Header Ads

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ATOA SOMO LA SHERIA WAKATI WA UCHAGUZI MKUU
Na Happiness Katabazi

KWA mujibu wa Ibara ya Ibara  ya 59.-(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977  ,inasomeka hivi nanunukuu; "Kutakuwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambaye katika ibara zifuatazo za Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama "Mwanasheria Mkuu" ambaye atateuliwa na Rais"

Ibara ya 59 (3) ya Katiba hiyo inasomeka hivi: "  Mwanasheria Mkuu atakuwa ndiye mshauri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo ya sheria na, kwa ajili hiyo, atawajibika kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusu mambo yote ya kisheria, na kutekeleza shughuli nyinginezo zozote zenye asili ya au kuhusiana na sheria zitakazopelekwa kwake au atakazoagizwa na Rais kuzitekeleza, na pia kutekeleza kazi au shughuli nyinginezo zilizokabidhiwa kwake na Katiba hii au na sheria yoyote."

Tanzania ,Oktoba 25 Mwaka huu, itafanya uchaguzi Mkuu wa nafasi ya rais,Ubunge na udiwani. Hivyo Niliamua kumtafuta Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kwa mujibu wa Ibara hiyo ndiyo mwenye mamlaka ya kutoa ushauri wa kisheria kwa serikali ili aweze kutoa mwongozo kwa umma wa Watanzania hususani Wapiga kura wa fahamu ni Sheria zipi,Kanuni na Taratibu zitatumika na ni mambo gani hawataki kuyafanya wakishamaliza kupiga kura,mamlaka zipi zina jukumu la kusimami na Kuratibu uchaguzi, pamoja na kupata mtazamo wake kuhusu sintofahamu inayoendelea ya iwapo wananchi wanaruhusiwa, baada ya kupiga kura, kukaa mita 200 nje ya eneo la kituo cha kupigia kura ama la?


Jumapili iliyopita Mwanasheria Mkuu wa Serikali,George Masatu alikuwa mgeni rasmi Katika mahafali  ya kidato cha nne ambapo jumla a wanafunzi 49 walihitimu .

Mahafali hayo ni ya nane ya Patrick Mission High School,Jijini Dar Es Salaam ,na maadhimisho ya   Miaka Kumi ya tangu shule hiyo ilipoanzishwa na  katika  kipindi hiki jumla ya wanafunzi 602 wamemaliza kidato cha nne na wanafunzi 202 walihitimu kidato cha sita na Kuwa shule hiyo imetoa  mchango mkubwa kwa Taifa  kwa kutoa elimu kwa watoto hao kwani kimsingi jukumu hili ni la Serikali. 

Masaju alitoa hotuba yake kuhusu mahafali hayo pia alitumia muda huo kuzungumzia Sheria zinazotawa la Katika uchaguzi Mkuu ambapo alitaka wananchi wazi some  waielewe na wazitii na akasema jukumu la Mpiga kura ni kupiga kura na kuondoka sio kulinda kula.


Anasema huo utakuwa ni Uchaguzi Mkuu wa nne tangu nchi yetu ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1992. 

Na  Watanzania, Taasisi, dini na madhehebu mbalimbali kwa kuombea na kuhimiza umuhimu wa kudumisha amani katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu. 

Anasema Uchaguzi Mkuu ni Tukio la Kisiasa lakini kama zilivyo shughuli zote za Umma, linaratibiwa, kuendeshwa na kusimamiwa Kikatiba na Kisheria ili kuwezesha tukio hili muhimu kufanyika katika mazingira ya amani na utulivu na hivyo kuwa Uchaguzi huru na haki.  

Ndiyo maana mbali na Tume ya Uchaguzi ambayo ndiyo mamlaka inayoratibu kuendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu, kwa upande mwingine ipo Serikali ambayo ndiyo mamlaka inayoratibu na kusimamia udumishaji wa amani na utangamano katika Nchi  kwa kutekeleza ipasavyo jukumu lake la msingi la usimamizi wa utekelezaji wa sheria za Nchi.  

Kwa hiyo ni vyema tukafahamu kwamba hata katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu, kuna mamlaka ya usimamizi wa shughuli za Uchaguzi Mkuu (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) na Mamlaka ya Usimamizi wa amani na utangamano katika Nchi (Serikali).

Masaju anaeleza kuwa Moja ya mambo yanayoweza kutusaidia kutunza amani ya nchi yetu katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu ni kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na taratibu zinazoongoza uchaguzi huu, kwani zinaweka msingi mzuri kuhusu haki na wajibu unaopaswa kuzingatiwa na kila Mtanzania, Chama cha Siasa, Mgombea, Wakala wa Chama au Mgombea, Serikali na wadau wengine wote. Kila jambo na kila hatua katika uchaguzi mkuu, inaongozwa na Katiba na Sheria. Hakuna jambo lolote la Umma linalofanywa au kutekelezwa pasipo kuwekewa taratibu za kisheria.


Aidha anasema Msingi wa uchaguzi tunaofanya mwaka huu ni Ibara ya 21(1) inayoweka masharti kuwa kila raia anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika utawala wa nchi moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi, ninanukuu;

21.-(1) bila kuathiri masharti ya ibara ya 39, ya 47 na ya 67 ya Katiba hii na ya sheria za nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.”
Kutokana na masharti ya Ibara hii, ni wazi kuwa pamoja na kwamba kila mtu ana haki ya kushiriki katika uongozi wa nchi ama kwa kuchagua au kuchaguliwa, ushiriki wake unapaswa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Katiba pamoja na Sheria. Hapa mtaona kuwa kauli mbiu ya siku ya leo kwamba tufanye uchaguzi kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi ni ya kikatiba pia" anasema Masaju.

Masaju ambaye ndiyo aliyeipatia serikali ushindi katika Rufaa ya kesi ya maarufu ya mgombea binafsi mwaka 2010 katika Mahakama ya Rufaa nchini, anasema  Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano ya Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo yenye jukumu kuu la kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura pamoja na uendeshaji wa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. 

'Ni vizuri tukafahamu kuwa Tume ya Uchaguzi ni huru katika utekelezaji wa majukumu yake na hailazimiki kufuata amri ya mtu au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali, au maoni ya chama cha siasa kama inavyoelezwa katika Ibara ya 74(11) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, tuwe na imani na Tume yetu ya Taifa ya Uchaguzi. Tuipe ushirikiano na kufuata ipasavyo maelekezo tunayopewa na Tume hiyo' anasema.

Aeleza kuwa Mbali na Katiba ya Nchi, zipo sheria nyingine zinayoongoza uchaguzi ikiwa ni pamoja ni Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (The National Election Act),Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (The Local Authorities Elections Act),Sheria ya Gharama za Uchaguzi, (The Election Expenses Act), Sheria ya Vyama vya Siasa (The Political Parties Act), Sheria ya Kanuni za Adhabu (The Penal Code), Sheria ya Jeshi la Polisi (The Police Force and Auxiliary Services Act),Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (The Prevention and Combating of Curruption Act), Sheria ya Utangamano katika jamii (The Public Order Act), na Sheria ya Baraza la Taifa la usalama (The National Security Council Act).  Kwa sababu hiyo basi, tuzipatie ushirikiano Mamlaka za Serikali na Dola zenye dhamana ya kusimamia udumishaji wa amani, usalama na utangamano katika Nchi.

Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na Sheria ya Gharama za Uchaguzi zinaweka masharti kuhusu uandikishaji wa wapiga kura, uteuzi wa wagombea, matumizi ya fedha wakati wa kampeni, makosa ya jinai, makosa ya rushwa, kutangazwa siku ya uchaguzi, kujiondoa au kifo cha mgombea, kampeni, taratibu za uchaguzi na kutangaza matokeo na namna ya kupinga matokeo ya uchaguzi kwa upande wa uchaguzi wa wabunge na madiwani.

 Aidha sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Sheria ya Vyama vya Siasa inaelekeza kwamba huduma ya ulinzi na usalama katika mikutano ya Kampeni, vituo vya kupigia kura na mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa itaratibiwa na Jeshi la Polisi.


Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ambayo inaweka masharti kuhusu matumizi ya fedha wakati kampeni na uchaguzi wenyewe. Aidha, Sheria hii inadhibiti vitendo vilivyozuiwa (prohibited practices) ikiwemo rushwa wakati wa kampeni na uchaguzi.

Na Sheria ya Vyama vya Siasa inaweka masharti kuhusu usajili wa vyama vya siasa na namna vyama vya siasa vinavyotakiwa kutekeleza majukumu ambapo kuhusu mikutano ya hadhara ikiwemo ya mikutano ya kampeni za uchaguzi, kifungu cha 11 kinaelekeza kuwa mikutano hiyo ifanyike kwa kuzingatia masharti yaliyoko katika Sheria ya Jeshi la Polisi.

Kwa upande mwingine, Sheria ya Jeshi la Polisi katika kifungu cha 42 inaweka masharti yanayolipa Jeshi la Polisi mamlaka ya kutoa amri kuhusu mikusanyiko na maandamano katika sehemu za umma kwa kadri litakavyoona inafaa ili kutunza amani na utangamano katika jamii. 

Aidha, Sheria ya Jeshi la Polisi pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa zinaweka utaratibu wa watu na vyama vya siasa kufanya mikusanyiko au maandamano baada ya kutoa taarifa Jeshi la Polisi. 

"Kwa mujibu wa sheria hizi mbili, Jeshi la Polisi lina mamlaka ya kuzuia mkusanyiko au maandamano hayo iwapo litaridhika kuwa mkusanyiko au maandamano husika yanaweza kusababisha uvunjifu kwa amani. " anasema.

Sheria hii ya Jeshi la Polisi (the Police Force and Auxiliary Serice Act), inaweka masharti yanayolipa Jeshi la Polisi mamlaka ya kulinda amani na mtengamano katika jamii. Katika kuteleza jukumu hilo, Jeshi la Polisi limepewa mamlaka ya kuzuia mikusanyiko inayoweza kuhatarisha amani kama inavyoonekana katika kifungu cha 42 cha Sheria hiyo.

Pia kifungu cha 43 kinaweka masharti kuhusu watu au chama cha siasa kinachotaka kufanya mkusanyiko au maandamano kutoa taarifa na iwapo Jeshi la Polisi litaona kuwa mkusanyiko huo unaweza kuhatarisha amani, basi lina mamlaka ya kuzuia mkusanyiko au maandamano ambayo taarifa yake iliwasilishwa polisi.

Sheria ya Kanuni za Adhabu inaweka masharti kuhusu jambo ambalo mtu akilitenda linakuwa kosa la jinai na kuadhibiwa pale inapothibitika. Kufanya mikusanyiko isiyo halali, vurugu, uchochezi na kutokutii amri halali ni baadhi tu ya makosa ya jinai yaliyoko katika Sheria hii. Aidha, mtu anayeshiriki mkusanyiko ambao si halali anatenda kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 75 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.

Sheria ya Utangamano katika Jamii (The Public Order Act) inazuia kuanzishwa au uwepo wa kwa Vikundi vinavyojitwalia (usurp) mamlaka ya Jeshi la Polisi kusimamia Ulinzi wa amani na usalama katika Nchi. Sheria hiiyo inaweka masharti kuhusu kutunza amani na utangamano wakati wa mikutano ikiwemo kutobeba silaha katika Mikutano isipokuwa kama imeidhinishwa hivyo, na kutotumia meneno yanayoweza kuvuruga amani wakati wa mikutano.

Kwa upande wake Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa pia inatumika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa wakati wa shughuli zote zinazohusiana na Uchaguzi Mkuu.


Kwa kuwa siku ya Uchaguzi Mkuu ni maalum na mahususi kwa ajili ya kupiga kura, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inakataza katika kifungu chake cha 104 kufanyika kwa Mikutano au mikusanyiko siku hiyo au kufanya Mikutano ndani ya umbali wa mita 200 kutoka katika  kituo cha kupigia  kura ambacho pia ndicho kituo cha kuhesabia kura.  Hivyo hivyo Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nayo katika kifungu chake cha 103 inakataza kufanyika mikutano ndani ya umbali wa mita 300 kutoka chumba cha kupigia kura.  Sheria zote hizi mbili katika vifungu hivyo tajwa zinakataa mavazi, kuonyesha kadi yoyote, picha, upendeleo au nembo inayoonyesha kuunga mkono mgombea fulani katika uchaguzi.  

Kwa mujibu wa sheria hizi mbili za Uchaguzi watu wanaoruhusiwa kuwepo katika kituo cha kupigia kura ni msimamizi wa kituo, msaidizi wa upigaji kura, wakala, wa Mgombea, mpiga kura, msaidizi wa mpiga kura mwenye uhitaji maalum, mwangalizi wa Uchaguzi aliyeidhinishwa na Tume, mgombea, mjumbe wa Tume ya Uchaguzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Afisa wa Tume, Mratibu wa Uchaguzi wa Mkoa, askari polisi au mtu anayehusika na usalama kituoni, msimamizi wa uchaguzi na msaidizi wake. Watu hao pia ndio wanaoruhusiwa kuwepo wakati wa zoezi la kuhesabu kura isipokuwa mpiga kura au msaidizi wa mpiga kura.


Ndiyo maana kutokana na masharti haya ya kisheria, wananchi baada ya kupiga kura wanapaswa kurejea katika makazi yao kusubiria huko matokeo ya uchaguzi kwa kadri matokeo hayo ya uchaguzi yatakavyokuwa yanatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia Wasimamizi wa Uchaguzi au na Tume yenyewe  kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, watu wanaotaka kukusanyika nje ya umbali uliotajwa kwenye Sheria hiyo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi au Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sharti watambue kuwa kuna sheria nyingine za nchi zinazoweka utaratibu kuhusu namna ya kufanya mikutano au mikusanyiko.

Kama nilivyoeleza awali sheria mojawapo inayotumika wakati wa Uchaguzi ni Sheria ya Kanuni za Adhabu ambayo katika kifungu cha 74 inaweka masharti kwamba pale watu watatu au zaidi wanapokunyika wakiwa na lengo linalofanana na wakawa katika hali inayosababisha watu wengine walio jirani kuogopa kuwa watu hao waliokusanyika wanaweza kuvuruga amani au wanaweza kusababisha watu wengine kuvuruga amani basi wanafanya mkusanyiko ambao si halali (unlawful assembly).

Ni katika muktadha huu ndipo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Kiongozi  wa Serikali, Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu anapokuwa na haki ya kutoa maelekezo kuhusu udumishaji wa amani, usalama na utangamano katika Nchi hata wakati wa Uchaguzi Mkuu kwa kuwa ni jukumu la Serikali kusimamia utekelekezaji wa sheria ili kudumisha amani, usalama na utangamano katika Nchi.

Ninapohitimisha ninaomba kwa mara nyingine tena niwakumbushe na kuwashauri kwamba shughuli zote za Umma huratibiwa, kuendeshwa, kusimamiwa, kuongozwa na kutawaliwa na Katiba na Sheria za nchi.  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ibara yake ya 26 inaelekeza kwamba kila  mtu ana wajibu wa kuifuata na kutii Katiba hiyo na sheria za Jamhuri ya Muungano na kwamba kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria kuchukua hatua za  kisheria kuhakiksiha hifadhi ya Katiba na Sheria. Ni kutokana na hali hiyo ndipo tunapokuwa na dhana ya Utawala wa Sheria (Rule of Law) katika misingi ya Utawala Bora.

Na kwa kuwa Serikali ndiyo mwenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria, ndipo Mwalimu Nyerere alipotufundisha  kwamba “Serikali ni sheria.  Hakuna kitu kinaitwa Serikali bila Sheria na Sheria zikishatungwa lazima zifuatwe”

Masaju anawaomba  Viongozi wa dini wawakumbushe    waumini wao kurejea maelekezo ya Mwenyezi Mungu katika Warumi 13:1-6 kuhusiana na  umuhimu wa kuitii Serikali inapokuwa inatekeleza  jukumu lake la kusimamia udumishaji wa amani, usalama na utangamano katika Nchi. 

"Ninawashauri na kuwakumbusha Watanzania wote umuhimu wa kuendelea kuzingatia na kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kutii Sheria na mamlaka ya Nchi (serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) bila shurti." anasema Masaju ambaye amewahi Kuwa Mshauri wa Rais Jakaya Kikwete Kwenye masuala ya Sheria.

Ninaomba na kushauri tuendelea kumwomba Mungu ili Uchaguzi Mkuu 2015 ufanyike kwa amani na sisi wenyewe kila mmoja wetu tuchukue hatua kwa vitendo ipasavyo kuwezesha Uchaguzi Mkuu kufanyika kwa amani ipasavyo  kwa kuzingatia Katiba, na Sheria zinazosimamia Uchaguzi na sheria zinazosimamia udumishaji wa amani, usalama na utangamano katika Nchi yetu.  

Kwa kuwa Tanzania ni yetu wote, tudumishe amani, tufanye uchaguzi wetu kwa kufuata Katiba na sheria za Nchi yetu.  Hatua hiyo inawezekana kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake ipasavyo.

Facebook: Happy Katabazi
20/10/2015No comments:

Powered by Blogger.