MANJI,MWALUSAKO WAKIMBILIA MAHAKAMA YA RUFAA
Na Happiness Katabazi
MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga Yusuph Manji na Katibu Mkuu wake, Lawrence Mwalusako, jana walifika katika Mahakama Kuu Diveshi ya Kazi Dar es Salaam lakini hawakusimama kizimbani kujieleza ni kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kosa la kudharau amri ya mahakama.
Manji ambaye pia ni mfanyabiashara na Mwalusako walifika mbele ya Msajili wa mahakama hiyo Mohamed Gwae lakini hawakuhojiwa chochote kwasababu jalada la kesi limepelekwa Mahakama ya Rufani kwaajili ya kufanyiwa marejeo.
Katika kesi hiyo timu ya Yanga inadaiwa kukiuka umuzi uliyokwishatolewa na mahakama hiyo ambayo iliitaka timu hiyo iweke mahakamani Sh milioni 106, kwasababu ilishindwa kuwalipa walalamikaji katika kesi hiyo, ambae ni Kipa wa zamani wa timu hiyo Stephen Marashi na beki raia wa Malawi, Wisdom Ndlovu.
Jalada la kesi hiyo hiyo limeitwa Mahakama ya Rufaa baada ya mdaiwa (Timu ya Yanga), kuwasilisha ombi katika mahakama hiyo ya Rufani linaloiomba mahakama hiyo ifanye marejeo ya uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu Diveshi ya Kazi ambao uliitaka timu hiyo iweke kiasi hicho cha fedha mahakamani.
Jana Msajili Gwae
alisema kuitwa kwa Manji na Mwalusako tena mahakamani hapo, kutategemea uamuzi
utakaotolewa na Mahakama ya rufaa.
Ombi hilo la Yanga la linaloomba Mahakama ya Rufaa ifanyie marejeo uamuzi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi , waliliwasilisha Machi 25 mwaka huu, chini ya hati ya dharura likiomba mahakama hiyo ya juu kabisa nchini iitishe jalada la kesi ya msingi ili iweze kuupitia mwenendo mzima wa kesi hiyo iliione uamuzi huo ulikuwa sahihi.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo kilichoapwa na mdaiwa wa pili ( Mwalusako) inayounga mkono ombi hilo, Oktoba 11 mwaka jana waliwasilisha ombi la marejeo pamoja na kuwasilisha ombi la kusitisha utekelezaji wa tuzo ya kuwalipa wachezaji hao.
Kwa mujibu wa hati hiyo, Februali 5 mwaka huu, Msajili Gwae ilikataa ombi la kusitisha utekelezaji wa hukumu hiyo na kuwataka Yanga kuweka fedha hizo mahakamani wakati wakisubiri uamuzi wa ombi la marejeo.
Anadai
kuwa, utekelezaji dhidi ya walalamikaji umekwenda kinyume na utaratibu
kwa kuwa msuluhishi alishindwa kuzingatia nafasi ya mlalamikaji katika suala
hilo, pia Klabu hiyo haina mali yoyote ya kuweza kutekeleza tuzo hiyo.
Katika kesi ya msingi, Marashi na mwenzake, wameiomba mahakama kumfunga jela mwenyekiti huyo na katibu wake, baada ya timu hiyo kushindwa kutekeleza amri ya mahakama, ikiamuru kiasi hicho kulipwa.
Kamisheni ya Usuluhishi na Upatanishi iliiamuru Yanga iwalipe wachezaji hao fedha hizo kutokana na kukatisha mkataba wao kinyume cha taratibu, na walitakiwa kulipwa wiki mbili kuanzia tarehe ya hukumu.
Yanga iliingia kwenye mgogoro na wachezaji hao, baada ya kuvunja nao mikataba mwaka 2010 kutokana na sheria mpya ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuzitaka klabu kuwa na nyota watano tu kutoka nje, hivyo kuwaacha Ndlovu, Mkenya John Njoroge na Mtanzania Marashi. Njoroge alilipwa milioni 17.
Walalamikaji hao
wanadai kuwa, walisajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili kuanzia Machi
18, 2010, wanadai Julai 17, 2010, wakiwa wanajiandaa na kipindi kingine kipya
cha msimu wa ligi, Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic aliwaambia kwa mdomo
kwamba wao si wachezaji wa Yanga.
Walidai kwa
mujibu wa mkataba, Yanga walitakiwa kuwasiliana nao kuhusu kukatisha mikataba
yao ndani ya siku saba kabla ya tarehe iliyokuwa imewekwa na TFF, kwa timu za
ligi kuu kuwasilisha majina ya wachezaji watakaoachwa jambo hilo liliwakosesha
nafasi ya kucheza katika timu nyingine.
Kamisheni
iliamuru, Ndlovu alipwe sh. milioni 57 kama mshahara wa miaka miwili, sh.
milioni 1.8 kama gharama za usafiri wa kumrejesha Malawi na sh. milioni 20 kama
fidia ya kumkosesha nafasi ya kucheza.
Kwa upande wa
Marashi, Yanga iliamriwa imlipe sh. milioni 18 kama gharama za kutia saini
mkataba na mshahara kwa miaka miwili, sh. milioni 10 kwa kupoteza nafasi ya
kucheza na sh. 500,000 kama malipo aliyopaswa kulipwa wakati anatia saini
mkataba wa 2009 hadi 2010.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 28 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment