaka kuingia ndani ya viwanja hivyo walifikia zamu ya kumuwekea kifaa hicho maalum mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Rajabu Zuberi(30), ambaye alisema yeye ni mganga wa kienyeji  na  ni mkazi wa eneo la Kerege Wilayani Muheza Mkoani Tanga.
Wakizungumza na waandishi wa habari wanausalama hao waliomkamata Rajabu ka masharti ya kutotajwa majina yao kwasababu wao siyo wasemaji wa jeshi la polisi, waliwaeleza waandishi wa habari za mahakamani waliokuwepo eneo hilo la tukio na kumshuhudia Rajabu akiwa amewekwachini ya ulinzi huku akiwa na matunguli yake, walisema baada ya kumuwekea kifaa hicho cha upekuzi katika mfuko uliokuwa umeshikwa na Rajabu,kifaa hicho kilianza kupiga kelele.
Wanausalama hao walisema baada ya kifaa hicho kupiga kelele walianza kumhoji Rajabu ndani ya ule mfuko alikuwa amebeba nini, mtu huyo huyo akawajibu wanausalama hao kuwa mfuko huo alikuwa amebebeshwa na  na mama mmoja  ambaye ni mfanyabiashara  aitwaye Senorine Urasa (35) na ni mkazi wa Kimara Dar es Salaam.
“Na Rajabu akatueleza kuwa huyo Senorine tumeishamkagua na tayari ameshakimbilia kwenda  katika choo cha wanawake kilichopo ndani ya mahakama ya Kisutu”alisema mwanausalama mmoja.
Mwanausalama mmoja aliendelea kuwaeleza waandishi wa habari kuwa baada ya Rajabu kuwaeleza hilo, ndiyo baadhi ya wanausalama wakaamua kwenda na Rajabu hadi katika vyoo hivyo na kufanikiwa kumkuta Senorine na kumhoji ambapo Senorine mbele ya wanausalama hao likiri kumleta mganga huyo wa kienyeji  mahakamani hapo ili aweze kumfanya mambo ya imani za kishirikina ambayo yangeweza kumsaidia kaka yake ambaye ni mshtakiwa katika moja ya kesi ya jinai inayoendelea mahakamani hapo lani hata hivyo wanausalama hao hawakuweza kufanikiwa kulipata mara moja jina la kaka ya Senorine mara moja waandishi wa habari walimshuhudia a Rajabu akapandishwa kwenye gari la Polisi huku akiwa na matunguli yake na kisha kupelekwa kwenye Kituo Kikuu Kati cha Polisi kwaajili ya mahojiano zaidi.
Kufuatia tukio hilo la kukamatwa mtu huyo, baadhi ya mawakili wa serikali na mahakimu ambao hawakutaka kutajwa jina lao gazetini wameliambia gazeti hili kuwa wanalipongeza jeshi la polisi kwa kufanikiwa kumnasa mtu huyo ambaye vifaa alivyokamatwa navyo vinaonyesha wazi alikuwa amefika mahakamani hapo kwa kazi moja ya kuja kufanya mambo ya kishirikina ambayo yamekuwa yakiwaathiri wao pamoja na mashahidi.
“Hii  kazi ya uhakimu, uendeshaji wa mashtaka siyo nyepesi kama watu wanavyofikiri, tunakutana na mambo mengi tena mazito yakiwemo ya kufanyiwa vitendo vya kishirikina na baadhi ya ndugu wa washtakiwa ila ndiyo hivyo hatuna pakwenda kulalamikia,ni mungu tu ndiye anatulinda na tukio hilo la leo limeonyesha wazi kuwa wengine wanaokuja hapa mahakamani hawaji kwa wema wanakuja kwaajili ya kuja kudhuru watu wengine wasiyo na hati kwa njia kama hizi za kishirikina na tunawapongeza wanausalama na ahojiwe zaidi”walisema kwa masharti ya kutotajwa majina yao.
Katika hatua nyingine jana kesi  ya uchochezi na wizi wa Sh. milioni 59 inayomkabili Ponda, Ponda alishindwa kufika mahakamani hapo kwa kile kilichoelezwa na wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka kuwa amepokea taarifa kutoa jeshi la Magereza kuwa Ponda ni mgonjwa na hivyo  askari magereza wameshindwa kumleta mahakamani jana.
Wakili Kweka aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na kusikilizwa pia ila mshtakiwa Ponda ni mgonjwa na mshtakiwa mwingine ambaye Ally Shaban naye ni mgonjwa na hawajafika mahakamani na wakili wa washtakiwa, Nassor Mansoor na kwamba ili haki itendeke ,anaiomba mahakama hiyo iiarishe kesi hiyo .
Ombi ambalo lilikubaliwa na hakimu Nongwa ambaye aliarisha kesi hiyo hadi Desemba 31 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya shahidi wa nne wa upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wake na akaamuru mshtakiwa wa tano, Mukadam Abdal Swalehe(45) ambaye katika kesi hiyo ya jinai Na.245/2012 arudishwe gerezani kwasababu bado Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi hajaiondoa hati yake aliyoiwasilisha ambayo imefunga dhamana ya Ponda na Mukadam.
Awali Oktoba 18 mwaka huu, ilidaiwa na wakili Kweka kuwa kosa la kwanza alidai ni la kula njama ambalo linawakabili washitakiwa wote,kosa la pili ni kwaajili ya washitakiwa wote ambalo ni la kuingia kwa nguvu kwa nia ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 85 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kuwa Oktoba 12 mwaka huu huko Chang’ombe Markas, wasipokuwa na sababu za msingi waliingia kwa jinai kwenye kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd, kujimilikisha kiwanja hicho kwa njia ya iloyopelekea uvunjifu wa amani,wizi ambapo baada ya kuvamia waliiba vifaa na malighafi ikiwemo nondo, kokoto zenye jumla ya thamani ya Sh. 59,650,000 mali ya kampuni ya Agritanza na kosa la tano ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 390 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ambalo sasa kosa hili la uchochezi litamkabili Mukadamu na Ponda peke yao kuwa wakiwa ni viongozi wa jumuiya hiyo , Oktoba 12 mwaka huu ,waliwashawishi wafuasi wao watende makosa hayo hata hivyo walikanusha mashtaka yote.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Desemba 19 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.