Header Ads

LWAKATARE SASA AKIMBILIA MAHAKAMA KUU


 Na Happiness Katabazi

MAWAKILI wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), jana wamewasilisha Mahakama Kuu Dar es Salaam, ombi la kuomba mahakama hiyo iitije majadala ya kesi tuhuma za ugaidi zilizofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwaajili ya kuzifanyia marejeo.

Maombi hayo ambayo tayari yameishapewa namba 14 ya mwaka huu, na yameapwa na wakili wake  wa washitakiwa hao Peter Kibatara   yaliwasilishwa jana mchana na karani wa wakili huyo  mahakamani hapo.

Kwa mujibu wa kiapo kilichoapwa na wakili Kibatara, mawakili hao wanaomba mahakama hiyo ifanyie marejeo wa majadala ya kesi ya ugaidi Na.37/2013 iliyofunguliwa wa Machi 18 mwaka huu na Mkurugenzi wa Mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya Lwakatare na Ludovick Joseph mbele ya hakimu Emilius Mchauru  ambapo siku hiyo alisikiliza maombi  ya pande mbili.

Maombi ya mawakili wa utetezi yaliomba washitakiwa wapewe dhamana wakati mawakili wakuu wa serikali Ponsian Lukosi, Prudence Rweyongeza na Peter Mahugo waliomba mahakama isitoe dhamana kwasababu kesi makosa yanaoyoangukia katika sheria za ugaidi ya mwaka 2002 hayana dhamana.

Ambapo siku hiyo hakimu Mchauru aliairisha kesi hiyo hadi Machi 20  kwaajili ya kuja kutolea uamuzi wa maombi hayo pamoja na maombi mengine lakini  hakimu huyo alijkuta akishindwa kutoa uamuzi wake kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer  Feleshi amewasilisha  hati ya kuwafutia kesi washitakiwa hao chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kwasababu hana  haja ya kuendelea kuwashitaki.

Lakini dakika chache baada ya hakimu Mchauru kuwafutia kesi hiyo, wanausalama waliwakamata tena washitakiwa hao na kisha kuwapandisha mahakamani mbele ya Hakimu mwingine Alocye Katemana na wakili wa serikali  Rweyongeza alianza kuwasomea mashitaka manne mapya katika kesi mpya iliyopewa Na.6/2013 ambayo mashitaka ni yale yale  yaliyokuwa kwenye hati ya mashitaka ya awali  iliyofutwa na DPP,ambapo Katemana aliwataka washitakiwa wasijibu chochote na akaamuru waende gerezani hadi Aprili tatu.

Kwa mujibu wa madai yao mawakili wa Lwakatare wanaomba Mahakama Kuu ipitie uamuzi wa  DPP wa kuifuta hati ya awali ya mashitaka na kisha kuwafungulia kesi upya washitakiwa hao wakati kesi hiyo ilikuwa imekuja kwaajili ya mahakama kuitolea uamuzi lakini mahakama ikashindwa kutoa uamuzi wake kwasababu DPP aliwasilisha hati ya kuifuta kesi hiyo.

Kwa mujibu wa habari za kuaminika toka ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, zimelieleza gazeti hili kuwa tayari uongozi wa mahakama imeishatoa amri ya kuyaitisha majalada hayo mawili ya kesi yanayomkabili Lwakatare na mwenzake yatoke mahakama ya Kisutu yaletwe mahakama kuu kwaajili ya kuyafanyia marejeo.   

Kosa la kwanza ambalo linawakabili washitakiwa wote kuwa ni la kula njama kutenda kosa la jinai kinyume na kifungu cha 284  cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , na kwamba mnamo Desemba 28 mwaka jana, huko Kimara King’ong’o  Stopover, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia  sumu kwa lengo la kumdhuru  Denis Msaki  ambaye ni Mhariri wa habari wa Gazeti la Mwananchi ambalo ni kinyume na kifungu cha 227 cha sheria hiyo.

Wakili Rweyongeza alilitaja  kosa la pili kuwa ni la kula njama  ambalo pia ni kwaajili ya washitakiwa wote  ambalo ni kinyume na kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na.21 ya mwaka 2002, ambapo washitakiwa hao walitenda kosa la ugaidi la  kutaka kumteka Msaki  kinyume na kifungu  cha 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

Shitaka la tatu ni la washitakiwa wote ambapo wanashitakiwa kwa kosa la  kupanga kufanya makosa ya ugaidi  kinyume na kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi kwamba Desemba 28 mwaka jana,walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyaraka Msaki  kinyume na kifungu 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

Shitaka la nne, Rweyongeza alidai linamkabili Lwakatare peke yake  ni aliwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume na kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi , kwamba Desemba 28 mwaka jana, Lwakatale akiwa ni mmiliki nyumba hiyo ilipo Kimaraka King’ong’o  kwa makusudi  aliliruhusu  kufanyika kwa kikao hicho baina yake na Ludovick  cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka nyara Msaki hata hivyo walikanusha mashitaka hayo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Machi 23 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.