Header Ads

WAWEKWA CHINI YA UANGALIZI NA MAHAKAMA


Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilitoa amri ya kuwaweka chini ya uangalizi kwa mwaka mmoja watuhumiwa  wanne ambao walifikishwa jana na upande wa jamhuri.

Wakili Mwandamizi wa Serikali Bernad Kongora mbele ya Hakimu Mkazi ,Mchauli aliwataja wananchi hao kuwa ni Sheikh Mkongo Hassan Zuberi, Basoty Tandele,Mohamed Hassan, Salum Athuman ambao hawakuwa na wakili.

Kabla ya hakimu kutoa amri hiyo ,wakili Kongora aliwasilisha ombi hilo la jinai Na.4/2013  chini ya kifungu cha 70,72 na 73 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambao aliomba mahakama itoe amri ya kuwataka washitakiwa waweke dhamana na kuwa na wadhamini kuwa wataakikisha kuwa na tabia njema  kwa kipindi cha mahakama itakapoona inafaa.
Wakili Kongora alieleza kuwa ombi hilo la jinai wameliwasilisha chini ya hati ya kiapo  ambacho kimeapwa na Kamishna Msakidizi wa Polisi, Hamisi Mhaka na kwamba washitakiwa wanakaa mburahati Barafu, Gongo la Mboto ,Tabata Bima na Tunduma mkoani Mbeya.

“Mheshimiwa hakimu hivi sasa jeshi la polisi lipo kwenye oparesheni dhini  ya watu  wanaojihusisha  na uchochezi na kuiaminisha jamii kufanya makosa  ya  kutukana  imani za kidini  na kwamba tunazo taarifa  kuwa watuhumiwa  hao wanajihusisha    na vitendio hivyo  vinavyohatarisha usalama wa jamii”alidai Kongora.

Akitoa masharti ya dhamana Hakimu Mchauli alisema ili wapate dhamana ni lazima  kila mshitakiwa asaini bondi ya Sh.milioni tano, wadhamini wawili wanaotoka taasisi zinazofahamika, wawe wanaishi makazi yanayofahamika, kuripoti polisi  na watakuwa chini ya uangalizi wa mahakama ndani ya mwaka mmoja kuanzia jana.

Itakumbukwa kuwa Mapema wiki hii Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova alifanya mkutano na waandishi wa habari na kusema jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata washitakiwa hao ambao wamewakuta wakitenda makosa ya uchochezi wa kidini na kwamba muda wowote wangefikishwa mahakamani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa,Machi 8 mwaka 2013

No comments:

Powered by Blogger.