KESI YA LULU YAFUNGWA KISUTU,YAAMISHIWA MAHAKAMA KUU
*Dhamana ya Hassanor yasikilizwa, uamuzi utatolewa Jumatatu
Na Happiness Katabazi
UPANDE wa serikali katika kesi ya kuua
bila kukusudia inayomkbaili msanii wa filamu nchini Elizabeth Michael maarufu
kama Lulu ambaye anadaiwa kumuua bila kukusudia msanii mwenzake Steven Kanumba,
jana ulimsomea kwa mapana kesi inayomkabili mshtakiwa huo (Comittal
Procedings).
Wakili Mwandamizi wa Serikali Shadrack
Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi Mmbando
alidai kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kumsomea maelezo ya awali
mshtakiwa huyo na alianza kwa kumsomea
maelezo uya mashahidi ambao anakusudia kuwaleta katika kesi hiyo na maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo pamoja na kuvitaja vielelezo watakavyovitumia
katika kesi hiyo hiyo itaakapoanza kusikilizwa Mahakama Kuu.
Wakili Kimaro alieleza kuwa pia wataleta
mashahidi tisa na vielezo ikiwemo ramani ya eneo la tukio kwenye chumba
alichofia marehemu Kanumba, ripoti ya uchunguzi wa kifo na maelezo ya onyo ya
Lulu.
Aliwataja mashahidi hao wanaokusudia
kuwaleta katika kesi hiyo ni Sethi
Kamugisha (24) ambaye alikuwa akiishi na Kanumba, Sophia Kassim (45) ambaye
alimpangisha Kanumba, Dk Paplas Kagaiga (29) ambaye alikuwa daktari wa Kanumba,
Esther Zefania (40) askari polisi Oysterbay, Morris Sefwao mkazi wa
Kijitonyama, Mrakibu wa Polisi (ASP) Daniel Shilla kutoka ofisi ya Mkuu wa
Upelelezi mkoa wa Kinondoni, Dk Magreth Ibobo (40) ambaye aliombwa na familia
ya Kanumba kusimamia upasuaji wa mwili, Inspekta Mwesiga (35) Afisa Uhamiaji
kutoka kituo cha Horohoro Tanga na Ditective Sajent Renatus wa kituo cha polisi
Oyesterbay.
Akisoma maelezo ya onyo ya Lulu mbele ya
Hakimu Mkazi Augustina Mmbando, wakili wa serikali, Shadrack Kimaro, alidai
kuwa Lulu alitoa maelezo hayo Aprili 7 mwaka huu katika kituo cha polisi
Oysterbay mbele ya askari wa kituo hicho Ditektive Sajent Renatus.
Alidai kuwa Lulu alizaliwa mwaka 1994 na
kwamba alimaliza kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Midway na baada ya
hapo aliendelea na shughuli za sanaa ambazo aliianzia kuzifanya tangu mwaka 2000.
Kimaro alidai Lulu alifahamiana na
Kanumba kwa muda wa miaka 10 na walikuwa wakifanyakazi za sanaa ya uigizaji
pamoja na Januari mwaka huu ndipo
walipoanza rasmi mahusiano ya kimapenzi.Katika mahusiano yao ya kimapenzi hawakuwahi kuishi
pamoja isipokuwa alikuwa akienda nyumbani kwa marehemu anapojisikia na alikuwa
wakati mwingine akilala huko.
Wakili huyo alidai kuwa katika kipindi
cha miezi minne ya mahusiano yao walikuwa wakigombana mara chache lakini sababu
kubwa ilikuwa ni wivu wa mapenzi kwa sababu wote walikuwa hawaaminiani katika
mahusiano..
Pia wakili huyo alidai kuwa Aprili 5 mwaka
huu Kanumba na Lulu walitumiana ujumbe mfupi wa simu. Baadhi ya jumbe hizo
zilisomeka hivi.
Kanumba: Uniheshimu, unanidharau,
unanijibu unavyotaka wewe.. nakupenda sana..this love kill me soon..vipi baby
mzima umekula? nakupenda mke wangu..natarajia kwenda USA hivi karibuni je
nikuletee zawadi ipi kwa ajili ya birthday yako?
Alidai kuwa Lulu alimjibu kwa kumtumia
ujumbe wa kumtuliza kama vile nakupenda mme wangu..niletee zawadi yoyote ile
lakini ujumbe mwingine haukumbuki na kwamba walipatana siku hiyo hiyo.
Alidai kuwa jioni ya siku hiyo Lulu
alimpigia simu Kanumba na baada ya muda mfupi alikwenda nyumbani kwake Sinza
Vatican. Alidai kuwa alipofika kwa Kanumba chumbani kwake alimkuta akinywa
pombe ambayo ilikuwa imechanganywa na soda na ghafla simu yake iliita na
alipotoka nje kutaka kwenda kuisikiliza Kanumba alimfukuza hadi barabarani.
Alidai kuwa baada ya kumkimbiza alimkamata na kuanza kumpiga vibao na mateke
huku akilalamika kwamba anamdharau na alimpeleka hadi chumbani ambapo alichukua
panga lililokuwa chini ya kitanda na kuanza kumpiga kwa ubapa.
Alidai kuwa baada ya kumpiga kwa upanga ghafla
alitupa panga chini huku akiwa amesimama alianza kupumua kwa taabu na baada ya
muda mfupi alipojigonga ukutani na kuanguka chini. Alidai baada ya kuanguka,
Lulu alikimbia na kwenda kujifungia chooni kwa hofu na baada ya muda alitoka na
maji na kwenda kummwagia Kanumba lakini hakuamka.
Alidai kuwa baada ya kuona hali hiyo
alishikwa na hofu na kuamua kukimbia kwenye ufukwe wa Coco Beach.Alidai kuwa
akiwa huko alipewa taarifa kuwa Kanumba amefariki na ndipo alipompigia simu
rafiki yake ili aende kumsaidia kuendesha gari waelekee kwenye msiba.
Kwa mujibu wa maelezo ya mashahidi
yaliyosomwa mahakamani hapo inadaiwa kuwa Aprili 6 mwaka huu saaa 3 usiku Kanumba
akiwa nyumbani kwake, alimwambia mdogo wake Sethi asitoke kwakuwa kuna mahali
wanataka kwenda hivyo amsindikize na kwamba alikuwa akinywa kinywaji aina ya
Wisky.
Inadaiwa kuwa ilipofika majira ya saa 6
usiku Lulu alifika nyumbani kwa Kanumba na kuingia hadi chumbani na baada ya
muda walianza kugombana na baada ya kuanguka mapovu yalianza kumtoka mdomoni.
Aidha alileza kuwa baada ya Kanumba kuanguka, mdogo wake
aliwasiliana na daktari wa Kanumba na baada ya kufika aligundua kuwa Kanumba
tayari alikuwa amefariki lakini alishauri apelekwe hospitali ndipo walipoamua
kumpeleka hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo baada ya kupimwa iligundulika
kuwa amefariki.
Na baada ya Kanumba kufariki, Lulu alitoroka na
baada ya kutafutwa aliwekewa mtego na kukamatwa saa 11 alfajiri katika eneo la
Bamaga na kupelekwa kituoni Oysterbay.Uchunguzi wa awali wa polisi ulionyesha
kuwa hakukuwa na jeraha lolote kuanzia kichwani hadi mwilini.
Baada ya kusomwa maelezo hayo Hakimu
Mmbando alimuhoji Lulu kama ana lolote la kuongea na baada ya kujadiliana na
wakili wake, Lulu alijibu kuwa ana cha kuongea.
“Mahakama hii inaziarifu pande zote mbili
katika kesi hii kuwa kesi yenu leo imefikia mwisho katika mahakama hii hivyo jarada la kesi hii linaamishiwa
mahakama kuu tayari kwaajili ya kuanza
kusikiliza na kwamba Lulu utaendelea kuishi rumande hadi pale utakapokea wito toka Mahakama Kuu
wa kukuita kwaajili ya kesi yako.”alisema Hakimu Mmbando na kuahirisha kesi
hiyo.Wakati huo huo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana isikiliza ombi la kuomba apatiwe dhamana Mwenyekiti wa Mpira wa Soka mkoa wa Pwani(COREFA),Hussein Othman Hussein 'Hassanor' na wenzake sita wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ya Sh bilioni 1.1 ambapo wanadaiwa walisafirisha kontena na pembe za ndovu kinyume cha sheria kutoka Tanzania kwenda Hong Kong nchini China.
Jaji Zaina Mruke alisikiliza ombi hilo ambapo Hassanor alikuwa akiwakilishwa na wakili wa kujitegemea Richard RWeyongeza ambao upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakiliwa na mawakili wa serikali waandamizi Biswalo Mganga, Mutalwemwa Kishenyi, Benard Ikokola ambapo hata hivyo mawakili wa serikali waliomba Hassanor asipewe dhamana kwasababu ametenda kosa la kesi hii wakati tayari anakabiliwa na kesi ya awali Na.209/2011 iliyopo mahakama ya KIsutu mbele ya Hakimu Devota Kisoka ,na kisheria mtu yoyote anayetenda kosa wakati yupo ndani ya dhamana ,mshtakiwa huyo anatakiwa asipewe dhamana.
Jaji Mruke aliarisha kesi hiyo jana saa 12:20 jioni hadi jumatatu saa tatu asubuhi ambapo atakuja kutoa uamuzi wa ama ampatie dhamana Hassanor na wenzake au laa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Desemba 22 mwaka 2012.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Desemba 22 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment