Header Ads

JAJI MKUU AWATAKA MAWAKILI WAJIKITE VIJIJINI




Na Happiness Katabazi

JAJI Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman amewataka wamawakili wakujitegemea wapya waende kutoa huduma ya sheria vijijini kwani huko vijijini kuna wananchi wanaoitaji huduma hiyo.

Wito huo ulitolewa jana Jaji Othman katika sherehe ya 47 ya kuwakubali na kuwasajili mawakili wapya 618 katika viwanja vya Shule ya Sheria Tanzania iliyopo Sinza ‘C’ jijini Dar es Salaam, ambapo alisema hata huko mikoani kuna mahakama pia ambapo wananchi wanataka kuwakilishwa na mawakili wa kujitegemea mahakamani.

Waliosajiliwa jana kuwa mawakili wa kujitegemea ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali jaji Fredrck Werema, Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela,Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais ,Sazi Salula, Balozi Ali Said Mchumo,Jenerali Ulimwengu na John Peter Kahungenge.

Jaji Chande alisema Julai mwaka huu, mawakili 283 walisajili kuwa mawakili na kwamba jana jumla ya mawakili wapya 618 ambao wanafanya kuwa jumla ya idadi ya mawakili waliopishwa kwa mwaka huu kufikia 901.

“Katika idadi hiyo ya 618 waliopishwa jana , mawakili 300 ni mawakili wa serikali toka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ofisi nyingine za serikali ambao wao wamefaulu mtihani waliopewa na Baraza la Sheria na mawakili 318 walifanya mtihani uliokuwa umeandaliwa na Shule ya Sheria Tanzania”alisema Jaji Mkuu Chande.

Jaji Chande alisema hapo awali mawakili wa serikali licha walikuwa wamelikuwa wakifanya mitihani ya uwakili lakini walizuiwa kuapishwa ili waingie kwenye orodha ya mawakili wa kujitegemea lakini jana kwa mara ya kwanza Tanzania imeandika historia mpya kwa kuwasajili na kuwakubali mawakili wa serikali wanaotoka taasisi mbalimbali za serikali kuwa mawakili wa kujigemea .

“Lakini licha ya mawakili hao wa serikali kukubaliwa kuwa mawakili wa kujitegemea lakini mawakili hao wanaotoka taasisi zote za serikali hawataruhusiwa kufanya kazi za uwakili wa kujitegemea ili kuepusha mgongano wa kimaslahi na mwajiri wao ambae ni serikali…..hivyo wameingia kwenye orodha ya mawakili wa kujitegemea licha hawataruhusiwa kufanyakazi za uwakili wa kujitegemea”alisema Jaji Chande.

Aidha jaji Chande aliwaasa mawakili hao kuzingatia nidhamu, utu,maadili na uweledi pindi watimizapo majukumu yao na kwamba waakikishe kila wakati wanapenda kujisomea ili waweze kujijengea uwezo katika taaluma yao.


Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa serikali Jaji Fredrick Werema amewaasa mawakili hao wapya kuzingatia maadili ya kitaaluma ya sheria, usafi na ukweli kwa wateja wao.

Jaji Werema ambaye wakati akitoa hotuba yake alikuwa akishangiliwa na watu alisema watu wengi wamekuwa wakilalamikia mlundikano wa kesi mahakamani unasababishwa na mahakimu,na mawakili wa serikali na kwamba yeye anachoamini ni kwamba ukosefu wa uweledi wa kitaaluma kwa mawakili wakujitegemea, waserikali na mahakimu ndiyo chanzo kikubwa cha msongamano huo.

‘Ndiyo maana minasema yeyeyote anayepinga uwepo wa Shule ya Sheria uwa na mshangaa na ninasema wazi anayepinga shule hiyo basi hoja yake hiyo haina tija kwa taifa kwani mimi ndiye mwanasheria namba moja ,tangu kuanzishwa kwa mafunzo yanatotolewa kwa na shule ya sheria ya sheria (Law School) naona matunda yake kwani wanaopata mafunzo hayo wakija ofisi kwangu naona wameiva ;

‘Ndiyo maana naona hata mtu yoyote anayetaka kuwa hakimu pia apitie mafunzo ya Shule ya sheria Tanzania, ili tuondokane na maamuzi ya ubabaishaji na mlundikano wa mashauri mahakamani kwani wanafunzi wanaotimu mafunzo hayo wakitoka hapo wanakuwa na uweledi wa fani ya sheria”alisema Jaji Werema.

Kwa upande wake rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Francis Stola alisema tayari fani ya sheria imeanza kugubikwa na wimbi la mmomonyoko wa uweledi katika taaluma na kwamba vyuo vinavyowafunza sheria wanafunzi, na taasisi zote zinazofanyakazi za kisheria hazina budi kuanza kuziba nyufa hizo hili fani hiyo ya sheria isije kushuka heshima na hadhi yake.

Nao baadhi ya mawakili waliosajiliwa jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela na wakili mwingine wa kujitegemea John Kahungenge walisema wao ni watumishi katika taasisi za serikali na kwamba wamefurahishwa kwa kupewa leseni za kuwa mawakili wa kujitegemea licha wao kuwa ni watumishi wa serikali na wakaipongeza serikali kwa uamuzi huo mpya wa kuwaruhusu mawakili wanaofanyakazi katika taasisi za serikali kusajiliwa kuwa mawakili wa kujitegemea.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Desemba 18 mwaka 2012. 

No comments:

Powered by Blogger.