Header Ads

WASHITAKIWA KESI YA PONDA WADAI POLISI WALIFANYIA UNYAMANa Happiness Katabazi

WASHITAKIWA sita kati ya saba ambao wanakabiliwa na kesi ya wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu,Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake jana walianza kujitetea na kudai walitendea unyama na ukatili na polisi waliokuja kuwakamata.
Mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa wakili washitakiwa hao Juma Nassor  aliwaongoza washitakiwa hao wote saba jana kwa mpigo kutoa utetezi wao na wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka alikuwa akiwahoji maswali mashahidi hao, ambapo jana kesi hiyo ilikuja kwaajili ya washitakiwa kuanza kujitetea.
Ambapo mshitakiwa 2,3,4,6,7,8 na tisa  ambao majina yao ni Kuluthumi Mfaume,Zainabu Mohamed,Zaida Yusufu ambaye hajui kusoma na kuandika ,Juma(22),Farida Nnko, ,Adam Ramadhan,Athumani Salim (40) ndiyo jana walipanda kizimbani kutoa utetezi wao wakati Ponda bado hajaanza kutoa utetezi wake.
Wote kwa ujumla washitakiwa hao katika utetezi huo walikiri kukamatwa na polisi Oktoba 16 mwaka jana  wakiwa ndani ya msikiti wa Shule ya Chang’mboe Markas wakiwa kwenye ibada maalum ya kusali Itikafu ambayo swala hiyo ni maalum ambayo inamuongezea nguvu za kiimani muuislamu anayesali swala hiyo ya Itikafu.
Washitakiwa hao walidai sala hiyo ya Itikafu ilianza kusomwa kuanzia saa 7,8 na tisa usiku wa siku hiyo na kwamba ilipofika saa tisa usiku wakiwa macho wanaendelea na kusali sala hiyo maalum walisikikia kishindo kizito na kabla ya kumaliza kutaamaki waliona askari polisi wakivunja milango na madirisha ya msikiti huo na kisha kuingia ndani ya msikiti  bila kuvua viatu na kuanza kuwapiga virungu na kuwakamata na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi cha Kijitonyama.
“Yaani hakimu nikwambie unapotaka kuingia msikiti kwanza ni lazima utie udhu kwanza ndiyo uingine msikitini  na msikitini hatuingiagi na viatu,lakini wale maaskari waliokuja kutukamata pale ndani ya msikiti wa Markas kwakweli walitufanyia unyama na ukatili wa hali ya juu, hakujali sisi tulikuwa tunasali walianza kutupiga na virungu na kututolea maneno ya kashfa kwamba ni kwanini tumeacha kulala na wanaume zetu tumekulala na wanaume zetu tumekuja kukesha msikitini”alidai shahidi wa saba ,Farida na kusababisha watu kuangua vicheko.

Washitakiwa hao  hata hivyo walikana kuifahamu Bakwata kwa madai kuwa wao dini yao kiislamu wanaongozwa na kitabu kitakatifu cha Kurani na Suna na siyo Bakatwa  lakini haya hivyo mshitakiwa wa nane (Adamu) yeye katika utetezi wake alidai anaifahamu Bakwata kama  ni taasisi ya inayowaongoza waislamu nchini na kwamba ndiyo imekuwa ikiwatangazia waislamu sherehe za Maulid pindi mfungo wa ramadhani unapomalizika.
‘Hivi wakili wa serikali kwanini unanilazimisha hilo swali la kwamba kiongozi wangu wa dini ni nani, nimeishakwambia mikiongozi wangu wa dini ya kiislamu ni kurani na suna na hiyo Bakwata siitambui kwasababu sina uhusiano nayo na siitaji kuitambua’alidai mshitakiwa Kuluthumu.
Hata hivyo washitakiwa wote wakijibu swali la wakili wa serikali Kweka lilokuwa likiwauliza walipataje habari za kwenda kwenye msikiti wa Markas, walijibu kuwa wao walipata taarifa kutoka kwa watu tofauti tofauti ambao hawawajui majina yao waliokuwa wakitangaza kuwa siku hiyo ya Oktoba 16 mwaka jana, katika  usiku wa manane katika Msikiti wa Markas kutakuwa na Sala ya Itikafu ndiyo wakaamua kuitikia wito huo kutoka kwa watu hao wasiyowajua na kwenda msikitini hapo kusali na wakajikuta wanakamatwa na polisi.
Oktoba 18 mwaka jana , washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na makosa matano likiwemo kosa la kula njama kutenda kosa, kuingia kwa jiani katika eneo la chang’ombe Markas, kujimilikisha kijinai eneo hilo, wizi wa malighafi zenye thamani y ash.milioni 59 na uchochezi ambapo washitakiwa hao wakati wakijitetea jana walikanusha mashitaka hayo.
Hakimu Nongwa aliarisha kesi hiyo hadi leo ambapo shahidi wa kumi anataanza kujitetea katika kesi hiyo inaondeshwa chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama ambayo inawakabili jumla ya washitakiwa 50.
Wakati huo huo , Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Waliarwande Lema jana alishindwa kuendelea kusikiliza kesi ya kuandika makala ya uchochezi inayomkabili mwandishi wa gazeti la Tanzania,Samson Mwigamba na Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari, Absalom Kibanda na Theophil Makunga kwasababu Kibanda amelazwa katika wodi ya Moi akiwa ana maumivu makali kwasababu ya usiku wa juzi kuamkia jana alivamiwa na watu wasiyojulikana walimvamia na kumshambulia vikali na hivyo kumsababishia maumivu hivyo hakimu huyo aliarisha kesi hiyo hadi Machi 26 mwaka huu.

Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 7 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.