MAHAKAMA YAMNG'ANG'ANIA PONDA
Na Happiness Katabazi
HATIMAYE
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemuona Katibu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu Sheikh Ponda Issa Ponda
na wenzake 49 wana kesi ya
kujibu.
Sambamba na
kuwaona washitakiwa wote wana
kesi,Hakimu Mkazi Victoria Nongwa pia ameamuru
Ponda na wenzake wapande kimbani
na kuanza kujitetea kuanzia kesho na keshokutwa.
Uamuzi huo
ambao ulikuwa ukisubiri kwa shahuku kubwa, ulitolewa jana saa 5:24 asubuhi na Hakimu Nongwa ambapo
hakimu huyo alianza kuikumbusha mahakama kuwa washitakiwa wote wanakabiliwa
na kosa la kula njama kutenda kosa,
kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Chang’ombe Markas, kujimilikisha kiwanja
hicho kwa jinai, wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.milioni 59 na kosa la tano ni uchochezi ambalo
linamkabili Ponda na mshitakiwa wa tano (Mukadamu Abdallah).
Hakimu
Nongwa alisema kabla ya kuanza kuandika uamuzi wake alipitia ushahidi wa 17 na
vielelezo 13 vilivyowasilishwa na upande wa jamhuri unaotetewa na wakili
Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka , mahakama imeuchambua ushahidi huo na
kuona kuna mashahidi ambao ni viongozi wa Bakwata walitoa ushahidi ulioonyesha kuwa kiwanja cha
Chang’ombe Markas zamani kilikuwa ni mali ya Bakwata lakini Bakwata ikaamua
kubadilishana kiwanja hicho na Kampuni ya Agritanza Ltd.
Hakimu
Nongwa alisema pia ushahidi ulitolewa na upande wa Jamhuri unaonyesha Bakwata
ipo chini ya waumini wa dini ya Kiislamu wote nchini, na kwamba kuna baadhi ya waumini wa dini ya
Kiislamu hawakuridhishwa na uamuzi wa Bakwata kuamishia umiliki wa kiwanja
hicho kwa kampuni ya Agritanza Ltd.
Hakimu huyo
akichambua hoja za wakili wa utetezi, Nassor Juma na Njama alizowasilisha
Februali 28 mwaka huu, zilizoomba mahakama hiyo iwaone washitakiwa hawana kesi
ya kujibu kwa sababu kesi inayowakabili si ya jinai ni ya madai ambayo inahusu
mgogoro wa ardhi ambao ilipaswa ikasikilizwe katika Mahakama ya Ardhi na siyo
Mahakama ya Kisutu.
“Kwanza
kabisa mahakama hii inapenda kuweka wazi kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi
za migogoro ya Ardhi ….na ieleweke wazi kuwa mahakama hii haijamzuia mtu yoyote
anajiona ana maslahi katika uuzwaji wa kiwanja hicho kwenda katika Mahakama ya
Ardhi kufungua kesi ya kupingwa uuzwaji wa kiwanja hicho na pia mahakama yangu
haiwezi kuzungumzia kesi za ardhi….na hoja hiyo ya wakili Nassor
naifananisha mfano baba anaamua kuuza
ardhi halafu wake wanakuwa hawajaridhika
na uamuzi huo , watoto wanaweza kwenda kufungua kesi mahakama ya ardhi kupinga
uamuzi huo wa baba yao….kwa kwa kifupi tu mahakama hii inasema hivi kesi hii ni
ya jinai na mahakama hii ina mamlaka ya kuisikiliza”alisema Hakimu Nongwa.
Hakimu
Nongwa alisema kwa mujibu wa kielelezo cha nne, tano, 11,13 ni maelezo ya onyo yaliyotolewa na baadhi ya
washitakiwa wakati wakihoji wa polisi, na ndani ya maelezo hayo ambayo
yalipokelewa kama vielelezo na mahakama hiyo yaonyesha washitakiwa
hawakuridhishwa na uamuzi wa Bakwata wa kuibadilishana ardhi ile na kampuni ya
Agritanza na ndiyo maana washitakiwa hao wakaamua kwenda kuweka kambi tangu
Oktoba 12-17 mwaka jana, katika kiwanja hicho kwa lengo la kukikomboa kiwanja
hicho ambacho washitakiwa wanadai ni mali ya waislamu ambacho kimeporwa na
kwamba aliyekipora ndiye ataenda mahakamani.
“Licha ya
wakili wa washitakiwa Nassor katika majumuisho yake alizama ndani kabisa hadi
kufikia hatua ya kusema ushahidi wa jamhuri hauna uzito wowote,mahakama hii
inaona katika hatua wakili huyo hakupaswa kuingia ndani hadi kupima uzito wa ushahidi
uliotolewa na upande wa jamhuri kwani tayari kuna ushahidi wa upande wa jamhuri
unaonyesha washitakiwa 48 walikiri kukamatwa wakiwa ndani ya kiwanja hicho isipokuwa wa Ponda na Mkadamu ambao
hawakukumatwa katika eneo hilo.
“Na ieleweke
wazi kila kesi ina mazingira yake na kesi hii tunaona kabisa kuna washitakiwa
katika maelezo yao ya onyo walikiri kukamatwa katika eneo hilo…sasa mahakama
hii imefikia uamuzi kuona upande wa jamhuri umeweza kujenga kesi yao na hivyo
imewaona washitakiwa wote wana kesi ya kujibu ili washitakiwa hao wapate fursa
ya kujitetea kwa kuileleza mahakama kuwa katika kiwanja siku hiyo wavyokamatwa
walikuwa wakitafuta nini’ alisema Hakimu Nongwa.
Aidha
alisema anaiarisha kesi hiyo hadi kesho na kesho kutwa ambapo washitakiwa hao
wataanza kupanda kizimbani kujitetea.Kesi hii inasikilizwa chini ya ulinzi
mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama ambapo baadhi ya wanausalama uketi ndani
ya ofisi ya mapokezi ya mahakama hiyo kwaajili ya kuwapokea wageni wote
wanaingia mahakamani na kisha kuwapekua kwa kifaa maalum.
Kesi hiyo ya
kwa mara ya kwanza ilifunguliwa mahakamani hapo Oktoba 18 mwaka jana ambapo washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa
matano likiwemo kosa la kula njama kutenda kosa,kuingia kwa jinai,
kujimilikisha eneo kwa njia ya jiani, wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.milioni
59 na uchochezi.
Wakati huo huo, Hakimu Mkuu Mkazi Ilvin Mugeta aliarisha kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya
umma inayomkabili Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Usafirishaji
(UDA), Idd Simba na wenzake hadi Aprili 4,5 mwaka huu, kwasababu upande wa
jamhuri hakuleta mashahidi kwaajili ya kuanza kuisikilizwa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 5 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment