WAKILI AJITOA KESI YA WAFUASI 54 WA PONDA
Na Happiness
Katabazi
WAKILI wa
upande wa utetezi katika kesi ya wafuasi 54 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu, Sheikh Issa Ponda ,Hamidu Ubaidi jana alitangaza kujitoa kuendelea
kuwatetea washitakiwa hao kwa kile alichodai kuwa kesi hiyo imekuwa ikiendeshwa
haraka na mfululizo na mahakama.
Kesi hiyo
ambayo jana ilikuja kwaajili ya mshitakiwa wa 24 ananza kutoa utetezi wake
lakini wakili Ubaidi mbele ya hakimu Sundi Fimbo aliomba kesi hiyo isiendelee
kusikilizwa kwasababu yeye anawasilisha ombi rasmi la kujitoa .
“Naona
sitawatendea haki washitakiwa ambao ni wateja wangu kulingana na kesi hiyo ya maandamano haramu
ya kutaka kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi ili
wamshinikize aondoe hati yake ya kumfungia dhamana Ponda, kwasababu kesi hii
inavyokwenda haraka na mfululizo kwani sipati muda wa kuzungumza na kuwaandaa
washitakiwa”alidai wakili Ubaidi.
Lakini hata
hivyo ombi hilo lililamikiwa na wakili mwandamizi wa serikali Benard Kongora,
Joseph Mahugo kwa madai hiyo ni mbinu ya kuichelewesha kesi hiyo isimalizike
haraka kwani uongozi wa mahakama ndiyo uliotoa fursa ya kesi hiyo iendeshwa
mfululizo tangu ilipofunguliwa mahakamani hapo Februali 18 mwaka huu.
“Mhesimiwa
hakimu ni huyu huyu wakili Ubaidi,Jumatatu
na Jumatano aliomba kesi hii tuairishe mara kwa lisaa limoja lakini
hakutokea …leo hii anakuja kuieleza mahakama kuwa eti anajitoa kuwatetea
washitakiwa kwasababu kesi hii inaendeshwa mfululizo na hapati muda wa
kuwaandaa washitakiwa wake….sisi upande wa jamhuri tunasema hii ni mbinu ya
kutaka kuchelewesha kesi hii isimalizike mapema kwani ni uongozi wa mahakama
ndiyo uliotoa fursa ya kesi hii kuendeshwa mfululizo hivyo sisi tunaona tutumie
fursa hiyo kuendesha kesi hii”alidai wakili Kongora.
Kwa upande
wake hakimu Sundi Fimbo aliarisha kesi hiyo hadi Machi 11 mwaka huu,
itakapokuja kwaajili ya washitakiwa kuendelea kujitetea.
Wakati huo huo; Jumla ya washitakiwa tisa wa kesi ya
uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh. Milioni 59 inayomkabili
Ponda na wenzake 49 ,waliyakana maelezo waliyoyatoa wakati wakihojiwa na jeshi
la Polisi ambapo wakati walipokuwa wakihojiwa na jeshi la polisi walikiri kuwa
walikamatwa katika eneo la kiwanja cha Markas Chang’ombe kinachomilikiwa na
kampuni ya agritanza Ltd. Lakini jana wakati wakitoa utetetezi wao walikanusha
kukamatwa eneo hilo na kwamba wao walikamatwa na polisi Oktoba 16 mwaka
jana,wakiwa ndani ya msikiti wa shule ya Markas Chang’mbe wakisali sala ya
Itikafu.
Washitakiwa
hao ambao walikuwa wakiongozwa na wakili wao Nassor Juma, ni mshitakiwa
10,11,12,13,14,15,16 na 17.
Wakihojiwa
na wakili Mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka ni kwanini jana walipopanda
kizimbani wametoa maelezo mapya wakati walipohojiwa na polisi walitoa maelezo
ya kikiri kukamatwa ndani ya kiwanja hicho ambacho kiliuzwa na Bakwata kwa
kampuni ya Agritanza Ltd.
Washitakiwa
hao wakijibu swali hilo wengine walidai hawajui kusoma na kuandika na wengine
wakadai kuwa hayo maelezo ni yao na saini ni zao ila hizo saini waliziweka
kwenye hayo maelezo baada ya kulazimishwa na askari polisi na wengine walidai
kuwa hawakufahamu ni kitu gani kilikuwa kikiandikwa na polisi waliokuwa
wakiwahoji kwasababu polisi hawakuwasomea hayo maelezo yao, na mshitakiwa
mwingine alidai maelezo aliyochukuliwa na askari yaliandikwa na wino wa blue na
siyo mweusi kama alivyoonyeshwa jana nakala ya maelezo yake ambayo yapo
mahakamani kama kielelezo na wakili Kweka.
Aidha kwa
ujumla wao washitakiwa hao walidai kuwa polisi waliwafanyia unyama, waliwapora
simu zao za mikononi,waliwatukana matusi ya nguoni na waliwapiga virungu na
kwamba baadhi ya askari polisi waliokuwa wamekuja kuwakamata ndani ya msikiti
walikuwa wananuka pombe na hawakuvua viatu wakati wanaingia ndani ya msikiti
kuwakamata.
No comments:
Post a Comment