Header Ads

MAHAKAMA YA RUFAA YAKWAMISHA KESI ZA DOWANS, TANESCO

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Rufani Dar es Salaam, jana ilijikuta ikishindwa kuanza kusikiliza maombi mawili yaliyowailishwa mbele yake na kampuni ya Dowans dhidi ya Tanesco na pia kushindwa kuanza kusikiliza ombi la Tanesco linaloomba mahakama hiyo itoe amri ya kuzuia utekelezwa wa hukumu ya Mahakama Kuu Kanda iliyotolewa Septemba mwaka jana ambayo iliruhusu tuzo iliyopewa kampuni ya Dowans ya Dola za Kimarekani 65,812,630.03 isajiliwe hapa nchini kwasababu jaji mmoja katika jopo lilopangwa kusikiliza mapingamizi hayo wakati akiwa jaji wa Mahakama Kuu alitolea uamuzi moja ya mapingamizi hayo.

Hayo yalisemwa jana na Jaji Bernad Luanda kwaniaba ya majaji wenzake Natalia Kimaro na Catherine Oriyo muda mfupi baada ya mawakili wa Tanesco wanaowakilishwa na Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Dk.Angelo Mapunda na wakili wa Dowans ambaye ni Kennedy Fungamtama muda mfupi baada ya kujitambulisha na kuikumbusha mahakama hiyo kuwa wapo tayari kuendelea  na usikilizwaji wa pingamizi hayo.

Baada ya mawakili hao kusema hayo Kiongozi wa jopo la majaji hao Kimaro alisema mahakama yake haipo tayari kuendelea kusikiliza maombi hayo matatu ambapo ombi la kwanza ni ombi Na.53/2011 ambalo limewasilishwa mahakamani hapo na Dowans dhidi ya Tanesco  ambapo Dowans itupilie mbali hati kusudio ya kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa na Jaji Mstaafu wa mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,Emmilian Mushi Septemba mwaka jana ambayo iliruhusu tuzo ilitolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya kibiashara(ICC) kwa kampuni ya Dowans kwa madai halina msingi wowote na limefunguliwa nje ya muda.

Jaji Luanda alisema ombi la pili ni Na.142/2011 limewasilishwa mahakamani hapo na Tanesco dhidi ya Dowans.Katika ombi hili Tanesco wameiomba mahakama ya rufani itoe amri ya kuzuia utekelezwaji wa hukumu ya Jaji Mushi ambao uliruhusu tuzo ya Dowans usajiliwe.

Aidha jaji huyo alisema ombi jingine ni Na.131/2010 ambalo liliwasilishwa mahakamani hapo na Dowans dhidi ya Tanesco  ambapo Dowans inaiomba mahakama rufani ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara ambapo uamuzi huo ulitoa amri ya kuzuia mitambo ya Dowans isiuzwe, kuamishwa.Na kesi hii wakati ipo Mahakama Kuu ilishughulikiwa na Jaji Oriyo ambae hivi sasa  ni jaji wa mahakama ambaye amepangwa katika  jopo hilo kusikiliza maombi hayo.

“Ili haki ionekane inatendeka jopo hili limefikia uamuzi wa kuarisha usikilizwa wa maombi haya matatu kwasababu mmoja wa wanajopo letu yaani (Jaji Oriyo), alipokuwa jaji wa Mahakama Kuu alisikiliza na kutolea uamuzi moja ya ombi ambalo lilipaswa lianze kusikilizwa leo(jana) na jopo letu…na kwasababu hiyo leo hatutaweza kusikiliza hadi pale jopo jipya linatakapoundwa tena na uongozi na tarehe ya kuja kusikilizwa kwa maombi haya”alisema Jaji Luanda.

Kwa mujibu wa hati ya majibu ya kampuni ya Dowans dhidi ya Tanesco kwenye ombi Na.142/2011, wakili Fungamtama anaeleza  kuwa hadi kufikia Novemba 20 mwaka huu, siku ambayo aliwasilisha majibu yake kwa njia ya maandishi mahakamani  kuwa pamoja na mambo mengine deni wanalolidai Tanesco lilikuwa limefikia Dola za Kimarekani 176,318,457.45 sawa na Sh.122,577,442665.54 kwa kiwango cha Dola moja wa siku hiyo ya Novemba 20 mwaka huu, ilivyokuwa ikiuzwa kwenye maduka ya kubadilishia fedha za kigeni ambapo siku hiyo dola moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh. 1,606 kwa siku na liba nayo ilikuwa imepanda ambapo kila siku lipa hiyo ambayo ni ya asilimia 7.5 ya jumla tuzo  

Wakili Fungamtama hadi kufikia siku hiyo pia  liba wanaoyoidai Tanesco  ni asilimia 7.5 ya   tuzo ya Dola za Kimarekani   65,812,630.03 ambayo liba hiyo inaongezeka kila siku tangu ilipotolewa na Jaji Mushi Septemba mwaka jana.

Septemba mwaka jana,Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ,alitoa hukumu ya kuruhusu tuzo ya Dowans waliyopewa na mahakama ya ICC isajiliwe na akatupilia mbali hoja za Tanesco zilizotaka tuzo hiyo isisajiliwe kwa madai hoja hoja za Tanesco hazina mantiki ya kisheria na kwasababu hiyo Tanesco ilitakiwa iilipe Dowans Dola za Kimarekani 176,318,457.45 na liba ya asilimia 7.5 kila siku.

Hukumu hiyo ya Jaji Mushi ambayo Tanesco hawakuridhika nayo iliwafanya baadaye Tanesco kuwasilisha ombi mbele ya Jaji Dk.Fauz Twaib wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuomba mahakama  mahakama hiyo iwapatie kibali cha kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ile lakini Jaji Dk.Twaib katika uamuzi wake aliupilia mbali ombi hilo la Tanesco kwa maelezo kuwa Tanesco haikuwa na sababu ya kurudi tena Mahakama Kuu kuomba ruhusa ya kukata rufaa mahakama ya Rufaa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Desemba 6 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.